December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu: Utawala huu umenifikisha hapa

Tundu Lissu, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, akirudisha fomu ya kuteuliwa nafasi hiyo kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage

Spread the love

TUNDU Lissu, mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameeleza kwamba, utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, umemsukuma kugombea urais. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa chama hicho amesema, kilichotokea katika kipindi cha miaka mitano ya serikali hiyo, kimeimarisha zaidi tamaa yake ya kugombea urais, na sasa anagombea.

Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 cha ITV tarehe 3 Septemba 2020 amesema, maendeleo ya nchi sio kuwa na barabara tu, bali uhuru, haki na maendeleo ya watu.

“Katika mazingira ya kawaida, si jambo la ajabu kwa mtu yeyote yule ambaye ni mzalendo wa nchi yake kutaka kuwa kiongozi wa hiki au kile.

“Kuna nafasi nyingi za uongozi, urais ndio nafasi ya juu ya uongozi, kama mwananchi nilikuwa nafikiria kwamba nina uwezo kiasi gani wa kuwa rais wa nchi hii.

“Lakini katika kipindi hiki cha miaka mitano, nilichokuwa nafikiria juu juu, kimekuwa wazi zaidi na imara zaidi kwa sababu ya yale ambayo tumeona kwa miaka mitano, haki haikutendeka,” amesema Lissu.

Katika mahojiano hayo, Lissu amesema Ilani ya Uchaguzi ya Chadema inasisitiza Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watu, hivyo endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, atairudisha nchi katika misingi hiyo.

“Tunapozungumzia maendeleo ya watu, haiwezi kuwa ya barabara tu kama watu wenyewe hawatendewi haki, sisi watu huru ndio maana tumesema katika kauli mbiu yetu ni haki na maendeleo ya watu,” amesema Lissu.

Ameahidi kufumua taratibu za kujitawala ili wananchi wawe na nguvu ya kujitafutia maendeleo wenyewe badala ya kuitegemea serikali.

“Bado unaona kwamba watu wanahofu na serikali, ukifanya hivi lazima uangalie nyuma serikali itafanya nini, sasa unapambanaje na umasikini, ujinga na maradhi wakati kila mtu anasema serikali  itusaidie kila kitu.

“Lazima tufumue taratibu za kujitawala na kuendesha nchi ili watu waweze kupumua, wajenge mashule wafanye shughuli za maendeleo yao,” amesema Lissu.

Apia ameibua machungu ya wananchi waliobomolewa nyumba zao katika Barabara ya Morogoro, hasa maeneo ya Kimara.

Amesema, haikuwa sahihi na kwamba, kulikuwa na njia mbadala za kushughulikia suala hilo bila kubomoa nyumba hizo.

“Kuna kazi kubwa sana imefanyika ya kujenga miundombinu, barabara ya Morogoro mpaka Kibaha yaani eneo ambalo barabara inajengwa zamani ilikuwa makazi ya watu kwa maelefu ambao wamebomolewa nyumba zao.

“Ndio barabara nzuri lakini ina maana gani kwa maelfu ya watu ambao unavunjia vitega uchumi vyao na maisha yao, maendeleo haiwezi kuwa barabara, lazima iwe barabara inayosaidia watu ambao wanabomolewa,” amesema Lissu.

Aidha, Lissu ameahidi kurudisha Uhuru wa Watu, hususan wa vyombo vya habari, taasisi binafsi na za kidini.

“Tutarudisha uhuru wa wananchi ambao umepotea kipindi hiki, tutarudisha uhuru wa vyombo vya habari,  uhuru wa wananchi kukosoa na kuisema serikali, kuwasema vibaya ni tendo la kidemokrasia.

“Tutarudisha uhuru wa wanahabari kuandika habari zote, tutarudisha uhuru wa vyombo vya uwakilishi, uhuru wa taasisi za dini kufanya shughuli zao, uhuru wa taasisi za kiraia,” amesema Lissu.

Amehoji kwamba, ulalamikaji na ukosoaji shida yake nini? Na kwamba kama kuna jambo linahitaji kulalamikiwa ambalo linatendeka, ni sawa mtu akilalamika.

“Mimi nafikiri uhuru wa kuzungumza ni pamoja na uhuru wa kulalamika pale unapoona mambo hayatendeki sawa sawa. Uhuru ni pamoja na kukosoa pale panapo hitaji kukosolewa,” amesema.

error: Content is protected !!