Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea atumia mkutano mkuu ACT- Wazalendo, kutema nyongo
Habari za SiasaTangulizi

Kubenea atumia mkutano mkuu ACT- Wazalendo, kutema nyongo

Spread the love

MBUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Ubungo, Saed Kubenea, amekimwagia sifa Chama cha ACT-Wazalendo, kufuatia hatua yake ya kuruhusu mchakato huru wa uchaguzi. Anaripoti Kevin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho leo Jumamisi, unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Kubenea alisema, kitendo cha chama hicho, kuendesha zoezi lake la uchaguzi, bila watu kuhambuliana, kinastahili kupongezwa.

“Siyo jambo la kawaida, kwa chama cha siasa kichanga kama hiki, kuendesha uchaguzi wake bila watu kutuhumiana usaliti, kutukanana, kushambuliana na kuzushiana uwongo. Ninyi mmeweza, angala mpaka sasa,” ameeleza Kubenea na kuongeza, “haya mliyofanya, wengi wameshindwa.”

Kubenea alihudhuria mkutano huo kama mgeni maalum, kutokana na eneo linalofanyika mkutano wa chama hicho, kuwa sehemu yake ya jimbo lake la uchaguzi.

Akiongea kwa hisia kali, Kubenea alisema, “ndugu zangu, kuitisha uchaguzi mkuu wa chama na mkatangazia wanachama wenu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, na wao wakajitokeza kufanya hivyo; na mkaenda kwenye mchakato wa uchaguzi, bila kushutumiana usaliti, bila kutukanana; na bila kuvuana nguo, hilo ni jambo kubwa sana. 

Amesema, katika baadhi ya vyama nchini, vikiwamo vyama vikubwa vya siasa, nafasi kama hizo, huwa hazisogelewi. 

Amesema, “wengine wamediriki hata kuwatisha wanachama wao kwa kuwambia, “sumu huwa hailambwi kwa ulimi,” na kwa maoni yake, “huo ni ukosefu wa demokrasia.”

Amesema, “kuna chama ambacho kipo madarakani, nafasi kama ya mwenyekiti wa chama, katibu mkuu, naibu makatibu wakuu na makamu wenyeviti, hazigombewi. Halafu chama hicho hicho, kinasimama na kusema, sisi baba wa demokrasia.

“Lakini kubwa zaidi, wajumbe wa Kamati Kuu (CC) hawachaguliwi. Mwenyekiti wa chama amepewa mamlaka ya kupendekeza wajumbe wa Kamati Kuu kutoka miongoni mwa wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC). 

Kwa maneno mengine, ikiwa mwenyekiti wa chama hakutaki, huna mwanya wa kuingia kwenye kamati kuu ya chama chake.”

Aidha, Kubenea amekipongeza chama hicho kwa kutoa nafasi sawa kwa wagombea wote, kueleza sera zao. Hususan katika mdahalo wa kupima uwezo wao.

“La pili niwaongeze kwamba, hiki chama ni kidogo kwa umri, pengine kuliko vyama vyote vya siasa kwa sasa. Lakini kimethibitisha kwa vitendo, kwamba kutangulia si kufika. Leo ukitaja vyama vikubwa vya siasa nchini vinavyofahamika kwa wananchi na Jumuiya ya Kimataifa, huwezi kuzungumza bila kuitaja ACT – Wazalendo.”

Mwanasiasa huyo ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari anasema, “hili halikuja kwa bahati,” hapana. Anasema, hili limewezekana kutokana na jitihada zilizofanywa na viongozi na wanachama wao, kwa kila mmoja na nafasi yake.

Kubenea amesema, “nimeona matangazo ya mwito wa watu kugombea nafasi, nimeona midahalo kupima viongozi wanaoomba hizo nafasi, hili sio jambo la kawaida. Mmefanya jambo kubwa ambalo linapaswa kuigwa na kuwa mfano kwa vyama vingine vya siasa.”

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, Kubenea amekitaka chama hicho kushirikiana na vyama vingine vya upinzani, katika kuhakikisha Tanzania hairejei katika mfumo wa chama kimoja.

Taifa letu linapita katika kipindi kigumu sana, ameeleza Kubenea na kusisitiza kuwa kipindi ambacho taifa linapita, kumeibuka malumbano ya uchaguzi mkuu ujao yanayotokana na kutokuwapo kwa uhakika wa kufanyika kwa uchaguzi huru na haki. 

Amekitaka ACT- Wazalendo, kwa kuwa ni wadau muhimu katika uchaguzi huo, ili kusimamia mfumo wa vyama vingi na kwamba bila mfumo wa vyama vingi, vipaji vingi vilivyoibuliwa, akiwamo yeye mwenyewe, pengine visingepatikana.

Katika hatua nyingine, Kubenea ameiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria. Ili kiwe chombo huru.

” Msajili hayuko huru, ofisi ya msajili iko chini ya ofisi waziri mkuu ambaye ni mjumbe kamati kuu CCM. Inapata fungu lake chini ofisi ya waziri mkuu, hawezi kuwa watu huru.

“Tunahitaji ofisi ya msajili kiwe chombo huru kinachojitegemea. Ukikuta vyama vinaandikiwa barua kila kukicha, huku wengine wakiendelea kuvunja sheria, lakini wakiwa hawabughudhiwi, basi elewa haraka kuwa Msajili wa Vyama hayuko huru katika kutimiza majukumu yake,” amesisitiza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!