April 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Madiwani ACT-Wazalendo waapishwa, wabunge wamfuata Ndugai

Spread the love

MADIWANI wa Chama cha ACT-Wazalendo, wameanza kuapishwa leo Jumatatu tarehe 14 Desemba 2020 huku wabunge wateule wakiwa kwenye maandalizi ya kuelekea Dodoma kwa ajili ya kuapishwa. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam…(endelea).

Arodia Peter, ofisa habari wa chama hicho akizungumza na MwanaHALISI Online leo Jumatatu amesema, tayari baadhi ya madiwani wa chama hicho, wameanza kuapa na kwamba, wataendelea kuapa sehemu zote.

“Wabunge wetu wapo kwenye maandalizi lakini nikueleza kwamba, madiwani wetu wameanza kuapa leo. Kwa mfano; Mkoa wa Mara leo ndio wameapishwa,” amesema Arodia.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 20920, ACT-wazalendo ilishinda majimbo manne ambayo ni; Hatibu Said Haji (Konde), Salum Mhamed Shafi (Chonga), Omar Ali Omar (Wete) na Khalifa Mhamed Issa wa Mtambwe wote kutoka Pemba visiwani Zanizbar

Ado Shaibu ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho, amesema wateule wa chama hicho wana baraka zote kutoka katika chama hicho na kwamba, wapo kwenye maandalizi ya kutekeleza takwa la kisheria la kuapishwa.

Hatua ya chama hicho kutoa wito kwa madiwani wake kuapa, wabunge kumsaka Spika Ndugai na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kuhudhuria vikao, kumekuja takribani wiki sita, tangu kiongozi mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, kuutangazia ulimwengu kuwa chama chake, hakitambui matokeo ya uchaguzi na uchaguzi wenyewe.

Alisema, “hatutambui uchaguzi huu na hivyo, hatututarajii kupokea hivyo viti vya ubunge na udiwani walivyotupa. Wananchi wasitarajie hata madiwani wetu na wabunge, kushiriki vikao vya madiwani na Bunge.”

Ado ametoa kauli hiyo iliyotanguliwa na wito wa Job Ndugai, Spika wa Bunge aliyoitoa hivi karibuni akiwataka wabunge wateule wa chama hicho kwenda kuapishwa.

“Nitoe wito kwa wabunge wengine wowote wale, nafikiri kumbukumbu zangu zinanionesha kwamba tuna wabunge wanne wa ACT-Wazalendo ambao bado hawajaapa,” alisema Spika Ndugai baada ya kumuapisha mbunge mteule na Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya

Ado amesema, wabunge wateule wa chama hicho wanakamilisha taratibu za kufika Dodoma na kuapa ili waanze kuwatumikia wananachi walioonesha matumaini kwao.

Maalim Seif Sharrif Hamad Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa

“Tayari wateule wote wanne wamepata baraka za chama, wanakwenda kuapishwa ingawa mpaka sasa ratiba ya siku ya kuapishwa haijawekwa,” amesema Ado na kuongeza:

“Ni jambo la kujivunia ndani ya chama chetu kutokana na wanachama wetu kuwa watulivu, hawakuwa na pupa na ndio maana tumeweza kufikia muafaka kwa maslahi ya wananchi, Zanzibar na chama chetu. Tumeumizwa lakini ilikuwa ni lazima kuamua.”

Amesema, wateule hao walizuiwa kuendelea na mchakato kutokana na uamuzi wa chama hicho kutokuwa tayari kushiriki mpaka pale vikao vya ndani vitakapofanyika.

“Tulipokutana, uamuzi wetu ulizingatia zaidi maslahi ya wananchi, tuliumizwa na tunandelea kusisitiza kwamba hatukuridhishwa na kile kilichofanyika kwenye uchaguzi mkuu.

“Tumewapa ujumbe wateule wetu kwenda kuonesha nguvu ya upinzani bungeni bila kujali uchache wao. Tunaamini endapo watasimama na hoja za wananchi, wananchi watawaunga mkono.”

error: Content is protected !!