KUJA kwa kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe na mwingine kutoka Afrika Kusini kushuhudiwa akihutubia kwa njia ya video kwenye jukwaa la kielektroniki, kulichangia kwa kiasi kikubwa kuupa mkutano mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo taswira halisi ya kuwa mkutano ulioandaliwa kwa umahiri mkubwa. Anaandika Jabir Idrissa, Dar es Salaam … (endelea).
Tendai Biti, makamu wa rais wa Chama cha Movement for Democratic Change (MDC) kilichoasisiwa na Morgran Tsvangirai mwanasiasa aliyekuwa mpinzani wa utawala dhalimu wa Rais Robert Mugabe, alialikwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano uliofanyikia Mlimani City, Dar es Salaam.
Lakini kama haikutosha vile, ndani ya ukumbi huo, wajumbe wapatao 500 wakiwemo karibu 400 wenye haki ya kupigakura, walishuhudia hotuba fupi lakini yenye ujumbe mzito wa kimapambano aliyoitoa Mmusi Maimane.
Maimane ni mwanasiasa kijana nchini Afrika Kusini ambaye Oktoba mwaka jana alijiuzulu kongoza Chama cha Democratic Alliance (DA) baada ya kuona hakijafanikiwa kuwavuta Waafrika weusi. Chama hicho kiliundwa kwa ajili ya Wazungu baada ya kuanguka kwa utawala wa makaburu mwaka 1991.
Akivalia kanzu maridadi nyeupe iliyozoeleka nchini Tanzania, Biti alijitokeza kama mwanasiasa mtulivu, na kuhutubia kwa dakika 30 hivi akitoa matamshi ya kuhimiza umma kushikamana na kustahmili harubu kabla ya kutarajia demokrasia ya kweli na utawala wa sheria.
Alisema jitihada za kukomesha udikteta unaoendeshwa na Waafrika weusi, zinahitaji kuunganishwa badala ya kuwa zilizogawanyika. Tatizo la barani Afrika si la kutokuwepo katiba nzuri, isipokuwa ni watawala kutoheshimu misingi ya kikatiba.
“Kila bila binadamu anazaliwa na uhuru wa kuchagua anachotaka maishani. Tunafanya maamuzi ya mengi tunayoyataka. Si ndivyo… basi ni muhimu pia tukawa na haki na uhuru wa kuchagua ni nani atuongoze. Lakini mbona tunachagua na bado tunalazimika kuendelea kupambana na tawala mbovu,” alisema.
Alisema watawala weusi Afrika hawaheshimu katiba na sheria hata kuliko walivyokuwa watawala Wazungu, ndio maana wakiingia wanadhibiti mamlaka yote – serikali, bunge na mahakama. “Unayo mahakama lakini haiko huru, bunge limedhibitiwa na dola. Ninasema Afrika tunahitaji watawala wanaoheshimu katiba na sheria,” alisema.
Nchini kwao Zimbabwe, amesema, dikteta Mugabe aliondolewa na Jeshi la Taifa, lakini tofauti na wananchi walivyodhani wangepata mabadiliko; hali ya mambo imezidi kuwa mbaya chini ya utawala wa Emmerson Munangagwa, mpigania uhuru mwenzake Mugabe aliyepata kumtumikia kama makamu wake wa rais.
Biti ambaye aliwahi kuwa waziri wa fedha, amehimiza Waafrika kuunganisha nguvu za kupambana na udhalimu.
Maimane yeye alitoa hotuba fupi kwa njia ya video, akisema Afrika inapaswa kuungana kama inataka kuona mifumo ya utawala ya kidemokrasia inashamiri.
Profesa Azaveli Lwaitama ni msomi mwingine aliyechangamsha mkutano kwa kutoa hotuba nzuri akisema anafurahi kuona ACT-Wazalendo kinajitokeza kuwa chama makini kinachojipanga ili kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema siku zote anaamini chama bora cha upinzani nchini ni kile kinachochukua hatua imara za kuiondoa CCM madarakani. “Jahazi kama hili alolipanda Maalim Seif na watu wake ili kuitafutia Zanzibar uhuru kamili ndani ya Muungano, ndilo makini. Fikiria ni wapi Maalim angekimbilia pasingekuwa na ACT-Wazalendo.
“Chama tawala kinachotumia dola kuhodhi mahakama hakitaondoka kwa vyama vya upinzani vinavyounga mkono juhudi za rais. Songeni mbele mwanangu Zitto Kabwe,” alisema.
Profesa Lwaitama aliyestaafu mwaka 2015 akiwa mwalimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema ni uhuni kukuta mwanasiasa wa upinzani anahama alipo na kusema “narudi nyumbani.” Unarudi nyumbani wapi… kule ambako CCM inahodhi Bunge na kuvuruga uhuru wa mahkama?”
Alimshangaa Sisty Nyahoza, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, akisema anasimamia vyama katika nchi isiyo na uchaguzi huru na wa haki. Katika hali hii, ni jambo kubwa nyinyi vyama vya upinzani vilivyo makini kuungana kwa maslahi ya nchi.
Awali naibu msajili wa vyama akihutubia mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo alisema anashukuru wamealikwa lakini wangekuja tu hata kama wasingealikwa kwa sababu sheria inawapa uwezo wa kufika kwenye vikao vya juu vya vyama vya siasa hata msajili asipoalikwa rasmi.
Aliwataka viongozi kukumbuka kuwasilisha taarifa ya maamuzi ya mkutano mkuu huo ndani ya siku 14 akisema ndivyo sheria inavyoelekeza.
Leave a comment