May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia awapa milion 10 wafanyakazi Dawasa

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa Sh.10 milioni kwa wafanyakazi bora wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) wa mwaka 2020/21. Anaripoti Ibrahim Yamola, Dar es Salaam … (endelea).

Ni mara baada ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kumaliza kuwakabidhi tuzo wafanyakazi bora wa Dawasa, katika mkutano wa kufunga mwaka wa fedha 2020/21 kwa watumishi wa mamlaka hiyo. Dawasa inahudumia mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Alipoanza kuzungumza na wafanyakazi hao, Waziri Aweso amesema, “nawaletea salamu za Rais wetu mpendwa, anafuatilia mkutano huu. Anawapongeza sana.”

Huku ukumbi wa Diamond Jubilee, ulipofanyikia mkutano huo wakishangilia, Aweso akasema “Rais ametoa Sh.10 milioni kwa wafanyakazi bora wote.”

Mara baada ya kutangaza zawadi hizo, Waziri Aweso alimwita Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja naye kusogea kwenye kisemeo ‘MIC’ kutangaza zawadi zake.

Hata hivyo, Mhandisi Luhemeja, aliomba awasiliane kwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasa, Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange ambaye, baada ya kujadiliana kwa takribani nusu dakika, Mwamunyange alisogea kwenye kisemeo.

Huku wafanyakazi wa Dawasa zaidi ya 2,300 wakishangilia, Jenerali Mwamunganye alisema, “bodi imeamua kutoa Sh.200,000 kwa kila mfanyakazi.”

Miongoni mwa walitunukiwa ni tuzo ya kujitoa kwa mfanyakazi, Erasto Majuto ambaye alionekana Mei Mosi 2021, katika picha akiziba bomba lililopasuka wakati wa mvua.

Waziri Aweso alitumia picha hiyo katika ukurasa wake wa kijamii, kumpongeza Majuto akisema “nimemuona na kuguswa kipekee na mtumishi wa Dawasa, Erasto Majuto akipambana kudhibiti upotevu wa maji wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha jijini Dar Es Salaam.”

“Ni wazi anatimiza majukumu yake lakini ni moyo wa kizalendo kutokana na mazingira anayotekeleza hivyo kama motisha naahidi kumpa zawadi kama pongezi mtumishi huyu hasa leo ikiwa ni siku ya wafanyakazi.”

Leo Jumanne, kwenye mkutano huo, Waziri Aweso baada ya kumkabidhi tuzo amempongeza “kwani alifanya kazi ya kizalendo, wakati wa mvua na ninaomba CEO, nasikia Majuto hana mkataba, kama ana vigezo basi aajiliwe.”

Kisha alimwita mbele na kumpa tena zawadi ya fedha ambazo hazikujulikana haraka haraka ni kiasi gani.

Tuzo ya mfanyakazi bora wa Dawasa, imekwenda kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja.

error: Content is protected !!