Tuesday , 16 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Mwl. Nyerere: Najua mtapata shida
Makala & UchambuziTangulizi

Mwl. Nyerere: Najua mtapata shida

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Spread the love

MANENO ya mwisho ya Mwalimu Julius Nyerere ambapo yaliyopata kuandikwa ni pamoja na haya, “Najua ugonjwa huu sitapona, Watanzania  watapata shida, lakini nitawaombea kwa Mungu.” Anaandika Mchambuzi Wetu … (endelea).

Maneno haya ya Mwalimu yanaonesha alivyoelewa vyema viongozi wajao. Wasiwasi wake ni uwezo mdogo wa viongozi kukabiliana na changamoto hizo bila ya ushauri makini.

Miaka ya bila mwalimu licha ya tambo za viongozi kudai kumuenzi, bado tunakwenda kama kishada.

Maisha yanavurugika, mayowe yanaongezeka kila kukicha. Wapi tunakosea? Hakika sasa tunayaona.

Marehemu Shaabani Robert katika moja ya kazi zake anawaelezea viongozi kama mwalimu ambaye hotuba na nasaha zake zinaelezea matatizo yanayotukabili katika kujiletea maendeleo  zinazoishi hadi leo, kuwa bado hawajafa kwa vile walichohubiri ndicho walichokitenda tofauti na viongozi wetu wa sasa wanachosema si watendacho.

Gwiji hilo la fasahi ya Mtanzania anawataja viongozi kama mwalimu na mashujaa wengine akiwemo mwenyewe kwenye kitabu chake  “matendo bora” kuwa, “ Ulimwengu una elimu ya kufa na kuishi.

Mtu hufa kitandani mwake na katika nyumba yake ni jambo rahisi kabisa. Hicho si kifo cha heshima ni mwisho wa maisha usio na maana yeyote.

Anaendelea kusema,  “Watu wafao kwa ajili ya matendo bora kama vile kupigania  Uhuru wa Taifa au Ulimwengu, kusaidia watu wenye shida wanaodhulumiwa na kudhalilishwa hufa kifo kitukufu. Hawafi, wafao katika matendo bora kwa sababu majina na sifa zao hazisahauliki na wala kifo cha mwili hakikomeshi  maisha yao.”

Watu kama Mwalimu wameendelea kuishi katika kumbukumbu na mioyo ya watu  na kuwa kiongozi  pekee mwenye mafanikio katika maisha.

Wengine tulio nao ni wale walao wanywao na wachezao hawafanikiwi sana kwani sifa zao huwa ni za muda tu wawapo madarakani, lakini wanapomaliza muda wao wanasahaulika mara moja.

 Lakini hawashindwi wafao kwa matendo bora kama alivyokuwa Mwalimu. Mtu hutupa maisha yake katika siasa na dini.

Huenda akashindwa kutengeneza matarajio yote ya wakati wa uhai wake, lakini kazi aliyoianza huendelezwa na wengine kwa kupokezana kwa zamu kama mwenge uliowashwa.

Hata kama Mwalimu alishindwa kufanikiwa. Kushindwa kwake ulikuwa mwanzo wa kufanikiwa wengine.

Wafao vitani kwa sababu ya Uhuru, hawafi bali huwa ni mashujaa na fahari kwa nchi au dunia na katika kumbukumbu zetu baadhi ya watu hutupa maisha yao katika elimu, uvumbuzi, uganga na matendo mengine ya thamani. Mtu afaye fofofo ni afanyae kazi kwa manufaa yake mwenyewe.

Sifa za Mwalimu katika kulingana na maneno ya Shaaban Robert ni nyingi mno ambazo ni nadra sana kuwa nazo viongozi wetu wa sasa.

Maishani mwake hakujilimbikizia mali, alifuata nadharia ya Mahatma Ghandi iliyosema kuwa, hayupo tayari kukaa juu ya kiti hadi wahindi wakae kwanza juu viti na yeye kama kiongozi wao angekaa mwishoni.

Kwenye utawala wake, hakukutokea rekode ta mamilioni ya pesa kupotea kwenye hisabu za serikali halafu ikawa basi, hakujivuna kwa ulimi, ndani ya utawala wake matendo yake yalivumisha jina lake.

Mwalimu alikuwa kiongozi makini kwa kila jambo japo dogo mathalani aliwahi kupiga picha huku akinyoosha kidole yenye ujumbe wa ‘jifunze kusoma wakati ni huu.’

Tulishuhudia nchi nzima mijini na vijijini watoto kwa watu wazima wakihudhuria kusoma kwa saa moja kila siku. Hata walevi hawakuruhusiwa kunywa hadi wasome kwanza.

Mwalimu alianzisha siasa ni kilimo na kilimo cha kufa na kupona na kutumia vyombo vichache vya uhamasishaji nchi nzima ilifanikiwa hadi tukawa na mikoa iliyojitambulisha kwa “the big four” ya Mbeya, Iringa, Ruvuma na Rukwa tulifanya yote haya kwa misingi ya kujitegemea.

Mwalimu alipinga sana watu binafsi kuwa msingi wa kujenga uchumi imara badala ya dola.

Matokeo yake zile mali za umma walizouziwa watu binafsi wameng’oa mashine zake na kugeuza maghala na maduka ya kuchuuza bidhaa kutoka nje. Hakuna bidhaa tunazoweza kujinasibu kuwa zimetengenezwa hapa nchini na vinyago vya bandia.

Tumeshindwa kuiendesha reli kama chombo imara cha uchumi. Tumekodisha bandari kwa watu binafsi.

Tumeuza viwanda, mabenki na mashirika ya umma Tumeua vyama vya ushirika na kuwaruhusu matajiri binafsi kununua mazao ya biashara. Kenya ambao walikuwa na siasa za kipebari bado mabenki na mashirika makubwa ni mali ya dola.

Mwalimu alihimiza kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi afanye kazi, akatunga sheria ya nguvukazi. Walikamatwa wazururaji na kupewa ardhi ya kulima nje ya jiji.

Leo hii waliopekwa Kibugumo, Mwanajilatu, Gezaulole, Kinyerezi wameubuka mashujaa ardhi waliyoitumia kwa uzalishaji sasa ina thamani kuwa na wanaiuza kwa bei kubwa.

Enzi za Mwalimu uliwekwa utaratibu wa kuwatumia matajiri na utajiri wao kuijenga nchi kwa manufaa ya taifa lakini leo tajiri utajiri na matajiri wanatumia ukwasi wao kutoa  zawadi na kamisheni  na rushwa kwa viongozi wetu.

Viongozi wetu wa sasa wanamiliki mali na majumba yenye thamani usiolingana  mchango na umri wao katika utumishi wa umma.

Viwanda na mashirika ambayo viongozi wetu ni wanahisa, wafanyakazi wake wanaishi katika hali za kukatisha tamaa hushindwa hata mlo mmoja tu japo vinatengeneza faida na hawana utetezi wa dhati.

Kwa unyonge wetu chini ya uongozi wa Mwalimu licha ya kutojitambulisha shabiki wa michezo  tulipata mafanikio makubwa.

Tuliweza kujenga viwanja vya michezo kila mkoa, wanariadha  walishinda mashindano makubwa ya kimataifa na kuleta medali, timu  za soka zilifika fainali ya mataifa huru ya kiafrika chini ya makocha wazalendo.

Leo hii tunaajiri makocha wazungu tunawalipa mamilioni ya fedha, tunajengewa viwanja vya kisasa na wageni na viongozi wetu kujitambulisha kuwa ni wapenzi wa michezo lakini timu zetu zinaposhiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, bado zinapachikwa majina kama watalii au kichwa cha mwenda wazimu huu ni ukosefu wa umakini tu.

Viwanja vya michezo vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi sasa ni magofu havitunzi wala kuendelezwa.

Viwanja vya wazi kwa ajili ya watoto na watu wazima vimeuzwa na viongozi wa kuchaguliwa na wale wa kuteuliwa.

Miji yetu na vijiji vilivyoasisiwa na mwalimu sasa ni makazi yasiyopimwa na yenye msongamano wa watu.

Mwalimu ni muasisi wa nyumba bora kwenye Jiji la Dar es Salaam ambapo wananchi wanyonge walijengewa nyumba na kukopeshwa kwa kulipa taratibu hadi wamalize madeni yao.

Leo hii tunashuhudia wakubwa (viongozi) wakijitaifishia na kujiuzia nyumba za serikali kwa bei ya kutupa na kuyageuza kuwa makasri na vitega uchumi vyao.

Wakati wa mwalimu, polisi wetu walikuwa wakitembea na virungu tu. Polisi anaajiriwa hadi anastaafu hakujua kufyatua risasi, na kwamba si kweli hakukuwa na uhalifu bali umakini wa viongozi, uwajibikaji na kulinda maadili ya kitanzania ya kutooneana yaliwekwa mbele. Leo hii polisi wetu kila uchao wanalalamikiwa kwa kufyatua ovyo risasi na kuua.

Kinachowasukuma Watanzania leo kuwakumbuka mwalimu Julius Nyerere Marehemu, Abeid Karume na Moringe Sokoine kila mwaka ni kwamba, waliamini katika kumtetea mnyonge dhidi ukandamizaji toka kwa matajiri au vyombo vya dola.

Mwalimu aliyotufundisha ni mengi, na mengi yametelekezwa. Kila anayeingia anacheza ngoma yake, anafanya atakavyo kwa namna akili na fikra zake zinavyomtuma.

Madhara kwa wananchi sio hoja kwake, mwalimu rudi maana bora enzi zako.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaTangulizi

Makonda kung’oka tena

Spread the loveUWEZEKANO wa Paul Makonda, kuendelea na wadhifa wake wa mkuu...

error: Content is protected !!