Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea amuasa Rais Magufuli
Habari za SiasaTangulizi

Kubenea amuasa Rais Magufuli

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amemtahadharisha Rais John Magufuli kuwa kuitekeleza sheria ya uwakala wa meli kutakuwa na madhara makubwa kiuchumi na kijamii. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Kutekelezwa kwa sheria hiyo baada ya kusainiwa, kutakwaza kazi ya mashirika yapatayo 700 yanayofanya kazi ya uwakala wa meli na forodha; na kwa upande mwingine, kutasababisha kupotea kwa ajira zaidi ya 10,000 za vijana wanaofanya kazi ya kibarua bandarini.

Ajira zitakazopotea ni pamoja na zile za upakizi wa mizigo kwenye magari yanayotumika kubebea mizigo inayotolewa Bandari ya Dar es Salaam, ambayo inaaminika kuwa ndio lango kuu la biashara na kitovu cha uchumi kutokana na kuhudumia nchi saba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kubenea amesema kuwa muswada huo uliopelekwa bungeni tarehe 27 Juni mwaka huu, ukiwa na jumla ya sheria tisa, ulipitishwa ndani ya saa tatu, na bila ya kupata michango ya wabunge.

“Siku hiyo kulipitishwa na kufanywa marekebisho ya Sheria Mbali Mbali ikiwemo muswada huu ninaouzungumzia leo. Miswada yote ilijadiliwa kwa saa tatu, kuanzia saa 4 kamili asubuhi hadi saa 7:30 mchana. Utaona namna sisi wabunge twenye jukumu la kiuishauri serikali, tulivyonyimwa fursa kwa makusudi ya kuchangia,” alisema.

Sheria nyingine ni Sheria ya Vyama vya Kijamii (Sura ya 337), Sheria ya Takwimu (Sura ya 351) na Sheria ya Muunganisho wa wadhamini (Sura ya 318).

Kubenea amesema kwa namna sheria hiyo ilivyokuwa hatari kwa uchumi ni vema Rais Magufuli aiangalie kwa jicho pana kwa sababu sidhani kama atakuja kujisikia amewajibika ipasavyo kwa Watanzania akiyashuhudia madhara yake.

“Ni imani yangu kuwa kama Rais Magufuli angepewa taarifa sahihi ya madhara ya moja kwa moja yatakayoathiri utungaji wa sheria hiyo kwenye sekta ya bandari, naamini muswada huo usingekuja bungeni vile ulivyolewa.”

Kubenea amesema katika marekebisho ya fungu la 415 la sheria hiyo, Shirika la serikali la uwakala wa Meli (TASAC) limepewa mamlaka ya kufanya kazi za uwakala wa meli na uwakala wa forodha (Clearing and Forwarding) ambao hapo awali walikuwa na jukumu la kusafirisha nakuondoa bidhaa zote za mafuta ya petroli, bidhaa za madini na makinikia; kusafirisha silaha, wanyama hai pamoja na nyara za serikali. 

“Katika marekebisho ya sheria hii, hasa kwenye kifungu hicho cha 415, TASAC imepewa mamlaka ya kufanya kazi ya forodha kwa mizigo yote inayopitia bandarini, kwenda kokote duniani, ikiwamo sukari na mbolea,” amesema Kubenea.

Kwa kuwepo sheria hiyo mpya, itasababisha mizigo iliyokuwa ikitarajiwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwenda au kutoka nchi za jirani, kuelekezwa kwenye bandari shindani kama Mombasa (Kenya), Beira (Msumbuji) au Cape Town nchini Afrika Kusini.

“Sheria imeipa mamlaka TASAC kuwa ndio chombo pekee chenye haki ya kuandaa, kusimamia na kuratibu usafirishaji wa mizigo kupitia kwenye makampuni ya meli.

Yawezekana kulikuwa na dhamira njema ya kuanzishwa kwa TASAC, lakini ukiangalia ukubwa wa kazi zilizopo bandarini na katika mipaka ya Tanzania; na kutokana na kutokuwapo maandalizi ya kutosha, Tanzania inaweza kujikuta ikiingia kwenye matatizo makubwa ya mdororo wa uchumi, amesema na kutahadharisha kuwa “kutakuwa na mlundikano wa mizigo unatokana na uwezo mdogo wa TASAC.”

Amesema anavyofahamu TASAC, haina nyenzo za kutosha za kufanyia kazi na wataalamu wenye uzoefu wa kazi hizo ikiwemo ya kushughulikia nyaraka zinazotakiwa katika usafirishaji wa mizigo bandarini. Amesema kazi hii imekuwa ikifanywa kisasa kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia.

“Msongamano huu wa mizigo bandarini, utasabababisha meli kushindwa kushusha mizigo kwa wakati, hii itaongeza gharama kwa wenye meli na kuwasukuma kuamua kutumia bandari za nchi jirani kushushia mizigo waliyobeba.”

Badala ya kusaidia ukuaji wa bandari, tutajikuta tunapoteza wateja. Makampuni mengi ya uwakala wa meli, wanakwenda nje ya nchi kutafuta wateja. TASAC hawawezi kufanya hivyo, matokeo yake, bandari yetu itapoteza wateja.”

Amekitaja chanzo cha serikali kupeleka muswada huo bungeni ni ripoti ya Tume ya Rais ya Makanikia ambayo katika ripoti yake, ukurasa wa 11, kumetajwa taasisi za serikali zinazowajibika kutoa tathmini ya mzigo unaotarajiwa kusafirishwa nje ya nchi na ACACIA.

“… ukweli ni kuwa kwenye biashara ya usafirishaji wa mizigo bandarini, kuna kitu kinaitwa house to house, kwamba wenye meli huombwa kuwapatia wasafirishaji makasha (makontena) matupu kwa ajili ya kazi hiyo.

Katika suala la Makanikia, wasafirishaji waliomba na kupeleka makontena matupu kwa mwenye mzigo. Mwenye mzigo akapakia mzigo wake chini ya uangalizi wa Afisa wa Forodha na Afisa wa Madini na baada ya ukaguzi kufanyika, maofisa hao wakafunga lakiri (Seal) kwa kila kontena. Wakati kazi hii ya kufunga seal inafanyika, si mwenye meli wala msafirishaji aliyeshuhudia,” amesema.

Amesema kuwa ripoti ya makanikia imetaja kampuni ya kimataifa ya uchunguzi wa maabara ya SGS na kwamba ripoti zake, zimekuwa zikitumika kuhalalisha usafirishaji wa makinikia, kwa zaidi ya miaka 19 sasa.

Meneja Mkazi wa ACACIA nchini, alinukuliwa  akidai kuwa kampuni yake haikuwa na taarifa ya kiasi cha dhahabu na madini mengine, kilichokuwamo kwenye makanikia na kwamba anayepaswa kuulizwa au kuhojiwa, ni kampuni hiyo ya kimataifa. “Tangu wakati huo, binafsi sijasikia kampuni hii ya SGS ikitajwa tena mahala popote kutuhumiwa na ama uzembe au udanganyifu,” amehofia Kubenea ambaye pia ni mwandishi wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL).

Ametilia shaka namna SGS ilivyopewa zabuni… (anadai) zipo taarifa kuwa kampuni hii iliwahi kupata kashfa nyingine kubwa ya kutuhumiwa kufanya udanganyifu kwenye mtambo wake wa kuratibu gharama za simu za kutoka nje, kazi ambayo ilipewa na Mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA). Amesema Serikali iliripoti hasara ya mamilioni ya dola.

Kubenea amezungumzia sasa athari zinazoweza kutokea kwa kutekelezwa sharia mpya ya masuala ya uwakala wa meli na forodha, kwa sababu ya kule kukosa fursa ya kuchangia muswada ulivyowasilishwa bungeni lakini pia kwa kuwa yeye ni mbunge wa mkoani Dar es Salaam ambako sehemu kubwa ya wananchi wanapata riziki kutokana na kazi zenye uhusiano na Bandari ya Dar es Salaam.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!