Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu anusurika kukamatwa
Habari za SiasaTangulizi

Lissu anusurika kukamatwa

Kutoka kushoto, Jabir Idrissa, Mhariri wa Mawio, Simon Mkina, Mhariri na Mmiliki wa gazeti la Mawio na Tundu Lissu walipokuwa mahakamani katika kesi ya uchochezi kupitia gazeti la Mawio
Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imekataa ombi la serikali kutaka itolewe hati ya kukamatwa mwanasiasa wa upinzani nchini, Tundu Lissu, kwa kuendelea kutofika mahakamani kwa ajili ya kesi inayomhusu akiwa ni mshitakiwa wa nne. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba, wakili wa serikali, Simon Wankyo aliomba mahakama itoe hati ya kukamatwa Lissu kwa kuwa si mgonjwa bali ni mshitakiwa anayezunguka nchi mbalimbali na kutoa maneno ya kisiasa dhidi ya serikali.

Wakili Wankyo alieleza kuwa Lissu hayuko nje ya nchi kwa matibabu isipokuwa anasema maneno na watu wanayasikia na dunia inajua.

Hakimu Simba alikataa kutoa hati ya kukamatwa Lissu lakini akawaonya wadhamini wake, Ibrahim Ahmed na Robert Katula kuwa wamekosea kutofika mahakamani wakati kwa muda mrefu mshitakiwa waliyemdhamini amekuwa hafiki.

“Nawaonya wadhamini kwamba si utaratibu wa mahakama huo wa kutofika mahakamani wakati mnajua kwa muda mrefu mshitakiwa hayupo kwa sababu ambazo hatuna sababu za kubishana nazo hapa… mnatakiwa lazima mtimize wajibu wenu wa kufika hapa kila kesi inapotajwa. Hii mahakama haichukui habari za kusikia ndio maana tunataka kuweka rekodi ili zenyewe ziseme,” alisema Hakimu Simba.

Hakimu Simba alitoa msimamo huo baada ya kuwasikiliza wadhamini hao ambao waliitwa kwa amri yake siku ya Februari 4 mwaka huu ili waje kueleza sababu za Lissu kuendelea kutofika mahakamani. Ibrahim aliiambia mahakama kuwa hakuwa anafika mahakamani kwa sababu baba yake mzazi amekuwa mgonjwa kiasi cha kumkwamisha kutimiza wajibu wake.

Akizungumzia hali ya Lissu, alieleza kuwa bado yuko matibabuni nchini Ubelgiji ambako tarehe 20 mwezi huu wa Februari alifanyiwa operesheni ya 23. Alieleza kuwa amemjulisha kuwa atarudi nchini mara tu atakapopona na kupata ruhusa ya madaktari wanaomtibu. Ibrahim aliomba radhi mahakama kwa kutofika mahakamani kwa muda mrefu kesi inapotajwa na kuahidi kuanzia sasa atatimiza wajibu wake wa kisheria ipasavyo.

Katula, Meneja Mkuu wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL) ambayo ikisambaza gazeti la MAWIO, ambalo makala iliyochapishwa ndiyo iliyotumika kuwafungulia mashitaka Lissu na wenzake watatu, aliomba msamaha kwa mahakama kwa kushindwa kufika wakati kesi inapotajwa. Naye aliahidi kutimiza wajibu wake wa kisheria ipasavyo.

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), anashitakiwa pamoja na Simon Mkina, mhariri mkuu wa gazeti la MAWIO; Jabir Idrissa, mwandishi wa gazeti hilo na Ismail Mahboob, meneja wa kiwanda cha uchapishaji magazeti cha Flint cha jijini Dar es Salaam.

Washitakiwa hao wa kesi Na. 208 ya mwaka 2016, wanakabiliwa na mashitaka matano yanayohusu kula njama na kuchapisha makala za uchochezi dhidi ya serikali kupitia makala iliyochapishwa katika toleo Na. 182 la tarehe 14-20 Januari 2016. Makala hiyo ilikuwa na kichwa cha habari “Maafa yaja Z’bar.”

Maelezo waliyoyatoa wadhamini wa Lissu hayakumridhisha wakili wWakili wa Serikali ndipo akaiomba mahakama itoe hati ya kumkamata.

Lissu amekosa kufika mahakamani tangu aliposhambuliwa kwa risasi akiwa mjini Dodoma ambako alikuwa anajhudhuria mkutano wa Bunge. Hiyo ilikuwa ni Septemba 7, mwaka 2017; na kulazimika kupelekwa jijini Nairobi, Kenya kwa matibabu ya kitaalamu zaidi baada ya kuwa amepatiwa matibabu ya dharura kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Baadaye kwenye Novemba mwaka 2017 alipelekwa nchini Ubelgiji ambako anaendelea na matibabu ya kitaalamu ya kiwango cha juu zaidi.

Lissu alishambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana.” Shambulio dhidi ya Lissu, lilifanyika wakati anawasili nje nyumbani kwake, eneo la Area D mjini Dodoma, akiwa ndani ya gari lake wakati akitokea bungeni.

Kesi iliahirishwa mpaka Machi 25 itakapotajwa tena.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!