December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Agizo la Magufuli lamng’oa kigogo wa madini

Waziri wa Madini, Dotto Biteko

Spread the love

DOTTO Biteko, Waziri wa Madini nchini amemvua madaraka Paul Gagala, Mwenyekiti wa Soko la Madini Wilaya ya Chunya sambamba na kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa Tume ya Madini wilayani Chunya, Mbeya. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Watumishi hao wa sekta ya madini wamesimamishwa kazi leo Jumatatu tarehe 14 Desemba 2020, baada ya Biteko kufanya ziara kisha kuzungumza na wachimbaji wadogo wa madini wilayani humo.

Biteko amewasimamisha kazi watumishi hao ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizokuwa zinawakabili, za utoroshaji madini gramu 15.4 yenye thamani ya Sh. 1.8 Bilioni.

Sambamba na hilo, Biteko ameagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kuwakamata watu 17 ambao ni wauza madini wa majumbani.

Kufuatia sakata hilo, Biteko amefuta leseni sita za wanunuzi wa madini ya dhahabu, pamoja na kuagiza uongozi wa Wilaya ya Chunya kufanya usajili wa mihalo ya uchenjuaji wa dhahabu kuanzia leo tarehe 14 Desemba 2020.

 

Biteko amechukua hatua hiyo akitekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuitaka Wizara ya Madini idhibiti utoroshwaji wa madini.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo tarehe 9 Desemba 2020, wakati akiwaapisha mawaziri 21 na manaibu waziri 23, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Wakati akimwapisha Biteko kuendelea kuwa waziri wa madini, Rais Magufuli alimsifu waziri huyo kwa kazi kubwa aliyoifanya ikiwemo kuongeza mapato katika baraza iliyopita, na kumuagiza aongeze juhudi katika kudhibiti mianya ya utoroshaji madini.

Katika baraza la mawaziri lililopita, Biteko alikuwa Waziri wa Madini.

error: Content is protected !!