May 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Mutungi awapa maagizo Jukwaa la Katiba Tanzania

Spread the love

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Francis Mutungi ameitaka Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) kuhakikisha inapigia upatu sera ya siasa safi na kwenda kunadi sera hizo katika jamii kwanza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea)

Jaji Mutungi ametoa maagizo hayo leo Alhamisi tarehe 11 Juni 2020 alipokutana na Jukata ambayo ipo chini ya mwamvuli wa Ushiriki Tanzania ofisini kwake jijini Dodoma ili kujadili masuala kadhaa ikiwemo utungwaji wa sera ya ushiriki wa makundi maalum katika siasa.

“Kama tunataka kuongelea ushiriki wa watu wenye ulemavu, twendeni huko katika familia zenye watu wenye ulemavu kuona matatizo yao,” amesema

Amesema ni muhimu kwa asasi za kiraia kuandaa jamii kubadili mtazamo wa makundi maalum na ushiriki wao katika siasa.

Amesema lazima kuiandaa jamii kuwaona watu wenye ulemavu wana haki katika kuongoza badala ya kutengeneza mazingira ya kujiona walichaguliwa kwa sababu ya ulemavu wao.

“Nasisitiza, tuanze na jamii yetu kisha ndipo tutengeneze huu mfumo mwingine wa ushiriki,” amesema

 Jaji Mutungi amesema, ni muhimu kuingiza ajenda hizi kwa jamii wanapomchagua mtu wanamchagua kulingana na uwezo wake na sio kwa sababu ya ulemavu wake au kwa sababu ni mwanamke.

Msajili huyo, ameshauri Jukata kuhakikisha wanapotaka kupeleka ajenda zao kwa jamii au kwa serikali wateue wajumbe wanaoweza kupeleka hoja kwa usahihi  na kizalendo.

“Kikubwa kinachohitajika ni kuhakikisha tunapokwenda kupeleka hii ajenda  ya ushiriki wa makundi maalum, tuhakikishe tunaenda kufanya siasa safi,” amesema

Amesema hata masuala ya ushiriki wa wanawake ni muhimu kuyasimamia lakini tukumbuke kuwa wapo wanawake ambao wameonyesha uwezo  mkubwa katika siasa na hao wanakuwa mfano wa kuigwa.

“Lakini kikubwa ni kuwa siasa safi inayobeba yote mnayotaka kufanikisha katika ajenda zenu,” amesema

Kuhusu ofisi yake kuhamia Dodoma, Jaji Mutungi amesema kwa sasa makao makuu ya ofisi ya Msajili ni Dodoma na wadau wengine wanaweza kupata huduma katika ofisi ya ndogo ya Dar es Salaam inapobidi.

“Haileti maana kuendelea kubaki Dar es Salaam wakati tayari Rais kahamia Dodoma,” amesema

Kwa upande wake, Mshauri Mwelekezi wa Jukata, Deus Kibamba, amesema walikutana na Jaji Mutungi, ili kufikisha ajenda ya jukwaa hilo chini ya mwamvuli wa Ushiriki Tanzania kuhusu ushiriki wa makundi maalum katika siasa.

Kibamba amesema, Jukata walifanya uchambuzi wa vifungu vya katiba, vifungu vya sheria na sera mbalimbali na kuorodhesha changamoto zinazokwamisha ushiriki wa makundi maalum katika siasa.

“Tuliona nafasi ya Msajili ni muhimu hasa katika kukuza demokrasia na malezi ya vyama siasa, tukasema tuzungumze naye ili tumpe mawazo tuliyoyaandika kuhusu ushiriki wa makundi maalum,” amesema

Kibamba amesema, Ushiriki Tanzania ilianzishwa ili kuibua vuguvugu la ushiriki wa makundi maalum katika siasa.

“Ni kweli zipo juhudi nyingi za Serikali lakini nyingi hazijazaa matunda badala ya kulalamika tukaunda Ushiriki Tanzania ili kumsaidia msajili na taasisi nyingine katika kuunda hizi siasa safi,” amesema

“Tulifanya uchambuzi kuonyesha hizo changamoto katika siasa za Tanzania ambazo zinaonyesha kuna ushiriki duni wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” amesema

Kibamba ameiomba ofisi ya Msajili iratibu wizara inayohusika na sera, kuratibu utungwaji wa sera ya ushiriki wa makundi malum.

Kibamba amesema, vipo vikwazo kadhaa vinavyowakabili wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikiwamo fedha za kampeni,  siasa chafu  na uteuzi  duni wa makuni hayo ndani ya vyama.

Kibamba ameshauri kuwe na ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC), Tume ya Taifa Uchaguzi Tanzania (NEC) na Ofisi ya Msajili ili kuongeza vigezo vya usawa  wa kijinsia.

Naye, Mwenyekiti wa Ushiriki Tanzania, Israel Ilunde, amesema ili kufanikisha kampeni ya siasa safi na ushiriki wa wananchi, ni muhimu kuwekeza  zaidi katika elimu ya uraia kwa  jamii.

“Lakini zaidi hasa tutaangalia ni nani anayeweza kubeba ujumbe kwa usahihi na kwa uweledi juu ya siasa safi,” amesema Ilunde

 

error: Content is protected !!