Tuesday , 18 June 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi “Haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa.”
Makala & UchambuziTangulizi

“Haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa.”

Nyundo ya Hakimu
Spread the love

NI wachache kati ya wananchi wanaokuwa kwenye ukumbi wa mahakama huendelea kutarajia kusikia hukumu ya kesi wanayoifuatilia baada ya kumuona asiyekuwa jaji msikilizaji ndiye anaketi kitini. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Nyoyo za wengi wa wale wanaojazana mahakamani hupata sononeko kwa sababu watu wanaanza kuzoea sasa utaratibu unaoharibu dhana ya upatikanaji wa haki kupitia mahakama – mhimili mmojawapo wa dola.

Inazoeleka kwenye mahakama za Tanzania kusikia hukumu ya kesi imeahirishwa kwa sababu hii au ile na wananchi waliofika wakiwemo wadai na wadaiwa, kulazimika kusubiri siku itakayopangwa tena.

Moja ya sababu hizo za kuahirishwa kwa utolewaji wa hukumu mara kadhaa huwa ni “Jaji anayeisikiliza kesi amepangiwa majukumu mengine.”

Baadhi ya wakati, maelezo hayo ya sababu za kuahirishwa hukumu, hutolewa kwenye ofisi ya msajili kwa kukaribisha tu mawakili wahusika wa kesi pamoja na wanaowawakilisha.

Bali hutokea msajili akatoka ofisini na kwenda ukumbi wa mahakama ili kutoa maelezo ya “dharura” iliyompata jaji wa kesi husika na pendekezo la kuahirishwa hadi siku nyingine.

Nani ukiacha huyu msajili wa mahakama na jaji mwenyewe anayejua kwa uhakika uthabiti wa kilichopo nyuma ya pazia. Si aghlabu kuhoji mazingira kama haya na sababu kubwa hapa ni kuiheshimu tu mahakama.

Lakini je, ni halali kila wakati kutohoji utaratibu huu wa hukumu kuahirishwa mara moja, mbili au hata tatu na sababu ikawa ni dharura ya jaji ya “amepangiwa majukumu mengine” au “hajakamilisha kuiandaa hukumu?”

Hiyo tuseme ni haki ya upande huo wa watendaji wa mhimili wa mahakama. Iko wapi haki ya upande wa umma, wakiwemo wahusika wakuu katika kesi husika?

Umuhimu wa swali hili unazingatia hasa mambo mawili: Wajibu wa Mahakama kutoa haki na (ikiwezekana) kwa haraka na pili, uhalali wa kuitegemea mahakama yenyewe na iliyo pekee katika jukumu la utoaji wa haki.

Sikusudii kuihoji mahakama. Hata kidogo. Ninajisikia wajibu wa kizalendo wa kutoa mchango kwa nia nzuri ya kusaidia hilo jukumu la mahakama kutoa haki – ambalo ni la kikatiba – kutekelezwa kwa ufanisi unaoonekana.

Umuhimu wa haki kupatikana kwa haraka na utaratibu wa hiyo haki kufikiwa kuonekana hasa unatumika, umeelezwa kwa ufasaha na rais wa chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Amani Karume katika hotuba yake ya Siku ya Sheria mapema mwezi huu.

Wakili huyu wa Mahakama Kuu nchini alijenga hoja yake kwa kuielezea kesi inayohusu mirathi ya familia ambayo hakuitaja bayana, na namna ilovyochukua mlolongo mrefu hadi baadhi ya warithi kupoteza maisha.

Pale jaji anayesubiriwa kutoa hukumu ya kesi – iwe iliyokuwa na mvuto mkubwa machoni pa watu au kinyume chake – anapokosa kukidhi matarajio ya wahusika kwa kisingizio cha “kupangiwa majukumu mengine” au “sijamaliza kuandaa” hauna maana sana kwa watu.

Ni afadhali jaji apange muda mrefu wa kujiandaa kuandika hukumu kuliko kuiahirisha mara kadhaa kwa sababu hizo. Ushauri huu una mantiki hasa kesi zinazosubiriwa hukumu zinapohusu maslahi makubwa ya jamii iwe kisiasa au kiuchumi.

Hivi amefikiria usumbufu wanaoupata waliotarajia hukumu? Anachukuliaje wale wananchi walioamka alfajiri na kuanza safari ya kwenda mahakamani katikati ya jiji la Dar es Salaam, kwa mfano, kufuatilia hukumu ya kesi?

Analipaje usumbufu unaotokana na watu hao kugharamika kifedha kufunga safari ya kufika mahakamani?

Lakini lililo muhimu zaidi huyu jaji anadhani ni kwa kiasi gani ametimiza wajibu wake wa kuihakikisha haki kwa wakati; na hivyo kuwa amezingatia ule usemi wao wanasheria kwamba haki si tu ipatikane bali ionekane hasa inatopatikana.

Ni kwa njia hii watendaji hawa wa mahakama watakuwa wanachangia kuijengea heshima mahakama katika jukumu lake la kikatiba la kutoa haki. Ikumbukwe haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa.

Majaji na mahakimu wanao wajibu huu na inafaa kuelewa kuwa wanatekeleza jukumu muhimu la kutoa haki kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wake.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mazingira magumu ya JPM yamechangia ‘Comedy Journalism’

Spread the loveMwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia hali ya uchumi wa vyombo...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

RC Chalamila: Nimeacha ubabe

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chamalila amemthibishia...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Rais Samia amng’oa Matinyi Maelezo, ateua viongozi mbalimbali

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwamo...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

error: Content is protected !!