Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kiongozi Uamsho apata kigugumizi suala la katiba mpya
Habari za Siasa

Kiongozi Uamsho apata kigugumizi suala la katiba mpya

Shekhe Mselem Ali Mselem
Spread the love

 

KIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Mselem Ali Mselem amesema hatoweza kujitosa katika mjadala wa Katiba mpya, kwa kuwa Serikali haijaruhusu mchakato wa upatikanaji wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Sheikh Mselemu ametoa kauli hiyo hivi karibuni, alipoulizwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kama ataendelea na harakati zake za kupigania Katiba mpya, alizokuwa anazifanya na wenzake kabla ya kusota rumande miaka nane iliyopita, wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.

Kiongozi huyo wa Uamsho na wenzake 17, waliachwa huru Juni 2021, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, kuwafutia mashtaka hayo yaliyokuwa yanawakabili kwenye Kesi ya Jinai Na. 121/2021. Masheikh hao waliakamatwa katika nyakati tofauti 2012 hadi 2014.

Sheikh Mselem amesema mwanzo walishiriki katika harakati za kudai Katiba mpya, kwa kuwa Serikali iliruhusu Watanzania watoe maoni yao kwenye mchakato wa marekebisho ya Katiba iliyopo, iliyotungwa 1977.

“Mwanzo nilishiriki sababu fursa ya kufanya hivyo ilikuwepo, kabla ya kutoka hiyo fursa sijabuni hicho kitu. Kwamba nataka hivi na hivi, sina mamlaka hayo,” amesema Sheikh Mselem.

Sheikh Mselemu amesema, kama Serikali itaruhusu mchakato huo, atatoa mchango wake.

“Kwa hiyo ikiwa nchi imetaka maoni ya watu na mimi nikikubalika kuwa mtu miongoni mwa Watanzania, basi naweza nikaitumia fursa wakati wowote,” amesema Sheikh Mselem.

Sheikh Mselemu amesema, kilichosababisha yeye na wenzake kusota rumande ni harakati zao za kudai Katiba mpya.

“Sababu iliyopelekea kukaa mahabusu ni kazi tuliyofanya kutoa elimu kwa wananchi, kuwaandaa namna gani watatoa maoni yao wakati Tume ya Jaji Warioba itakapoifanya kazi. Tulifanya mihadhara ya wazi zaidi ya 100,” amesema Sheikh Mselem.

Amesema mwanzo walifanya mihadhara zaidi ya 100 Zanzibar, kwa ajili ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa upatikanaji Katiba hiyo, kwa kuwa Serikali ilitaka.

“Mimi ni raia wa kawaida si mwanachama wa chama chochote katika chama cha siasa, kwa ujumla sio mwanasiasa. Lakini ile fursa ilipotokea na kwa kuzingatia mimi nimesoma kwenye Katiba kila mtu anayo haki ya kutoa maoni yake, ilipotokezea ile fursa ndiyo tukaitumia,” amesema Sheikh Mselem na kuongeza:

“Mara nyingi kwa muda mrefu viongozi wetu wananung’unikia ni kero za muungano. Ilipotokea ile fursa panatakiwa Katiba sababu hii iliyopo ilikuwa nje muda na haifai tena, inahitajika mpya inayoendana na wakati .Tukaona tutuimie hii fursa tupate Katiba bora.”

Mchakato wa Katiba mpya ulianza 2011 chini ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ambapo Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83 /2011 ilitungwa pamoja na Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.

Mchakato huo uliishia Aprili 2015, katika maandalizi ya wananchi kuipigia kura Katiba pendekezwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC), kuahirisha zoezi hilo kutokana na uandikishaji daftari la wapiga kura kutokamilika.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!