Saturday , 27 April 2024
Home Kitengo Biashara Kilo 4.3 za dhahabu zadakwa zikitoroshwa
BiasharaTangulizi

Kilo 4.3 za dhahabu zadakwa zikitoroshwa

Spread the love

Katika kuhakikisha Tanzania inalinda rasilimali madini ili zichangie maendeleo ya nchi na kuinua uchumi wa watanzania, Serikali imesimamisha leseni zote nchini za Kampuni ya Nadoyoo Mineral Trading baada ya mmoja wa wahusika wa kampuni hiyo kukamatwa akitorosha dhahabu takribani kilo 4.3 zenye thamani ya zaidi ya Sh 562.2 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Hayo yamesemwa jana  tarehe 11 Oktoba, 2023 usiku na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Wilayani Kahama baada ya kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo.

“Serikali haitakubali kuona watu wachache wanajihusisha na vitendo hivyo viovu vya kutorosha madini. Nataka niwaambie, tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote tutakayemkamata akijihusisha na utoroshaji wa madini.

“Nilipoingia Wizara ya Madini mwezi mmoja uliopita nilisema, ukitaka kufahamu sura yangu nyingine basi jaribu kutorosha madini. Sasa basi, kuanzia leo mtu yeyote atayekamatwa kwa kosa la kutorosha madini, tutakwenda kusimamisha leseni zake zote nchi nzima wakati tukisubiri hukumu ya vyombo vya sheria, na iwapo mahakama itabaini mhusika ana hatia, tutakwenda kuchukua hatua kali ikiwemo kufuta kabisa leseni zote na kuhakikisha hatajihusisha tena na biashara ya madini nchini” aliongeza Mavunde.

Sambamba na hilo, Mavunde alitoa wito kwa wafanyabiashara wa madini kuwa wazalendo kwa kufuata taratibu zilizopo na kulipa tozo, ada na kodi mbalimbali ili kuiwezesha Serikali kupata mapato na kuendelea kuimarisha huduma kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara, umeme, afya na elimu.

Pia, Mavunde alionesha utayari wa kutenga siku na kukaa pamoja na wafanyabiashara wa madini ili kwa pamoja wamweleze hasa ni nini wanadhani inaweza kuwa ni changamoto kubwa inayopelekea baadhi yao kufikia hatua ya kujihusisha na vitendo vya utoroshaji madini, hatua ambayo anaamini itasaidia Serikali kuchukua njia sahihi kushughulikia suala hilo.

Vilevile, Mavunde alieleza bayana kuwa pamoja na hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watoroshaji wa madini, pia madini yote yatakayokamatwa yatahifadhiwa na Serikali na kupelekwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kusubiri hatma ya Mahakama.

Awali, akieleza taarifa ya masoko ya dhahabu, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Madini Kahama, Jeremiah Hango alibainisha kuwa takribani kilo 562.3 za dhahabu zenye thamani ya Sh 74.8 bilioni ziliuzwa katika masoko na vituo vya madini kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2023 hadi 10 Oktoba, 2023.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini na kuahidi kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha vitendo vyote vya utoroshaji wa madini vinakomeshwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Jacob, Malisa waachiwa kwa masharti

Spread the love  JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,...

Biashara

Sloti ya Mega Jade kasino njia 10 za malipo unaposhinda

Spread the love  TUNAKULETEA mchezo wa kasino wa kufurahisha sana ambapo unapewa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!