Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Katiba mpya: Dk. Kigwangalla ashambuliwa, ajitetea
Habari za SiasaTangulizi

Katiba mpya: Dk. Kigwangalla ashambuliwa, ajitetea

Dk. Hamisi Kigwangallah
Spread the love

 

DAKTARI Hamis Kigwangalla, Mbunge wa Nzega Vijijini kupitia chama tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameibua mjadala makali wa mchakato wa katiba mpya akielezwa “aliyeshiba hamjui mwenye njaa.” Anaripoti Ibrahim Yamola, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Kigwangalla ameibua mjadala huo mitandaoni kupitia akaunti yake ya Twitter, baada ya kueleza mtazamo wake juu ya mkwamo wa katiba mpya na kinachoendelea kwa sasa.

Waziri huyo wa zamani wa maliasili na utalii, amekubaliana na kile alichoeleza Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa katiba ni muhimu lakini kwa sasa aachwe aisimamishe nchi kiuchumi.

Rais Samia, alitoa kauli hiyo tarehe 28 Juni 2021, Ikulu ya Dar es Salaam, alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari, kuhusu siku 100, tangu alipoingia madarakani, kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.

Samia aliyekuwa makamu wa Rais, aliapishwa kuwa Rais tarehe 19 Machi 2021, Ikulu ya Dar es Salaam ikiwa ni siku mbili kupita tangu kutokea kwa kifo hicho.

Katika mtazamo wake, Dk. Kigwangalla amesema “chama cha siasa huanzishwa kuwaleta pamoja watu wenye mawazo na sera zenye kufanana.”

“Lengo kuu ni kuleta ustawi wa watu. CCM haikuahidi mchakato wa Katiba kwenye ilani, bali ustawi wa watu. Nakubaliana na Mhe. Rais, kwa sasa tukomae na ustawi wa uchumi, Katiba baadaye!”

Mbunge huyo ameendelea kusema “kwa kuzingatia Katiba yetu ilipotoka, na uwepo wa mabadiliko makubwa ya mwaka 1984, na jinsi ilivyoweza kutuvusha kwenye kipindi kigumu cha msiba mzito kwa amani, na ilivyoweza kudumisha Muungano wetu kwa kipindi chote hiki, mabadiliko ya Katiba yanaweza kusubiri kidogo kwanza.”

Dk. Kigwangalla amesema, wale wanaodai katiba leo, ndiyo waliokimbia Bunge la Katiba. Walikimbia kitu gani na je walichokimbia kimeondoka ama kipo? Kama kipo wana uhakika gani kwa safari hii kitabadilika? Ama ni ajenda ya kisiasa tu kuwayumbisha wananchi na kujaribu kuchelewesha shughuli za maendeleo?

“Kama Katiba tuliyonayo imetuwezesha kuvuka kipindi kigumu cha msiba, na imetuwezesha kujenga barabara na kufikisha maji ya Ziwa Victoria Tabora, inafaa kuendelea nayo kwa muda mpaka hapo mahitaji ya kweli ya Katiba Mpya yatakapojitokeza. Tusikubali kutoka kwenye reli!,” amesema Dk. Kigwangalla

Bruno anayetumia jina la @wa_bruno amemjibu akisema “hayo ni maoni yako, mwana CCM, mbunge, na ex minister. Siwezi kushangaa maoni hayo kwakua alie shiba hamjui mwenye njaaa.”

Martin M.M @IAMartin_ amesema “@HKigwangalla Your incompetence is legendary. Miaka 69 baada ya uhuru bado tunahubiri maji, madawati na umeme?

“Karne ya 21? Bagaile, siyo lazima uwe na Ph.D ili kufahamu uhusiano wa katiba bora na maendeleo. Kitu ambacho ninaamini, Rais akiruhusu, utakuwa wa kwanza kuunga mkono.”

Jogoo la Shamba Mjini @JMariotz amesema “kumbe anayeamua katiba mpya iwepo ni chama cha siasa na siyo wananchi? Nahitaji kujifunza kitu kipya leo.”

Mwandishi wa vitabu mashuhuri, Richard Mabala @mabalamakengeza amesema “CCM wasitudanganye. Wao ndio walioanzisha mchakato wa katiba kwa gharama kubwa wakati watu walijitahidi elimu afya na maji pia.”

“Walipoona wananchi walitaka katiba tofauti na matakwa yao kwanza walivuruga mchakato kwa bunge la katiba KICCM tu kisha wakazika.”

Dk. Kigwangalla amemjibu Mabala akisema “Mwalimu Mabala, CCM hatukuvuruga mchakato, bali Chadema walisusia mchakato baada ya kuona hoja yao ya kuvunja Muungano haipiti! Kwenye kikao siyo lazima hoja yako ipite. Unapaswa usikilizwe lakini ujue tu walio wengi watashinda! Ndiyo demokrasia hiyo.”

Jchris@Jchris66283712 akamjibu Dk. Kigwangalla akisema “baada ya wengi kushinda ikawaje sasa?. Mbona unalaumu Chadema kama unajua kwamba wengi mlishinda?. Hiyo katiba ambayo wengi mlishinda iko wapi?”

Naye kibuga nandiga @kibuga_maga akasema “waliosusia mchakato ni wananchi baada ya kuiona CCM imevuruga mchakato wa Katiba wakawataka wawakilishi wao kupitia CDM na NGO’s wasiendelee kupoteza fedha za walipa kodi kwa upuuzi ulioanza kuonyeshwa na CCM.”

Naye @iamZature akamhoji Dk. Kigwangalla akisema “kiongozi unataka kusema mchakato wa katiba utasimamisha shughuli za kiuchumi,?

“Yaani imekua vita hiyo, kumbuka hayo madeni yasiyolipika yamesababishwa na katiba inayolalamikiwa, wasemeeeni wananchi wenu pasi na unafiki Liquidy muachie piere.”

Naye @erickkimanijr akasema “kwani Kigwangalla hyo PhD uliyonayo huionei huruma kaka?

“Mbona unaitumia vibaya pasipo kufkria hata kidogo. Woenee wana Nzega huruma wanao mbunge wa ajabu sana kuwahi kutokea katika historia ya nchi.”

Mchakato wa Katiba ulioanza mwaka 2013 na kuishia Katiba Inayopendekeza Aprili 2015, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuahirisha kwa kura ya maoni kutokana na uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kutokamilika.

Rais wa Tanzania,
Samia Suluhu Hassa

Mara baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani Oktoba mwaka 2015, chini ya Hayati John Magufuli, aliahidi kuundeleza mchakato huo hadi kupatikana kwa katiba mpya na kuiainisha kwenye ilani ya uchaguzi yam waka 2015/20.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 11 aliyoitoa tarehe 20 Novemba 2015, bungeni jijini Dodoma, alizungumzia Katiba mpya akisema, “Serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika awamu iliyopita kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura.”

“Napenda kuwahakikishia kuwa, tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa,” alisema Rais Magufuli

Alisema “tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba.”

Hayati John Magufuli

Ahadi hiyo ya Rais Magufuli, ilipewa nguvu katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/20, kifungu cha 144 (e) iliposema “mchakato wa kutungwa kwa Katiba mpya umeendeshwa na umefikia hatua ya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba ambayo itapigiwa Kura ya Maoni na wananchi”

Katika kifungu cha 145 (g), CCM itahakikisha, inakamilisha mchakato wa kutunga Katiba mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025, haikuzungumzia lolote kuhusu mchakato huo na hata hotuba ya Rais Magufuli wakati akizindua Bunge la 12 jijini Dodoma tarehe 13 Novemba 2021, hakugusia kabisa suala la Katiba mpya.

Naye Rais Samia alipokwenda kuzungumza na Bunge, tarehe 22 Aprili 2021, hakugusia suala la katiba mpya.

1 Comment

  • Nzega vijijini hatuna Mbunge
    Wananchi wameshajua nsiyo maana hawaendi kwenye mikutano yake

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!