December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Timu JPM washusha nyundo tena

Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Dodoma

Spread the love

KIKUNDI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachomtetea Dk. John Magufuli, mwenyekiti wa chama hicho, kinaendeleza mashambulizi. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).  

Wafuasi hao jijini Dodoma, wanataka Kanal Abdulrahman Kinana na Luteni Kanal Yusuf Makamba ambao ni makatibu wakuu wastaafu wa CCM, washughulikiwe.

Wamedai, kitendo cha Kinana na Makamba kuandika barua ya malalamiko kwa Pius Msekwa, Katibu wa Baraza la Viongozi Wastaaf uwa CCM kwamba anachafuliwa na Cryspian Musiba, imevunja taratibu za chama.

Kinana na Makamba walimwandikia barua Mzee Msekwa wakilalamika kuchaguliwa pia kuzushiwa uongo na Musiba, ambaye anajitambulisha kama mtetezi wa Rais Magufuli. Pia barua hiyo, ilipelekwa kwa mwenyekiti wa chama hicho (Dk. Magufuli).

Akitoa tamko la Halmashauri ya CCM Mkoa wa Dodoma, Hanry Msunga ambaye ni Katibu wa Siasa na Uenezi wa mkoa huo amesema, Kinana na Makamba wamepotoka.

Na kwamba, viongozi hao wanapaswa kushtakiwa kwa ‘uovu’ walioufanya kwa kuwa, ni kinyume na utaratibu wa chama hicho.

Tofauti na hoja za watetezi wengine wa Dk. Magufuli kwenye sakata hilo, CCM Dodoma wameeleza kuwa, Musiba ni ‘mtu mdogo’ na kwamba, Makamba na Kinana wameshusha heshima ya chama hicho kwa kukihusisha chama na Musiba.

“Haiwezekani chama kikongwe kihusishwe na Musiba,” ameeleza Msunga na kuwa kauli hiyo ni kukishusha hadhi chama hicho hivyo, Makamba na Kinana hawakustahili kufanya hivyo.

https://youtu.be/MOtCw6fSJJY

Akimtetea Rais Magufuli, Godwin Mkanwa amesema, kiongozi huyo wa nchi hafai kubezwa kwa kazi nzuri aliyoifanya tangu aingie madarakani 2015.

Kauli za Msunga na Mkanwa zimetanguliwa na zile za Hussein Bashe, aliyeapishwa jana tarehe 22 Julai 2019 siku chache baada ya kueleza kuwa, Kinana na Makamba wanataka kumvuruga Rais Magufuli.

Kwenye barua yao Makamba na Kinana wameeleza; “mtu huyu (Musiba), anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.”

Wanasema, “zipo ishara kuwa watu wanaomkingia kifua Musiba, wana mamlaka, baraka na kinga, ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalumu kwa watu maalumu na kwa malengo maovu.”

Wabunge waliojitokeza kuwashambulia Makamba na Kinana mpaka sasa ni Livingston Lusinde, Mbunge wa Mtera; Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita Vijijini na James Millya, Mbunge wa Simanjiro.

error: Content is protected !!