September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Chadema yamgomea msajili Jaji Mutungi

John Mrema, Mkurugenzi wa Itikadi Uenezi na Mawasiliano Chadema

Spread the love

 

CHAMA kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimekataa wito kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, wa vyama hivyo kukutana na Jeshi la Polisi, kwa ajili ya kumaliza tofauti zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Msimamo huo umetolewa leo Jumanne, tarehe 7 Septemba 2021 na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, akizungumza na wanahabari mkoani Dar es Salaam.

“Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Mutungi amesema atakutanisha vyama na Jeshi la Polisi, sisi msimamo wetu kama Chadema, hatupo tayari kushiriki mkutano huo,” amesema Mrema.

Ahadi ya kuvikutanisha vyama vya siasa na jeshi hilo, ilitolewa na Jaji Mutungi jana Jumatatu, baada ya kuibuka mvutano kati ya pande zote mbili, kufuatia hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya ndani ya vyama hivyo hasa vya upinzani.

Licha ya hayo, msajili huyo wa vyama vya siasa alivitaka vyama vya siasa kutofanya mikutano ya ndani na makongamano, hadi vitakavyokutana na Insepkta Jenerali wa Polisi nchini, IGP Simon Sirro.

Lakini Mrema amesema Chadema hakitatekeleza agizo hilo, akisema“tunamkumbusha Msajili badala ya kusimamisha shughuli za vyama, ambavyo vinafanyika kwa mujibu wa Katiba, anapaswa amuonye na amkanye IGP aache kuingilia shughuli halali za vyama vya siasa.

“Msajili wa vyama vya siasa ametoa kauli tusitishe mikutano yetu ya ndani na makongamano mpaka tutakapofanya kikao na IGP, tunatumia nafasi hii kumkumbusha msajili ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu kuwa, hana mamlaka ya kisheria kusimamisha shughuli za vyama vya siasa,” amesema Mrema.

Miongoni mwa vyama vya siasa vya upinzani vilivyokumbwa na kadhia ya kuzuiwa kufanya mikutano ya ndani na Jeshi la Polisi, kwa maelezo ya kudhibiti mikusanyiko inayochangia kueneza virusi vya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19), ni Chadema.

Kwa zaidi ya mara mbili Chadema kilizuiwa kufanya makongamano ya kudai katiba mpya, kilichopanga kufanya jijini Mwanza na mkoani Mara.

Chama kingine kilichozuiwa kufanya mkutano wa ndani ni NCCR-Mageuzi.

error: Content is protected !!