THOBIAS Andengenye, aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania amemshukuru Rais wa nchi hiyo, John Magufuli kwa kumsamehe. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea)
Andengenye amesema hayo leo Alhamisi tarehe 11 Juni 2020, saa chache baada ya Rais Magufuli kutangaza hadharani amemsamehe, kufuatia sakata la mkataba tata wa manunuzi ya vifaa vya zimamoto, wenye thamani wa zaidi ya Sh. 1 trilioni lililomng’oa madarakani.
Baada ya Rais Magufuli kutoa msamaha huo, MwanaHalisi Online limemtafuta Andengenye kujua alivyopokea msamaha, amesema, “nimepokea kwa furaha sana taarifa hiyo, namshukuru sana Mungu, namshukuru mheshimiwa Rais.”
Katika msamaha alioutoa Rais Magufuli alisema, atampangia kazi eneo jingine na si kumrudisha ndani ya jeshi hilo ambapo Andengenye ameahidi kutomwangusha Rais Magufuli pindi atakapompangia majukumu mengine.
“Kwa nafasi yoyote nitakayopangiwa kama itakuwepo, nitaendelea kuitumikia kwa uaminifu na kwa juhudi zangu zote na kwa maarifa yangu yote, hiyo ndio ahadi yangu,” amesema Andengenye
Andengenye pamoja na Kangi Lugola, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na maafisa wengine kadhaa wa wizara hiyo, walituhumiwa kuingia mkataba huo wa manunuzi bila kuangalia masilahi ya taifa.
Tangu Februari 2020, Takukuru ilikwisha ueleza umma kwamba uchunguzi umekamilika na suala na kubaini kuna kubaini linahusiana na uhujumu uchumi, watapeleka jalada hilo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi.

Mpaka sasa, Ofisi ya DPP haijatoa maelezo yoyote ya kipi kinaendelea mpaka.
Mapema leo Alhamisi, Rais Magufuli akifungua jengo la ofisi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na mambo mengine alitangaza kumsaheme Andengenye.
“Mliopo hapa mkafikishie salamu kwamba nimemsamehe na hapa kwa sababu ameomba msamaha zaidi ya mara tatu, ni unyenyekevu wa aina yake, lakini kwenye jeshi hili hatarudi mtamuona katika maeneo mengine,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufulii amesema viongozi waliopo sasa katika jeshi hilo wameufanyia marekebisho mkataba uliomfanya kumwondoa kwenye nafasi hiyo Andengenye.
Aidha, Rais Magufuli amewataka maafisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa waaminifu na fedha za umma, kwa kuwa katika uongozi wake hakuna fedha za bure.
“Niwaombe sana ndugu zangu wa zimamoto yaliyopita si ndwele tuyasahau na tusiyarudie. Fedha za bure katika kipindi changu ni mbaya zitawaharibia katika maisha yenu na mimi hata mloge namna gani sibadiliki,” amesema
Leave a comment