Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Jaji Mutungi, apigwa makavu: Ashutumiwa, apongezwa
Habari za SiasaTangulizi

Jaji Mutungi, apigwa makavu: Ashutumiwa, apongezwa

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
Spread the love

 

SIKU moja baada ya msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi, kuvitaka vyama vya siasa nchini humo kuacha kufanya mikutano na makongamano, vyama vya upinzani vimekosoa vikali kauli hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu tarehe 6 Septemba 2021, Jaji Mutungi alisema yuko mbioni kuitisha mkutano wa pamoja baina ya pande hizo kwa ajili ya majadiliano na hatimaye kumaliza msuguano unajitokeza mara kwa mara.

Msajili huyo alitaka shughuli zote, kama vile makongamano, zisimamishwe kwanza hadi utakapomalizika mkutano wa maridhiano baina yake, vyama vya siasa pamoja na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro.

”Nisinge penda kusikia kesho tena kuna kongamano linaandaliwa mahali. Ebu watupe nafasi,” alisema Jaji Mutungi.

Wachambuzi wanasema, hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutaka kuzileta pamoja kwenye meza ya maridhiano pande zote zinazokinzana, ni ya kuungwa mkono.

Hata hivyo, baadhi ya vyama vya upinzani na wakosoaji wengine wanahoji, ukimya wa ofisi hiyo katika kushunghulikia kadhia hiyo wakati vyama hivyo vikikumbana na zuio la kufanya shughuli zake.

Tangu mwanzoni mwa utawala uliopita wa Hayati Rais John Magufuli na sasa mrithi wake ambaye alikuwa makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani, serikali imepiga marufuku mkikutano ya kisiasa, ikiwamo makongamano na hata mikutano ya hadhara.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kimelazimika kusitisha vuguvugu lake la kudai katiba mpya kutokana na kubanwa na vyombo vya dola, ni miongoni mwa vyama vilivyokosoa kauli ya msajili huyo.

John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema 

”Yeye alipaswa kwanza awambie polisi waache kuvizuiya vyama vya siasa kutimiza wajibu wake wa kikatiba na kisheria; siyo kuviambia vyama visubiri,” ameeleza John Mrema, mkurugenzi wa itikadi, mawasiliano na mambo ya nje wa chama hicho.

Vyama vya upinzani nchini Tanzania, vinakabiliwa na kibarua kigumu cha kufanya siasa, kufuatia chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kubebwa na vyombo vya usalama.

Nacho chama cha NCCR-Mageuzi, ambacho hivi karibuni kilijikuta kikishindwa kufanya mkutano wake wa ndani wa Kamati Kuu (CC), kutokana na kuzuiwa na polisi, kimeingia katika orodha ya kuishutumu kauli ya Jaji Mutungi.

Mkuu wa idara ya uenezi na mawasiliano ya umma wa chama hicho, Edward Simbeye, ameeleza kuwa msajili angeenda mbali zaidi kwa kuandaa mkutano na waziri mwenye dhamana na mkutano na rais, ili tuzungumze haya mambo yanayoendelea nchini.

Mbali na Chadema na NCCR-Mageuzi, chama kingine ambacho kimempongeza na kusikitishwa kauli hiyo ya Jaji Mutungi ni Chama Cha Wananchi (CUF).

Taarifa ya Mhandisi Mohamed Ngulangwa, mkurugenzi wa habari, uenezi na mahusiano na umma wa CUF alisema uamuzi huo wa kuitisha kikao una lengo zuri lakini kuzuia mikutano haikubaliki.

Hata hivyo, chama hicho kimesikitishwa na kauli ya msajili ya kuvitaka vyama vya siasa kusimamisha makongamano na mikutano ya hadhara mpaka kifanyike kikao hicho ambacho hakijapangiwa tarehe.

“Kwa nafasi yake kama mlezi wa vyama, msajili alitarajiwa kutoa ufafanuzi wa sheria mbalimbali ili kulielimisha Jeshi la Polisi kwamba mikutano ya hadhara na makongamano ni ruhusa ya kisheria kwa vyama vyote, si CCM pekee,” alisema Mhandisi Ngulangwa.

Kumekuwa na mgawanyiko wa kimaoni tangu msajili wa vyama kuonyesha nia ya kutaka kuzileta pamoja pande hizo na hasa kutokana na msisitizo wake wa kumaliza uhasama baina ya polisi na vyama vya upinzani.

Kwa muda mrefu sasa, upinzani umekuwa unamuona msajili wa vyama, kama wakala wa chama tawala.

Endapo hatua ya msajili ya kusaka maridhiano baina ya polisi na vyama hivyo itafanikiwa, yaweza kufungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini.

1 Comment

  • MUTUNGI ACHA KUCHEZA NA AKILI ZA WA TZ CHEZA NA “SHARUBU” ZAKOKAMA NYINYI MLOTEULIWA NA RAIS HAMFATI MAAGIZO YAKE NINANI ATAKUSIKILIZA KAMBARE WEWE?…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!