Wednesday , 27 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Kumekucha CCM: Barua ya Kinana, Makamba, siri nzito
Habari za SiasaTangulizi

Kumekucha CCM: Barua ya Kinana, Makamba, siri nzito

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza kupata ufa mwingine, kufuatia waliopata kuwa makatibu wakuu wake, Abdulrahaman Kinana na Yusuf Makamba, kumtuhumu Rais John Magufuli, kunyamazia njama za kuwachafua.” Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kinana na Makamba, wanamtuhumu Cyprian Musiba, mmoja wa watu anayejipambanua kuwa “mtetezi mkuu wa Rais Magufuli,” kuwachafua kupitia magazeti yake na mitandao ya kijamii, huku rais mwenyewe akinyamazia.

Kwa muda sasa, Musiba amekuwa akiporomosha tuhuma na shutuma lukuki wa watu mbalimbali, ikiwamo Kinana. Amekuwa akieleza kuwa viongozi hao wawili, pamoja na wengine kadhaa, wanapanga njama za kumkwamisha rais.

Jumatatu iliyopita, Kinana na Makamba, walisambaza waraka uliosheheni tafakuri nzito kwa nchi. Ndani ya waraka huo, viongozi hao wawili, wanatahadharisha kuwa vitendo ya Musiba na ulinzi anaopewa, vinahatarisha umoja na mshikamano wa taifa.

Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini amesema, “barua ya Kinana na Makamba, kwa mtu mwenye akili timamu, inatoa ujumbe mzito kwa Rais Magufuli na watu wake.”

Anasema, “hawa watu wamegusa pabaya. Maneno yao kwamba Musiba anahatarisha Muungano wetu, ni maneno mazito na yanayoweza kupunguza kwa kiasi kikubwa, wafuasi wa Rais Magufuli, hasa kutoka Zanzibar.

“Kwa mfano, haiwezekani Musiba amtuhumu Balozi Seif Iddi, Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kisha ukasema, Rais Dk. Ally Mohammed Shein, hashiriki njama hizo. Haiwezakani. Kama  Dk. Shein angekuwa hahusiki, kwa nini ameshindwa kumwajibisha Balozi Seif? Sasa maneno ya aina hii, yanaweza kumuweka Magufuli kwenye wakati mgumu zaidi.”

Katika barua yao ya kurasa tatu, Kinana na Makamba wanasema, kwa muda wa miezi kadhaa sasa, amejitokeza mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano.”

Wanasema, Musiba amewatuhumu wao wawili, kwa mambo ya uzushi na uongo, lakini bila kukemewa; na au kuchukuliwa hatua.

Soma hapa barua kamili ya Kinana na Makamba:

“Tumetafakari kwa kina kabla ya kuamua kutoa taarifa hii kwa umma kuhusiana na uzushi alioutoa Cyprian Musiba dhidi yetu katika nyakati mbili tofauti. Kwa sasa, Watanzania wote wanajua kuwa haja anayoyasema mtu huyu kuhusu watu mbalimbali siyo ya kwake. Yeye anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipasa sauti tu. Huyu ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi yetu. Katika mazingira hayo, hatuwezi kukaa kimya.

Baada ya kupata ushauri kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo viongozi watuu wastaafu wa CCM, viongozi wa dini, wanataaluma, wanahabari, wanaCCM na wananchi kadhaa, tumeamua kutoka kuhusu uzushi anaijitahidi kuueneza.

Mara ya kwanza alisema kuwa eti kunamkwamisha Ndugu Rais kutekeleza majukumu yake. Tuliyapuuza maneno hayo, kwanza kwa Imani kwamba viongozi wetu watayaona kwa namna yalivyo, kuwa haiwezekani tushiriki kuihujumu serikali ya chama tulichokitumikia maisha yetu yote. Na pili haingii akilini kwamba wastaafu wawili walio majumbani kwao eti wana uwezo wa kumzuia Rais, Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa chama kutekeleza majukumu yake.

Mara ya pili amekuja na tuhuma nyingine zinazotuhusisha na kutaka kumhujumu Rais ili asipate nafasi ya kupitishwa na chama kwa muhula wa pili 2020. Sisi tumekuwa watendaji wakuu wa Chama cha Mapinduzi. Tumesimamia michakato ya kupitisha wagombea katika nafasi ya Urais na nafasi nyinginezo. Huu nao ni uzushi na uzandiki uliosukwa kwa malengo maalum. Msingi wa tuhuma zote mbili ni hofu.

Tuliamini kabisa kwamba, pale unapojitokeza mtu hadharani na kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu na huku mtu huyo akijinasibisha na Serikali pamoja na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, basi hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma.

Kwa bahati mbaya viongozi wetu hawakuchukua hatua yoyote kuhusu jambo hili. Na zaidi, mtu huyu ameendelea kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima viongozi wastaafu na watu wengine wengi katika jamii. Mtu huyu amefikia hata hatua ya kuthubutu kuwatuhumu viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa wanamhujumu Rais. Amefanya hivyo bila kujali athari za kauli zake kwa Muungano wetu.

Tungependa kutamka rasmi kwamba shutuma anazotumwa Musiba dhidi yetu hazina ukweli wowote. Ni shutuma zilizoandaliwa kwa malengo maalum ya kutudhalilisha, kutuvunjia heshima, kutujengea chiki na kutuchafulia majina ndani na nje ya chama.

Tunawasihi Watanzania kwa ujumla wao kuzipuuza, kuzidharau n akuzinyanyapaa kauli za mtu huyu hatari kwa umoja na Amani ya nchi yetu. Tunashauri kuwa wakati tukimchukulia hivyo tuwe makini na kuwa na tahadhari na yanayoandaliwa na hao wanaomtuma. Hawa ni watu wanaoipeleka nchi yetu mahali pabaya kwa mwambuli wa kumsaifia Ndugu Rais.

Tunasikitika kwamza Musiba, licha ya kuwatuhumu na kuwakashifu Watanzania wenzake, viongozi na watendaji kwenye serikali, kwenye taasisi kadhaa za umma, za kijamii n ahata kwenye sekta binafsi, ameachwa akitamba, jambo linaloashiria kwamba anakingiwa kifua. Hata anapotumia lugha za vitisho na za kuhatarisha usalama wa raia hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yake.

Mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza maswali kadhaa yafuatayo; Kwanza, Cyprian Musiba anatumwa na nani? Pili, anakingiwa kifua na nani? Tatu, anatumika kwa malengo gani? Na nne, nini hatima ya mikakati yote hii?

Tarakuri yetu inatupelekea kupata majibu yafuatayo; Kwanza, kwa ushahidi wa kimazingira, mtu huyu anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala na mtu yoyote. Pili, zipo ishara kwamba watu hawa wanaomkingia kifua wana mamlaka, Baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalum, kwa watu maalum na kwa malengo maovu.

Tatu, Musiba anatumika kwa malengo ya kuwazushia, kuwakejeli, kuwavunjia heshima, kuwatia hofu na kuwanyamazisha, taasisi na watu ambao ni walengwa waliokusudiwa. Na nne, kuna dalili kuwa lengo na hatima ya mkakati huu ni kuandaa tufani ya kuwahusisha walengwa, wastaafu na walio kazini katika nafasi mbalimbali na matendo ya kihalifu, kimaadidli na kihaini ili kuhalalisha hayo wanayokusudia kuyafanya.

Sisi tumeamua kutokwenda mahakamani, walau kwa sasa, kwa sababu mbili. Kwanza, jambo hili lina taswira ya kimkakati na lina mtandao wenye malengo ya kisiasa. Kwa hiyo linapwswa kushughulikiwa kisiasa. Pili, unapochafuliwa, unachokwenda kudai mahakamani ni fidia, kwetu sisi, heshima yetu haiwezi kuthaminishwa na fidia.

Kwa msingi huo, tumeandika barua kwa Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, Mzee Pius Msekwa. Baraza ambalo Mwenyekiti wake ni Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais na Mwenyekiti wa CCM Mstaafu. Tunafanya hivyo kwa kuzingatia katiba ya CCM toleo la 2017 ibara ya 122. Tumeshawasilisha maombi yetu tukiwasihi wazee wetu watumie busara zao katika kulishughulikia jambo hili ambalo linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani ya Chama na nchini.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

Habari za Siasa

Mgongano wa kimasilahi wamhamisha Chande TTTCL

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),...

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme: Rais Samia ampa miezi sita bosi mpya TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi...

Habari za Siasa

Rais Samia avunja bodi ya REA

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Balozi Jacob Kingu, kuwa...

error: Content is protected !!