May 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kufuru ya Zitto Kusini, amtingisha Prof. Lipumba

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo akiwa katika mkutano wa ndani wilayani Kilwa, Lindi

Spread the love

ZITTO Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, ameacha simanzi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), Mkoa wa Mtwara na Lindi. Anaripoti Faki Sosi, Lindi … (endelea).

‘Ameteka’ madiwani waliokuwa wa CUF, huku wafuasi wa chama hicho kinachoongozwa na mwenyekiti wake Prof. Ibrahim Lipumba wakipokea kadi za uanachama wa ACT-Wazalendo.

Ziara yake aliyoifanya kuanzia tarehe 22 Juni – 2 Julai 2020, imekuwa ni yenye maumivu makubwa kwa CUF ambayo ilikuwa ikijinasibu kuwa Lindi na Mtwara ni ngome zake.

Siku ya kwanza ya ziara hiyo akiwa mkoani Pwani kwenye Halmashauri ya Rufiji, alipokea madiwani wanne wa CUF. Madiwani hao ni Juma Mlanzi (Kata ya Umwe); Issa Miduma, (Kata ya Kipugila); Hassan Mpota, (Kata Mgomba) na Sofia Mkengesi (Viti Maalum).

         Soma zaidi:-

Kwenye halmashauri hiyo  yenye kata 13, CUF ilikuwa na madiwani sita ambapo wanne wa kuchaguliwa na wawili wa viti maalum, wanne wamejiunga na ACT-Wazalendo, mmoja amekimbiliwa CCM na sasa kimebaki na diwani mmoja wa viti maalam.

Baada ya kukutana na upinzani kutoka Jeshi la Polisi, Lindi kiongozi huyo amaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini aliendelea na ziara yake tarehe 30 Juni 2020, akiwa Kilwa Kivinje alivuna madiwani watano kutoka CUF.

Madiwani hao ni Hassan Njenga (Likawage); Ashura Kuchao, (Kata ya Njinjo); Zainabu Mwishaa (Viti Maalum); Amina Gorge (Tingi) na Swalehe Mketo (Kibata).

Kisha alikwenda Tandahimba, Mtwara tarehe 2 Julai 2020, huku alikuta mwaliko kutoka kwa madiwani waliokuwa wa CUF, na kisha madiwani hao sita wakatangaza rasmi kukitaliki chama chao cha awali na kujiunga na ACT-Wazalendo.

Madiwani hao ni Sharf Dihoni (Dangote), Ramadhan Mtimbuka, (Obasanja), Fidea  Hittu, Asha Tebwa, Halima Tamatama na Hadija Mnipikwa.

Aliporejea Lindi Mjini, Zitto alikutana na ‘shehena’ ya madiwani ya wa CUF waliokuwa wa kisubiri kadi za uanachama wa ACT-Wazalendo.

Hawa Kipera (Viti Maalum Lindi); Saidi Kitunguli, (Mingoyo); Saidi Mateva, (Mnazi Mmoja); Ahmadi Zuber (Mwenge), ni miongoni mwa madiwani waliosajiliwa na ACT-Wazalendo na kuiacha CUF.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo akiwa ndani ya gari ya Polisi wilaya ya Kilwa baada ya kukamatwa akiwa katika mkutano wa ndani

Kwa sasa, chama kinachoongoza kwa kushika tama baada ya uchaguzi mkuu 2015, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, kinaweza kuwa CUF.

Ngome zake zilizokuwa zikitamba nazo kwenye uchaguzi mkuu 2005, 2010 na hata 2015 ikiwemo Unguja, Pemba, Lindi, Mtwara na hata Tanga ‘zimeteketea,’ kwa sasa CUF ni kama mfa maji.

Mvuto wa CUF kwa Watanzania umeporomoka, msingi wa kuporomoka huko ni mgogoro uliyochipua baada ya kupishana mtazamo kati ya viongozi wakuu wawili – Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho na Prof. Lipumba.

Hata hivyo, kuondoka kwa Maalim Seif kwenye chama hicho na kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo, kumezamisha kabisa ndoto za CUF. Hatua hiyo imesababisha Prof. Lipumba na chama chake kushindwa kuvuma bara na visiwani.

Chama cha Denokrasia na Maendeleo (Chadema), ni miongoni mwa vyama vilivyoumizwa kwenye utawala huu (2015-2020), lakini uimara wake unaonekana ndani ya chama, harakati na mipango iliyo wazi.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo akizungumza na wanachama wa chama hicho Rufiji, Pwani

Mzizi wa kuchechemea kwa Chadema hakutokani na viongozi wakuu kusigana, bali wale waliokuwa hawatoshi kwenye chama hicho na kuamua kuhama, walitaka kujenga taswira hasi-hawajafanikiwa. Hii ni tafauti kabisa na tatizo la CUF lililosukwa na mgogoro kati ya Lipumba na Maalim Seif.

Udhaifu wa CUF umekuwa neema kwa vyama vingine vya upinzani, ACT-Wazalendo ndio mnufaikwa wa kwanza wa kazi iliyofanywa na Prof. Lipumba kwa muda mrefu Bara na Visiwani.

Kwa sasa ACT-Wazalendo ni kama ‘wanamsukuma mlevi’ kwenye maeneo yaliyokuwa ya CUF, Prof. Lipumba na watu wake wameishiwa pumzi, hawafurukuti. Wameelemewa.

Ukiachana na Pemba ambapo CUF ‘imefutwa,’ Unguja bendera za chama hicho pia zimeshushwa, Tanga wanaelekea kuisahau CUF, Lindi na Mtwara ndio kwanza wanaisuka zambarau kwenye mitaa yao.

error: Content is protected !!