December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif awatia ‘ndimu’ Wazanzibari

Maalim Seif Shariff Hamad

Spread the love

MAALIM Seif Shariff Hamad, anaendelea kukaza ‘msuli’ dhamira yake ya kuichomoa Zanzibar katika mikono ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Jabir Idrisa, Zanzibar…(endelea).

Mwansiasa huyo nguli ambaye sasa ni Mshauri wa Chama cha ACT Wazalendo, amesema jambo ambalo litawezesha kutimia lengo hilo ni mshikamano kwa Wazanzibari.

Akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kutwa moja ndani ya Jimbo la Kijini, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja mwishoni mwa wiki, Maalim Seif aliendeleza kampeni yake ya kuwaunganisha Wazanzibari.

Katika maelezo yake, anatanabahisha kuwa umoja na mshikamano ndio silaha pekee ya kushinda mbinu za kuipoteza Zanzibar, nchi iliyokuwa huru na akiwa na kiti chake Umoja wa Mataifa, New York.

Amedai, CCM kinatumia mbinu nzito zikiwemo za mabavu na ulaghai ili kuendelea kushikilia hatamu za uongozi.

Maalim Seif amesema, mfano mzuri ni mfumo wa ubaguzi katika kutoa ajira na fursa nyegnezo za kiuchumi. Pia utaratibu wa kutoa kitambulisho cha Mzanzibari.

Kuhusu kitambulisho amesema, kilipotolewa kwa mara ya kwanza wakati wa uongozi Amani Abeid Karume kiliitwa Kitambulisho cha Mzanzibari, lakini sasa kineandikwa Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Maana yake nini, anauliza umma wa kijijini Mbuyutende Matemwe na Shangani “Kwamba wewe Mzanzibari kindakindaki ni sawa tu na mtu yeyote akiyetoka huko na kuamua kukaa Zanzibar. Nyote mnapewa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi. Huku ni kuipoteza nchi yetu Zanzibar,” alisema.

Anasema, “wanalenga ifike wakati idadi ya wageni iwe kubwa ya kutufunika sisi wenyewe, ili kupata ushindi watakapokuja kuitisha kura ya maoni kuuliza wanaoutaka Muungano,” alisema.

Alitoa mfano wa Fiji ambako kulikuwa na mfumo wa kuingiza wageni kimkakati, na mwisho kuja kumpata kiongozi mgeni asiyekuwa raia halisi.

“Utakapokuja uchaguzi. Kama utakuwepo uchaguzi, hakuna kususia. Tutaingia kwa nguvu zote ili kuendelea kudhihirishia ulimwengu kuwa CCM haitakiwi tena na umma. Tuwaoneshe kuwa wanaongoza bila ya ridhaa ya wananchi,” alisema.

Anasema, yeye na wengi wa Wazanzibari hawapingi Muungano isipokuwa siku zote kilio chao ni Muungano wa haki, utakaoiweka Zanzibar na mamlaka yake kamili ili ipange maendeleo ya watu wake.

Amesema, ni udhalimu kuichukulia Zanzibar kwa udogo wake, maana kama nchi hupimwa kwa udogo wake, basi China yenye watu zaidi ya bilioni moja ingekuwa na viti zaidi ya Burundi.

“Zanzibar ilijiunga na Tanganyika ikiwa nchi Huru sawa na mwenzake… kuichukulia kuwa nchi ndogo na kuikandamiza ni udhalimu mkubwa dhidi ya watu wake, na hicho ni kitu kisichokubalika kabisa,” alisema.

Katika ziara yake hiyo, alikabidhi kadi ya ACT Wazalendo kwa wanachama wapya 300 wakiwemo waliokuwa CCM na CUF. Alisema “ile CUF iliyokuwa na sisi, si hii ya sasa ambayo inashirikiana na madhalim wanaotukandamiza.”

Maalim Seif alianza ziara yake kwa kukagua eneo la ufukwe la Muyuni katika kijiji cha Mbuyutende, kujionea namna serikali ilivoruhusu kifisadi wawekezaji wageni kuhodhi eneo la wananchi linalotumiwa kama makaburi tangu enzi na dahari.

Wazee wa kijiji hicho wamelalamika kupuuzwa haki yao, na kudharauliwa utamaduni wao wa kuzikana eneo ambako baba na babu zao walizikwa.

Walimwambia Maalim Seif kuwa, wamepitia ngazi mbalimbali za serikali katika kueleza malalamiko yao na mara moja alifika Balozi Seif Ali Iddi na kuahidi kuwa eneo la wananchi halitaguswa lakini sivyo ilivyo.

error: Content is protected !!