Wednesday , 1 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kigoma walia rushwa ugawaji vitambulisho vya NIDA
Habari za Siasa

Kigoma walia rushwa ugawaji vitambulisho vya NIDA

Spread the love

BAADHI ya wananchi mkoani Kigoma wameilalamikia Mamlaka ya Taifa ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa madai kuwa baadhi ya maofisa wake mkoani humo wamekuwa wakiweka ugumu katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo ili kutengeneza mazingira ya rushwa. Anaripoti Faki Sosi, Kigoma …(endelea).

Malalamiko hayo yalitolewa wiki iliyopita katika mkutano wa Wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa Kigoma.

Baraza hilo linajadili ajenda ya kutopatikana kwa vitambulisho vya Taifa hali inayotajwa kuathiri biashara za wajasiriamali hususani wanaofanya biashara za kuvuka mpaka nje ya Tanzania.

Mmoja wa wananchi hao, Sadiki Chanda amedai NIDA imekuwa ikiwanyima vitambulisho wakazi wa Kigoma hali inayoendeleza unyanyasaji kwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji pindi wanapowakamata wakazi wa mkoa huo.

Amesema ugawaji wa vitambulisho hivyo umekuwa kama biashara na kuongeza; “Raia kama hujatoa chochote unaweza usikipate hicho kitambulisho hicho.

“Binafsi nimeshakwenda zaidi ya mara nne kutafuta kitambulisho hicho lakini mpaka leo sijapewa na hiyo ndio fimbo ya kutuadhibia,” alisema Chanda.

Amesema kwenye fomu zao za kuombea kitambulisho hicho zinawekwa alama ya ‘B’ wakiwa wanakuhisi unatokea Burundi, ‘R’ wakikuhisi unatokea Rwanda na alama C wakimaanisha ni Mkongo .

Kauli ya Chanda iliungwa mkono na Albano Mateo ambaye ni mkazi wa Kasulu mjini, kwamba usumbufu wanaoupata kutoka kwa maofisa uhamiaji unatokana na NIDA kuwawekea vikwazo wakazo hao katika suala la upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ambavyo vinamtambulisha raia husika.

“Maofisa uhamiaji waliwahi  kunishusha kwenye Geti la Kakonko nikiwa kwenye gari nilikuwa natokea Mwanza kwenye biashara zangu, nilikuwa narejea nyumbani Kasulu. Nilikamatwa kwa kudhaniwa kuwa mimi sio raia wa Tanzania,” amesema.

Albano alisema maofisa hao walimpekua kisha kumweka mahabusu kwa muda wa saa mbili baada ya kujiridhisha kuwa ni raia ndipo wakamuachia.

“Lakini wakati huo tayari washanipotezea muda, washakwamisha biashara zangu na kunipa gharama nyingine za usafiri” amesema Mateo.

Amesema kuwa maofisa wa Nida wangekuwa wanawajibika wasingesumbuliwa namna hiyo na maofisa uhamiaji.

Akijibu malalamiko hayo, Ofisa wa NIDA mkoa Kigoma, Odoyo Albertus amesema zaidi ya vitambulisho 250,000 vimeletwa mkoani humo kwa ajili ya kugawiwa kwa walioomba.

Thobias Andengenye

Amesema vitambulishon hivyo vilielekezwa kwenye ofisi za watendaji wa kata na kwamba wananchi wote wanatakiwa kwenda kwenye ofisi za watendaji wa kata kuchukua vitambulisho vyao.

Akizungumzia malalamiko ya waliohojiwa kutopata vitambulisho, alisema kuwa mkoa ulipokea majina ya watu 255,000 waliokuwa na changamoto mbalimbali kubwa, ikiwamo uraia na kutakiwa kurudi tena kufanyiwa uhakiki.

Amesema ni watu 41,000 waliorudi na kuhakikiwa huku wengine wakiitangaza NIDA vibaya kwamba ina usumbufu kupata vitambulisho.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoa wa Kigoma, Juma Chaurembo amesema kumekuwa na usumbufu mkubwa wa upatikanaji wa vitambulisho hivyo, jambo linalofanya watu wengi kukata tamaa kuvifuatilia.

Naye Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amewataka wananchi wa mkoa Kigoma kujitokeza kwenye ofisi za watendaji wa kata kuchukua vitambulisho vyao na wenye changamoto wafuate taratibu za kushughulikia changamoto hizo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!