GODBLESS Lema, amechukua fomu ya kuwania Ubunge Arusha Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea)
Lema amefika Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha leo Jumanne tarehe 18 Agosti 2020 akiwa anaendesha gari yeye mwenyewe pamoja na familia yake akiwemo, Neema Tarimo.
Lema ambaye ameongoza jimbo hilo kwa miaka kumi mfululizo, amekabidhiwa fomu na Msimamizi wa Uchaguzi wilaya ya Arusha, Dk John Pima.
Baada ya kukabidhiwa, Lema amezungumza na waandishi wa habari akisema ana uhakika wa kuibuka tena mshindi katika uchaguzi huo kwa sababu wananchi wanamtaka mbunge anayezungumzia masuala yao badala ya kuisifia Serikali.

“Nimekuja kuchukua fomu ili niendelee kuwa mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, nimeona majina ya wanaotaka kugombea ubunge jimbo hili, hawaninyimi usingizi,” amesema Lema
Amesema, mwaka 2015 “Chadema tulishinda Kata 24 udiwani moja ikaenda CCM, lakini sasa tumeshaweka mikakati ya kuchukua Kata zote.”
Amesema wapigakura wamekua na mashaka ya kura kuchakachuliwa na kuonya uchaguzi mkuu haupaswi kuchezewa kwasababu unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na hawatakua tayari kuibiwa kura.
Lema amesema hata kitendo cha kuchomwa ofisi yao ya kanda ni dalili za uvunjifu wa amani na wameshamkabidhi kamanda wa Polisi mkoa majina ya waliotekeleza kitendo hicho ambao watawataja hivi karibuni.
Leave a comment