November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NGO’s zatoa mapendekezo kuiomba   Tanzania ikubali hoja za UN

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa (katikati)

Spread the love

 

MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), yametoa mapendekezo manne ili kuiomba   Serikali ya Tanzania,  iyakubali mapendekezo yaliyotolewa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), kupitia kikao cha tatu cha tathimini ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR), kilichofanyika tarehe 5 Novemba 2021, jijini Geneva, Uswisi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumatano, tarehe 10 Novemba 2021 na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) na Shirika la Save the Children, jijini Dar es Salaam.

Wito huo umetolewa na mashirika hayo baada ya Serikali ya Tanzania, ikiwakilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, katika kikao hicho, kukubali mapendekezo 108 (43%) kati ya 252 iliyopokea, ambapo ilikataa 132 (52%), huku 12 (4.8),iliahidi kuyazingatia.

Akisoma tamko la mashirika hayo, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, ametaja pendekezo la kwanza  ni Serikali ya Tanzania, kuyakubali mapendekezo iliyokataa ambayo yanagusa haki za kiraia.

“Serikali ya  Tanzania ifikirie zaidi na kuyakubali mapendekezo ambayo hayajakubaliwa hasa yale yanayogusa, haki za kiraia na kisiasa,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa ametaja pendekezo la pili kuwa ni “serikali iwashirikishe wadau wengine wa haki za binadamu, hususani Asasi za Kiraia na nchi wanachama zilitoa mapendekezo ili kujadili uwezekano wa kuyaboresha, kulingana na mazingira halisia ya nchi.”

Pendekezo la tatu lililosomwa na Olengurumwa, ni la nchi wanachama waliotoa mapendekezo hayo waangalie uwezekano wa kuyaboresha hasa ambayo hayakukubaliwa na ambayo yanafikiriwa ili Tanzania iweze kuyabali.

Pendelezo la mwisho lililosomwa na Olengurumwa, ni la kuwataka qatetezi wa hali za binadamu nchini, kupitia rasimu ya ripoti hiyo ya UPR.

“Watetezi wa haki za binadamu wapitie rasimu hii ya repoti ya kikao cha tatu, cha UPR ili kuwasilisha mapema hoja zao kwa ajili ya  kuishauri Serikali juu ya mapendekezo yaliyotolewa. Hivyo tunawaomba viongozi wa mamlaka mbalimbali za Serikali kuchukua maoni ya wadau mbalimbali ili kufanya marekebisho katika mapendekezo yaliyokataliwa kabla ya kutoa maamuzi ya mwisho,” amesema Olengurumwa.

Awali, Olengurumwa alitaja baadhi ya mapendekezo ambayo Tanzania haijayakubali, ikiwemo yanayohusu haki za kiraia na kisiasa,  kama haki ya kupata dhamana na kutowekwa rumande kinyume na sheria.

” Haki nyingine ni ya ufutwaji adhabu ya kifo, pamoja na nchi kuridhia mikataba ya kimataifa inayolenga kukomesha vitendo vya utesaji binadamu,  pamoja na ulinzi dhidi ya kupotezwa. Mabadiliko ya sheria zinazohusu uendeshaji asasi za kiraia na kazi za watetezi wa haki za binadamu, haki za wakimbizi na watoto kuhusu mabadiliko ya sheria ya ndoa ya 1971, dhidi ya ndoa za utotoni,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amesema “mapendekezo mengine ambayo hayajakubaliwa katika mapitio ya mwaka huu 2021, yanagusa haki za msingi katika maeneo mbalimbali kama, haki za kijamii, uhuru wa kujieleza, haki za kiuchumi, haki za watetezi wa haki za binadamu, uhuru wa asasi za kiraia, haki za kisiasa , mikataba ya kimataifa, maboresho ya sheria na haki za binadamu kwa ujumla.”

error: Content is protected !!