May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Madaktari: Kuna ongezeko la wagonjwa, watahadharisha

Spread the love

 

CHAMA cha Madaktari nchini (MAT), kimewataka wananchi kuwa makini kutokana na ongezeko la wagonjwa wenye matatizo ya kupumua. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumatano tarehe 15 Februari 2021 na Dk. Shadrack Mwaibambe, Rais wa MAT, huku akisisitiza madaktari kutowabagua wagonjwa wakati wanapowapatia huduma za afya.

“Pamoja na kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wenye changamoto hii ya upumuaji, madaktari tuzingatie kiapo cha taaluma yetu.

“Tuendelee kuwahudumia wagonjwa bila kujali rangi zao, kabila au aina ya ugonjwa walionao huku tukizingatia hatua za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza,” imeeleza taarifa ya Dk. Mwaibambe.

MAT wameungana na viongozi wa dini pia wanasiasa wakiwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.

Tayari baadhi ya viongozi wa dini wamewataka waumini wao, kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa hayo ikiwemo corona (COVID-19).

Dk. Mwaibambe ameshauru wananchi na madaktari wenzake kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi magonjwa hayo.

Taarifa ya Dk. Mwaibambe imeeleza, wamebaini ongezeko la wagonjwa wenye changamoto ya upumuaji.

“MAT kama mdau mkubwa wa sekta ya afya nchini, kimebaini ongezeko la wagonjwa wenye changamoto ya upumuaji katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ambao umegusa hisia za watu wengi.

“Pamekuwa na maelezo kwa viongozi wa Wizara ya Afya na wadau mbalimbali juu ya ugonjwa huu. Chama kinapenda kuwaeleza wanachama wake pamoja na watu wote wenye mapenzi mema na sekta ya afya na taifa letu kwa ujumla kuchukua tahadhari,” imeeleza taarifa ya Dk. Mwaibambe.

Hata hivyo, taarifa ya Dk. Mwaibambe imesema, changamoto ya upumuaji si ugonjwa, bali ni dalili ya ugonjwa.

Taarifa hiyo imewataka wadau wote kushirikiana katika kudhibiti magonjwa yanayosababisha changamoto ya upumuaji ikiwemo Neumonia, pumu na magonjwa ya moyo.

“Changamoto ya upumuaji siyo ugonjwa bali ni dalili ya ugonjwa. Changamoto ya upumuaji inaweza kuwa Neumonia, Pumu, COPD, Magonjwa ya Moyo, hatua za mwisho za mgonjwa kabla håjafariki au COVID -19.

“MAT  kinasisitiza kwamba udhibiti wa ugonjwa unaosababisha changamoto ya upumuaji ambao ni wa mlipuko, ushirikishe wadau wote,” imeeleza taarifa hiyo.

Chama hicho kimewasisitiza Watanzania kuepuka mikusanyiko, kuvaa barakoa na kufuata miongozo mingine inayotolewa na Wizara ya Afya.

“MAT kinawasisitiza wananchi wote kwa ujumla kuondoa hofu, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono, kuvaa barakoa.

“Kwenye misiba watu wawe wachache na kuzingatia maelekezo mengine yote yanayotolewa na Wizara pamoja na wadau wengine wa afya,” imesisitiza taarifa yake.

error: Content is protected !!