May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kifo cha Magufuli: Spika Ndugai amwangukia Mama Samia

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amemuomba Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani, kukamilisha ndoto za aliyekuwa rais wa taifa hilo, Hayati John Magufuli (61), za kulifanya Jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Ombi hilo la Spika Ndugai, limetolewa leo asubuhi Jumatatu tarehe 22 Machi 2021, katika shughuli ya kuuga mwili wa Hayati Rais Magufuli, iliyofanyika kwenye viwanja vya bunge jijini Dodoma.

“Nilimwambia wakati ule, umesema sasa ni wakati wa Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, lakini Mungu anaweza kukuchukua wakati wowote kwa hiyo tutunge sheria, akasema sawa tukatunga sheria kufanya Dodoma kuwa makao makuu ,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amesisitiza “Rais Magufuli umeweza kuhamisha makao makuu kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, naamini hili litaendelezwa na serikali inayofuata. Ni jambo kubwa sana ilishindikana miaka mingi ikawezekana wakati wake.”

Spika Ndugai ameiomba Serikali ya Rais Samia kukamilisha miradi itakayopandisha hadhi ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, ikiwemo mradi wa bomba la maji kutoka Ziwa Victoria hadi jijini humo na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato.

“Hilo nalo tulibebe wakati linakamilika kuhakikisha bomba la maji linafikishwa Dodoma kutoka ziwa Victoria , tuhakikishe uwanja wa Msalato unajengwa, na mengine yote ya kuifanya mji huu kuwa kweli makao makuu kama ndoto ya rais wetu kama ilivyokuwa,” amesema Spika Ndugai.

Akizungumzia maisha ya Hayati Rais Magufuli enzi za uhai wake, Spika Ndugai amesema, takaukumbuka kwa jitihada zake za ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, hospitali, mradi wa bwawa kubwa la umeme ‘Stigler’s Gorge.

“Naimani mbegu uliyopanda ulipanda kwenye udongo mzuri, ulipanda mbegu ya barabara, madaraja ulijenga, masoko ulijenga ukanipa jina la mimi ndugu yako Soko la Ndugai, umefanya mengi. Umejenga meli, viwanja vya ndege,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai ameongeza “Umeendelea kujenga bwawa kubwa la Stigler’s Gorge, umejenga viwanda, shule vituo vya afya, hospitali za rufaa umejenga Magufuli, naimani mbegu hii umeipanda katika udongo mzuri , nasi tutahakikisha tunaikuza vizuri.”

Hayati Rais Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, kwenye Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.

Mwanasiasa huyo amefariki dunia miezi minne tangu, alipoapishwa kumalizia muhula wake wa mwisho wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, tarehe 5 Novemba 2020.

Hadi anapoteza maisha, Hayati Rais Magufuli aliiongoza Tanzania kwa miaka sita (2015-2021), baada ya kushinda kiti cha Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na 2020.

Mwili wa Hayati Rais Magufuli unatarajiwa kuzikwa Ijumaa ya tarehe 26 Machi 2021, kijijini kwao Chato mkoani Geita.

error: Content is protected !!