KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, imetoa mapendekezo manne kwa Serikali, juu ya namna ya kutatua changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Mapendekezo hayo yamewasilishwa bungeni jijini Dodoma, leo tarehe 8 Februari 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Joseph Mhagama, akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa kipindi cha kuanzia Februari 2022 hadi Januari 2023.
“Kamati inatambua kwamba, ukosefu wa ajira hasa kwa vijana ni changamoto ambayo ina athari kijamii na kiuchumi na kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ina wajibu wa kuratibu utekelezaji wa sera, sheria na mikakati ya kukuza ajira na kutoa huduma za ajira, ili kuongeza nafasi za ajira kwa watanzania ndani na nje ya nchi,” amesema Mhagama.
Mhagama ametaja mapendekezo hayo kuwa ni, Serikali kuongeza jitihada za kusimamia sera na sheria mbalimbali zinazoweka mazingira bora ya uwekezaji kwenye sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi na biashara.
Pendekezo lingine ni, Serikali kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili viweze kuajiri sehemu kubwa ya nguvu kazi nchini na vijana wengine kujiajiri wenyewe, huku lingine likiwa ni kubuni utaratibu madhubuti wenye uwazi ambao utaratibu zoezi zima la ajira Serikalini kwa namna ambayo, nafasi zitakozajazwa zitaakisi umoja wa kitaifa, bila kuathiri vigezo.
“Kuwa na mpango wa kuhamasisha vijana nchini kujifunza stadi za kazi za kimkakati na baadae kuwaunganisha vijana hao na fursa za kazi zenye staha nje ya nchi, kulingana na ushindani wa soko la ajira la kimataifa katika sekta za mbalimbali kwa kushirikiana na balozi zetu,” amesema Mhagama.
Katika hatua nyingine Mhagama amesema, kamati hiyo inaishauri Serikali kuweka mikakati ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya 2007, ili kuwawezesha vijana katika utekelezaji wa masuala ya maendeleo.
Leave a comment