Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kina Mbowe washinda pingamizi la pili
Habari za SiasaTangulizi

Kina Mbowe washinda pingamizi la pili

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wenzake wakiwa mahakamani
Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano jijini Dar es Salaam, imekataa kupokea kitabu cha kumbumbuku za mahabusu, chenye taarifa zinazodai Mohammed Ling’wenya, aliwekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ling’wenya ni mshtakiwa wa tatu katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kupanga vitendo vya kigaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, akiwemo Ling’wenya.

Wengine ni; Halfan Hassan Bwire na Adam Kasekwa.

Kitabu hiko ambacho shahidi upande wa mashtaka, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Arumeru, SP Jumanne Malangahe, aliiomba mahakama hiyo ikipokee kwa ajili ya utambuzi, kimekataliwa leo Alhamisi, tarehe 11 Novemba 2021.

Uamuzi huo, umetolewa na Jaji Joackim Tiganga, katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, inayowakabili Mbowe na wenzake ya kupanga njama za vitendo vya kigaidi.

Pingamizi hilo liliibuliwa na mawakili wa utetezi, wakiiomba mahakama hiyo isipokee kitabu hicho, kwa ajili ya utambuzi, kama ilivyoombwa SP Jumanne, wakidai shahidi aliyekileta kitabu hicho hakuweka msingi wa kuonesha kuaminika kwake pamoja na nyaraka hiyo.

Na wala hakuonesha mlolongo wa utunzaji kitabu hicho (Chain of Custody), kutoka mahakamani hapo hadi kumfikia yeye.

Akitoa uamuzi mdogo wa pingamizi hilo, Jaji Tiganga amesema mahakama hiyo inakataa kukipokea kielelezo hiko kwa ajili ya utambuzi, kwa kuwa shahidi ameshindwa kuonesha mlolongo wa utunzwaji wake.

“Mahakama inaona ili kuthibitisha kilelezo kimefika kihalali kwa shahidi lazima ionekana kimeombwa au kufuata utaratibu wa kupelekwa kwa shahidi na kuonekana kimeingia kwenye mkono wake.”

“Lakini kinajikuta kimefikia kwa shahidi bila kuonesha kimemfikia namna gani. Mahakama inaonesha hauko ushahidi wa kutosha kuonesha kilelezo hiko kimemfikiaje,” amesema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga amesema “hakuna ushahidi ulioonesha kiliombwa kwa mtunza vilelezo wa mahakama au alikitoa kwa upande wa mashtaka au shahidi ili kuonesha mtiririko wa Chain of Custody, shahidi anaonekana ameshindwa kutengeneza chain of custody, kwa sababu hiyo mahakama inakataa kupokea kilelezo hiki. Natoa Amari.”

Kufuatia uamuzi huo, Jaji Tiganga alielekeza shahidi huyo aendelee kutoa ushahidi wake aliouanza jana Jumatano katika kesi hiyo ndogo.

Wakati akitoa ushahidi wake mahakamani hapo jana Jumatano, SP Jumanne aliiomba mahahama hiyo ikipokee kitabu hicho kwa ajili ya utambuzi.

Katika kitabu hiko, kuna taarifa zinazodai Ling’wenya alifikishwa kituoni hapo tarehe 7 Agosti 2020, akitokea katika Kituo cha Polisi cha Kati Moshi mkoani Kilimanjaro, alikokamatwa kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi, tarehe 5 Agosti mwaka jana.

Hili ni pingamizi la pili kwa upande wa Mbowe na wenzake kushinda mahakamani hapo, likitanguliwa na lile lililowekwa juzi Jumanne, tarehe 9 Novemba 2021 na Wakili wa utetezi, Nashon Kungu dhidi ya nyaraka iliyoelezea namna Mbowe alivyokataa kutoa maelezo yake ya onyo mbele ya afisa wa polisi.

Wakili huyo, aliiomba mahakama hiyo isipokee nyaraka hiyo akidai Mbowe hakuandika maelezo yoyote.

Upande wa jamhuri uliiomba mahakama hiyo iondoe nyaraka hiyo ili shahidi wao, Jumanne Malangahe aliyekuwa akitoa ushahidi aendelee kutoa ushahidi wake.

Ilikuwa ni baada ya shahidi huyo wa jamhuri, akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, kuelezea jinsi Mbowe alivyogoma kuandikisha maelezo yake.

Mbowe aligoma kuandika maelezo hayo mbele ya Mwanasheria wake, Fredrick Kihwelo akisema “hayuko tayari kutoa maelezo yake mbele ya afisa wa polisi.”

Shahidi huyo alidai, Mbowe alipofikishwa kituo kikuu cha polisi tarehe 22 Julai mwaka huu, saa 6.51 usiku na yeye alikuwapo kituoni hapo.

Alidai, baada ya kuwa amefikishwa kituoni hapo alikabidhiwa mtuhumiwa huyo.

Shahidi huyo alidai, baada ya kujitambulisha nilimueleza, nataka kufanya naye mahojiano. Nilimuonya kwamba anatuhumiwa kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya kugaidi, kinyume cha kifungu cha 24 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Ugaidi.

Shahidi huyo alidai, nilimuekeza mtuhumiwa Mbowe tuendelee kuandika maelezo kama alivyoomba. Lakini alijibu kwamba hayuko tayari kutoa maelezo yake mbele ya afisa wa polisi.

Baada ya mahojiano hayo nilisaini na yeye alisaini.

Kesi hiyo inaendelea kwa shahidi wa kwanza kati ya wanne walioelezwa na Jamhuri itawaita kwenye kesi hiyo ndogo anaendelea kuutoa. Fuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

error: Content is protected !!