Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kambi Maalim Seif ‘wamwaga mboga’
Habari za SiasaTangulizi

Kambi Maalim Seif ‘wamwaga mboga’

Spread the love

MGOGORO ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) unachochewa na waliopo nje ya chama hicho hivyo kuwa na wakati mgumu kumalizwa. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Siku moja baada ya Kambi ya Prof. Lipumba kueleza kuwa, Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) imesajili Bodi ya Wadhamini iliyoundwa na kambi hiyo, kambi inayoundwa na Maalim Seif imeeleza kwamba, ahaitavumilia ‘uhuni’ huo na kwamba, inakwenda mahakamani.

Kambi ya Maalim Seif imeeleza kuwa, haitavumilia hujuma zinakazofanywa na kambi ya Prof. Lipumba na kwamba, iko tayari kujilinda kwa gharama yoyote.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 9 Machi 2019 jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu CUF Bara, Joran Bashange baada ya kambi ya Prof. Ibrahim Lipumba, mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutangaza kwamba bodi yao ya wadhamini.

Jana tarehe 8 Machi 2019 akiwa kwenye Ofisi Kuu  ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam, Nagdalena Sakaya Naibu Katibu Mkuu Bara (Kambi ya CUF Lipumba) pia Kaimu Katibu Mkuu wa CUF wa kambi hiyo alisema, bodi hiyo sasa ni halali baada ya kusajiliwa rasmi na Rita licha ya kuwepo kwa mvutano wa awali.

“Tuliwasilisha upya maombi kwenye ofisi ya RITA ili bodi yetu iweze kusajiliwa, kwa hiyo nafurahi kuwajulisha rasmi kwamba, nimetumiwa barua rasmi tarehe 6 mwezi huu kutoka Rita na sasa bodi yetu imesajiliwa rasmi,” amesema Sakaya.

Hata hivyo, Bashange ameeleza kuwa, mawakili wa chama hicho wako katika hatua za mwisho za kuwasilisha kesi mahakamani, kupinga usajili huo aliouita wa kihuni na usiozingatia sheria na Katiba ya CUF toleo la mwaka 2014.

“Katika hali isiyo ya kawaida, msajili wa vyama vya siasa alifanya kikao na genge la Lipumba tarehe 19 Februari 2019 na kuwasilisha majina upya RITA wakiomba usajili. Ni dhahiri kwamba, njama na hujuma za msajili zinaendelea,” amesema na kuongeza Bashange;

“Na kikubwa kinachotafutwa ni kutaka kulinda wizi wa ruzuku na kufuta kesi zote ikiwemo ile maarufu Na.23/2016 inayotegemewa kutolewa hukumu tarehe 18 Machi mwaka huu baada ya kuahirishwa mara nne. Ni imani yetu kama walivyoshindwa katika jaribio la kwanza mwaka 2017, watashindwa katika hatua hii ya sasa.”

Kuhusu fununu za kambi ya Prof. Lipumba kupanga kufanya mkutano mkuu hivi karibuni, Bashange amesema, kambi hiyo wameazimia kuipuuza mahakama kwa kutaka kuendelea na mkutano huo.

Na kwamba, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imezuia kuitisha mkutano kwa jina la CUF hadi pale kesi iliyofunguliwa  dhidi yao, itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

“Chama kilikwisha pata taarifa za njama hiyo ya uitishwaji wa Mkutano Mkuu wa Taifa feki wa Lipumba, na kupitia manaibu katibu wakuu wa chama, mapema tarehe 9 Mei 2018 walifungua shauri mama Na. 84/2018, na dogo Na. 248/2018 kupinga kuitishwa kwa mkutano huo feki,” amesema Bashange.

“Mahakama Kuu ilitoa hukumu baada ya kuhitimisha kusikiliza shauri dogo Na. 248/2018 na kutoa amri ya zuio ikimzuia Lipumba na genge lake au yeyote anayefanya kazi chini yao kuitisha mkutano huo kwa jina la CUF mpaka hapo shauri la msingi litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.”

Aidha, Bashange amesema wameshachukua hatua kadhaa kuzuia mkutano huo kufanyika, ikiwemo kumwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro na kunakili barua hiyo kwa Ofisi ya Rais , Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Polisi Ilala na jumuiya za kimataifa.

“CUF kwa kuheshimu utii wa sheria kimemwandikia barua IGP Sirro na jumuiya ya kimataifa, kumtanabaisha juu ya hatua hiyo, kuwataarifu kusudio la uvunjwaji wa amri halali ya mahakama.

“Katika hatua nyingine, meneja wa Lekam amepewa taarifa kumtahadharisha juu ya kujiingiza katika jinai ya kuingilia uhuru wa mahakama endapo ataendelea kukubali ukumbi wake kutumika kuvunja amri hiyo,” amesema Bashange.

Hata hivyo, Bashange amewataka watu walioitwa kuhudhuria mkutano huo kutohudhuria kwa kuwa CUF itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa wanakilinda chama hicho.

“CUF na viongozi wake haitawazuia wanachama wake kuchukua hatua zozote kwa kadri watakavyoona inafaa ili kuzuia mkutano huo,” amesema Bashange.

Mara kadhaa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) wamekuwa wakinyooshewa kidole kutokana na uamuzi wanaochukua ambao huumiza upande mmoja wa chama hicho.

Kambi ya Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF ndiyo inayolalamikia kuumizwa zaidi kuliko ile ya Prof. Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!