March 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

LHRC yafichua madudu mengine

Spread the love

MATOKEO ya ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara ya mwaka 2017 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) yamebainisha kwamba kutoshirikiswa kwa wananchi katika mchakato wa utwaaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji kumepelekea uwepo wa migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea) .

Akielezea matokeo ya Ripoti hiyo iliyozinduliwa leo tarehe 16 Agosti, 2018 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Wakili Anna Henga, Mratibu Msaidizi wa Haki za Binadamu na Biashara, Tito Magoti amesema wawekezaji wengi huchukua maeneo makubwa pasina kuyatumia kitendo kinachosababisha wananchi kuanzisha migogoro.

Wakili Magoti ametaja baadhi ya mikoa yenye migogoro hiyo ikiwemo mkoa wa Manyara, Kilimanjaro hasa Wilayani Moshi na Musoma ambapo utafiti wao ulibaini kwamba wawekezaji wengi hawayatumii maeneo kitendo kinachonyima fursa wananchi wa eneo husika kuyatumia.

“Wawekezaji hupewa maeneo makubwa huku wananchi wakizuiwa kutumia maeneo wanayoshindwa kuyatumia. Vile vile utafiti umebaini kwamba wananchi hawashirikishwi katika mchakato wa ugawaji wa ardhi kwa wawekezaji kitendo kinacholeta migogoro,” amesema Magoti.

Kufuatia matokeo hayo, Magoti ameitaka serikali hasa serikali za mitaa kuwashirikisha wananchi wakati wa mchakato wa utwaaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji ili kuondoa migogoro isiyo na lazima.

Kuhusu matokeo ya ripoti hiyo, yamebainisha kwamba asilimia 64 ya wanajamii walioshiriki katika utafiti huo walidai kwamba wawekezaji hawakuwaruhusu wanakijiji kutumia sehemu ya ardhi hiyo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi wakati asilimia 8 walikiri kuruhusiwa huku asilimia 28 wakisema hawajui.

error: Content is protected !!