May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Ndugai awashukia wanaofurahia kifo cha Magufuli

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amewashukia watu wanaofurahia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli (61), kilichotokea Jumatano ya tarehe 17 Machi 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dodoma … (endelea).

Kiongozi huyo wa mhimili wa bunge, amewashukia watu hao leo Jumatatu tarehe 22 Machi 2021, wakati mwili wa Hayati Rais Magufuli ukiagwa na wabunge kwenye viwanja vya bunge jijini Dodoma.

Hayati Magufuli amefariki dunia katika Hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Akizungumzia kifo hicho, Spika Ndugai amewafananisha watu hao na nyani waliofurahia kifo cha mwenye shamba la mahindi, ambaye alikuwa anawazuia kula mahindi yake.

“Sasa iko hadithi ya wale nyani walioshambulia shamba la mkulima kwenye mahindi, wakifurahi sana mahindi yanapokuwa yanaiva wanavuna wanakula, walipopata habari mwenye shamba amefariki wale nyani walifurahi sana.”

“Naamini katika nchi yetu manyani wa namna hii hawakosekani, lakini wakasahau mwaka uliofika wakati mahindi kuiva wakarudi shambani kula mahindi wakasahau mwenye shamba alifariki mwaka jana wakawa wanasikitika,” amesimulia Spika Ndugai.

Spika Ndugai ameshauri Watanzania, wasiwe kama ngedere hao kwa kutofanya mambo mabaya ambayo hayati Rais Magufuli aliyakataza.

“Naamini mwenye shamba amefariki lakini sisi hatutakuwa wale ngedere kusema tutafanya tunavyotaka,” amesema Spika Ndugai.

Kuali hiyo, anaitoa wakati tayari Jeshi la Polisi nchini Tanzania katika maeneo mbalimbali nchini, linawashikilia watu kadhaa kutokana na tuhuma za kufurahia kifo hicho.

Kufuatia maombolezo ya kifo cha Hayati Rais Magufuli, Spika Ndugai amesema wametenga tarehe 30 Machi 2021, kuwa siku maalumu ya kuweka azimio la kumuenzi kiongozi huyo.

 

“Tumetenga tarehe 30 siku tutakayoanza bunge hapa, tutakuwa na programu maalumu ambayo tutaifanya ndani ya ukumbi wa bunge ambapo kutakuwa na azimio maalumu,” amesema Spika Ndugai.

Mwili wa Hayati Rais Magufuli unatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Chato mkoani Geita, Ijumaa tarehe 26 Machi 2021.

error: Content is protected !!