ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk. Benson Bagonza, amewashauri watu wanaotaka au kupinga upatikanaji wa katiba mpya, watafakari udhaifu na mazuri ya Katiba iliyopo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Askofu Bagonza ametoa ushauri huo jana tarehe 5 Julai 2021, akichangia mjadala wa marekebisho ya Katiba iliyopo, uliobuliwa na makundi mbalimbali hasa wanasiasa na wanaharakati.
“Tukisema Katiba mpya, msitazame uzuri na ubaya wa Katiba iliyopo. Tazameni uzuri au ubaya wa Katiba inayodaiwa,” ameandika Dk. Bagonza.
Askofu Bagonza ameshauri mjadala wa kitaifa kuhusu upatikanaji wa katiba mpya, uanzishwe ili watu wajadili namna ya marekebisho ya Katiba iliyopo, kwa ajili ya kuondoa mapungufu yake.
“Wanaodai katiba mpya wako katika makundi matatu makuu, wanaosema ipitishwe Katiba pendekezwa. Wanaosema tuanzie Jaji Joseph Warioba alipoishia pale alipokabidhi kwa Bunge na wanaosema tuanzie kwenye sheria inayoruhusu kuandika katiba mpya.
“Yote yanatatulika kwa njia ya kuruhusu mjadala wa kitaifa. Hekima ziko nyingi zikiruhusiwa kufanya kazi,” ameandika Askofu Bagonza.

Samia Suluhu Hassa
Askofu Bagoza ameandika kuwa, wanaotaka marekebisho ya Katiba hoja yao kuu ni kupunguza madaraka ya rais na kwamba wanahitaji Katiba iwe na nguvu kuliko taasisi ya urais.
“Hoja ya Katiba mpya pamoja na sababu nyingine nyingi, inalenga kupunguza au kuondoa mgongano wa hatari kati ya ukuu wa Katiba na ukuu wa rais. Kwa hali ilivyo, rais na Katiba wako vitani.”
Katika mjadala huo, wanaopinga marekebisho ya Katiba wanasimamia hoja ya kwamba, ubora wa Katiba iliyopo umeonekana katika mchakato wa ugatuaji madaraka, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuingia madarakani kwa amani.
Kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Hayati Dk. John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021, kwenye Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam. Mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi 2021.
Akizungumzia hoja hiyo, Askofu Bagonza ameandika “Katiba hii haikutuvusha salama wakati wa msiba. Tulivushwa na hekima za watu na uvumilivu wa watanzania. Hekima, uzuri, uvumilivu na utu wa watu ni vitu vinavyopita. Tusiwekeze sana katika hivyo, tuviweke katika katiba mpya.”
Askofu Bagonza ameshauri kama mchakato wa marekebisho ya Katiba utafanyika, itakayopatikana iwe na nguvu kuliko taasisi ya urais.
“Rais (taasisi) tuliye naye ni mkuu kuliko Katiba, hata kama ni Katiba hii hii inayomleta madarakani. Ukuu wa Katiba hukoma pale inapomwingiza madarakani. Kinachobakia ni ukuu wa rais asiye mwanadamu wala Mungu. Ni hatari,” ameandika Askofu Bagonza.
Askofu Bagonza ameongeza “anayevunja Katiba hii anaweza pia kuvunja Katiba mpya inayodaiwa. Tofauti ipo kwenye madhara ya uvunjaji wa Katiba. Mpya ije na madhara yasiyomtegemea rais mvunjaji kujiwajibisha.”
Kiongozi huyo wa kiroho ameshauri Watanzania waweke pembeni tofauti zao pembeni, ili wapate muafaka juu ya upatikanaji wa Katiba mpya, yenye kukidhi matakwa ya wananchi.
“Nawasihi wanaojadili, watulize mioyo yao. Wasikilize kabla ya kusema na kama wakiweza, wasahau tofauti zao kwa muda wanapojadili suala hili. Tunaposema rais, msimwangalie Rais Samia. Itazame taasisi ya urais. Hata Rais Samia siku moja anaweza kujikuta ni mhanga wa maguvu yaliyo katika taasisi hii ya urais. Tumkumbuke Chiluba na Kaunda,” aliandika Askofu Bagonza.
Leave a comment