Wednesday , 27 September 2023
Home Habari Mchanganyiko Rushwa, vitisho vyatawala malipo ya korosho 
Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Rushwa, vitisho vyatawala malipo ya korosho 

Zao la Korosho
Spread the love

MALALAMIKO ya rushwa na vitisho kwa wakulima na wafanyabiashara wa korosho, vimetawala kwenye madai ya malipo ya biashara hiyo, mkoani Mtwara. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), inatuhimuwa kunyanyasa wakulima wa korosho kwa kuwaomba rushwa ili kuweza kulipwa fedha zao.

Mkazi wa Tandahimba mkoani Mtwara, Nurdin Adinani, ni miongoni mwa wakulima waliowasilisha malalamiko yao kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kuilalamikia bodi ya nafaka kwa vitendo hivyo.

Akizungumza na MwanaHALISI ONLINE, Nurdini amesema, urasimu umetawala kwenye bodi ya mazao; wakulima wanashindwa kupata haki zao, kutokana na kushindwa kutoa mlungura.

Amesema, “… hivi sasa, kuna mambo ya hovyo yanayoendelea kwenye bodi ya mazao. Kuna rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Hakuna malipo mpaka utoe fedha.”

 Amesema, “hapa watu tunalia kweli kweli. Hulipwi haki yako, mpaka utoe fedha na ndio maisha yaliyopo hivi sasa.” Amesema, kibaya zaidi, “watu wanachukuliwa fedha zao, lakini hakuna wanachoambulia.”

Mkulima huyo ameeleza kuwa wakulima wengi wamekuwa wakijengewa hofu ya kuhoji malipo yao na wengine wakitishwa.

“Watu wanaogopa kuzungumza, sababu ya kujawa na hofu. Ukitaka kuzungumza kuhusu korosho unatishwa. Ukitaka kuzungumza kuhusu malipo yako, unatishwa kubambikiwa kesi.

“Hata mkija kuwauliza wakulima, wanaogopa kuzungumza. Kwa kweli, maisha yetu hapa wakulima husani wakulima wa korosho wa Lindi na Mtwara, yamekuwa magumu sana.”

Kwa mujibu wa Nurdini, wengi wa wakulima hao wamekata tamaa ya kuwekeza kwenye kilimo hicho kutokana na ugumu wa kupata fedha zao, na kwamba baadhi yao mpaka sasa, wameshindwa kuandaa mashamba yao upya kwa ajili ya msimu ujao.

 “Tumekata tamaa kuwekeza katika kilimo, wakulima hatujalipwa, tulio wengi hatujandaa mashamba kwa ajili ya uzalishaji mwingine…ukiachana na habari ya kuandaa mashamba, maisha yetu wengine ni changamoto,”anaeleza Nurdini.

Anaongeza, “jambo hili linatishia kupungua uzalishaji kwenye msimu ujao. Leo ni Julai kuelekea Agosti. Ukishindwa kuandaa shamba lako mwezi huu, huwezi kuvuna chochote kwenye msimu ujao. Hivyo basi, hata mkulima akilipwa sasa, hawezi kuandaa shamba lake kwa ajili ya msimu ujao.”

MwanaHALISI ONLINE lilipomtafuta Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, John Maige, ili kutolea ufafanuzi wa madai hayo, lakini alishindwa kuzungumza lolote kwa maelezo kuwa alikuwa kwenye kikao.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho nchini, Francis Alfred, alipoulizwa juu ya madai hayo, haraka alisema, “malalamiko hayo ya wakulima, bado hayajafikishwa mwezani kwangu.”

Alipoelezwa kuwa hafahamu kuwa ni muda mrefu sasa, wakulima na hata wawakilishi wao bungeni, wamekuwa wakieleza tatizo la kutonunuliwa kwa korosho n ahata serikali kushindwa kulipa fedha za korosho ilizozisomba, mtendaji huyo wa bodi ya korosho anasema, tayari serikali ilinunua korosho zote.”

Alipoulizwa kuhusu madai ya rushwa, Alfred anasema, “zoezi hilo liliendeshwa kwa uwazi na weledi mkubwa.”

Amesema, “msimu wa kuuza korosho ulishafungwa mwezi Machi 2019; na kwamba katika msimu wa 2018/2019, Serikali ilinunua korosho zote zilizozalishwa. Ununuzi huo ulifanywa na taasisi mbalimbali kwa uwazi na weledi mkubwa. Hivyo hakuna urasimu wowote.”

Kuhusu malipo ya fedha za wakulima yanayofanywa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo (TADB), Alfred ametaka wakulima wenye malalamiko, kuyafikisha ofisini kwake ili yaweze kufanyiwa kazi.

Anasema, “lakini kama kuna taarifa za kina zaidi nitaomba nizipate, ili tudhibiti kwa msimu ujao. Lakini kwa mwaka huu, napenda kukuhakikishia kuwa hakuna tatizo.”

Gelasius Byakanwa, mkuu wa mkoa wa Mtwara, naye ameliambia MwanaHALISI ONLINE, kuwa ofisi yake haina taarifa za malalamiko hayo.

Byakanwa ametoa wito kwa wakulima walio na malalamiko hayo kwenda ofisini kwake ili ajue namna ya kuwasaidia kumaliza matatizo yao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

Habari za Siasa

Mgongano wa kimasilahi wamhamisha Chande TTTCL

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),...

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme: Rais Samia ampa miezi sita bosi mpya TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi...

Habari Mchanganyiko

Wizara ya madini kurusha ndege ya utafiti wa madini Geita

Spread the loveKutokana na mchango wa wachimbaji wadogo wa madini kwenye pato...

error: Content is protected !!