May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mto Msimbazi Dar kuanza kujengwa Julai 2022

Bonde la Mto Msimbazi

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imesema, mradi wa ujenzi wa Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam unatarajia kuanza Julai 2022. Anaripoti Helena Mkonyi, (TUDARCo) … (endelea).

Ni baada ya majadiliano ya mapendekezo ya awali kati yake na Benki ya Dunia (WB) kufanyika Desemba 2021.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Tamiasemi, David Silinde wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba.

“Je, ni lini Serikali itaanza kazi ya ujenzi wa Mradi wa Mto Msimbazi ambao umetajwa
katika Bajeti ya Mwaka 2021/22,” ameuliza Tarimba

Akijibu swali hilo, Silinde amesema, “Serikali na Benki ya Dunia inatarajia kufanya majadiliano mapendekezo ya awali ya mradi Desemba 2021 na kusaini mkataba mkopo wa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 120 ifikapo Machi 2022 na utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza Julai, 2022, baada ya kukamilisha masharti yote ya kutekeleza mradi wa mto Msimbazi.”

Amesema, mradi huo kwa sasa upo katika hatua za maandalizi ambapo usanifu wa miundombinu husika pamoja na nyaraka muhimu kwa ajili ya masuala ya mazingira na fidia zinaandaliwa.

Amesema “mradi huo wa Mto Msimbazi ni kwa ajili ya kukabiliana na mafuriko katika bonde la mto Msimbazi.’’

Aidha, Silinde amesisitiza mradi huu utahusisha ujenzi na wa Daraja la Jangawani lenye urefu wa mita 390, upanuzi wa mto kwa upande wa chini kuanzia Barabara ya Kawawa hadi Daraja la Salenda ili kuruhusu maji kwenda baharini kwa haraka kipindi cha Mvua.

Amezungumzia suala la uimarishaji wa kingo za Mto Msimbazi maeneo ya Tabata Kinyerezi jijini Dar es Salaam ili kuzuia mmonyoko wa udongo katika maeneo yote yanayozungukwa na mto huo.

Silinde amesema, ujenzi wa vitega mchanga na vituo vya kuhudumia mto Msimbazi kwa ajili ya kuzuia kiasi cha mchanga kinachotuama eneo la chini la mto huo ujenzi wa matuta kuanzia Daraja la Salender hadi barabara ya Kawawa yatakayoruhusu matumizi mbalimbali ya ardhi maeneo ya Mchikichini, Sunna na Hananasif’’

Akiuliza maswali ya nyongeza, Tarimba amesema, mto Tenge na Kibangu sambamba na mto Msimbazi maji huwa mengi je, serikali inampango gani wa kupeleka wataalamu ili mto Kibangu upeleke maji Msimbazi na lini naibu waziri huyo, Silinde atakwenda kuutembelea ili kujionea hali halisi?

Akijibu maswali hayo, Silinde ambaye pia ni mbunge wa Tunduma amekubali kupeleka wataalamu kwenda kuangalia jinsi ya kutatua changamoto hiyo na kuahiti mara baada ya kumalizika kwa mkutano huu wa Bunge atafanya ziara kwenda kuona mto huo.

error: Content is protected !!