Monday , 29 May 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Hakuna serikali moja – Dk. Shein
Habari za SiasaTangulizi

Hakuna serikali moja – Dk. Shein

Spread the love

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amekana kuwepo mpango wa kuupeleka Muungano wa Tanzania kuwa wa serikali moja. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Dk. Shein amesema hakuna mpango kama huo unaotajwa kudhamiriwa kutekelezwa kwa ushirikiano na Dk. John Magufuli ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“… eti wanasema mimi nikishirikiana na Rais Magufuli tutaipeleka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchi ya serikali moja. Wanaosema hivi ni waongo na wanafiki,” alisema.

Dk. Shein ametoa msimamo huo mbele ya viongozi waandamizi wakiwemo mawaziri katika serikali anayoiongoza alipokuwa akizindua ujenzi wa mradi mkubwa wa maji mjini Zanzibar.

Msimamo wake huo ni majibu kwa maelezo aloyatoa Maalim Seif Shariff Hamad hivi karibuni alipokuwa kwenye ziara ya kukagua uhai wa chama cha CUF kote Unguja na Pemba ambako alihutubia mikutano ya ndani katika wilaya zote kumi za Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi Maalim Seif ambaye kwa miaka mitano alifanya kazi na Dk. Shein akiwa mmoja wa makamu wake wawili wa Rais wa ZanIbar, chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), alikuwa na agenda mbili kubwa ziarani mwake.

Ya kwanza ni kuhamasisha wananchi na hususan vijana kukichukua chama katika hatua mpya ijayo baada ya kudhoofishwa na mgogoro uliopandikizwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumtumia Profesa Ibrahim Lipumba, aliyejiuzulu uenyekiti Agosti 2015.

Ajenda ya pili ni kuelezea wananchi ni kwa kiasi gani Dk. Shein ameshindwa uzalendo wa Zanzibar hata sasa kuwa tayari kumsaidia Rais Magufuli kuigeuza jamhuri nchi ya serikali moja.

“Nina jambo nalijua nikwambieni,” alihoji wafuasi wa CUF na alipojibiwa “twambie” alisema “Mjomba Magu anataka kuigeuza jamhuri nchi ya muungano wa serikali moja ati akidai anatimiza dhamira ya Mwalimu Nyerere.”

Alisema amepata taarifa kuwa Rais Magufuli amemuita Dk. Shein na wakiwa pamoja na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, aliwaambia anataka kykamilisha yale yote ambayo Mwalimu Nyerere aliyakusudia kwa kutamka lakini asiwahi kuyatekeleza kwa sababu mbalimbali.

Akasema “mambo mengi yanakaa sawa lakini unajua huyu Maalim Seif bado ni tatizo kubwa kwetu… ndio maana naona njia nzuri ya kumalizana naye ni kukamilisha azma ya Baba wa Taifa ya kuwa na serikali moja tu Tanzania.”

Maalim Seif alisema baada ya maelezo yake hayo Rais Magufuli, Dk. Shein alibaki kimya na kuinamia chini lakini hapohapo Samia yeye akasema ‘Mheshimiwa Rais mimi naona hili jambo halitawezekana kwa sababu Wazanzibari hawalitaki.”

Alimsihi Dk. Shein kama atakubali kushirikiana naye watumie umma wa Wazanzibari kukataa mpango huo. “Mimi kama nilivowahi kumwambia Dk. Salmin wakati ule nitaongoza umma kukataa kuifuta Zanzibar. Vijana wa Zanzibar kaeni macho dhidi ya mipango ya serikali za CCM.”

Katika mikutano yake hasa ya wilaya tatu za Mkoa wa Mjini Magharibi – Mjini, Magharibi A na Magharibi B – Maalim Seif alihamasisha wanaCUF kuwa tayari kuchukua chama chao kuanzia Jumatatu ambapo Mahakama Kuu ya Tanzania itatoa hukumu ya kesi ya kupinga hatua ya Ofisa Mtendaji wa Serikali kuisajili Bodi ya Wadhamini isiyo halali ambayo iliteuliwa na Prof. Lipumba.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Uamuzi juu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi 13 Juni

Spread the love  MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR), imepanga...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jeshi la Polisi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti

Spread the love  JESHI la Polisi Nchini limesema kuwa katika kukabiliana na...

KimataifaTangulizi

Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Spread the love  MMOJA wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya Kimbari ya...

Habari za Siasa

Musoma Vijijini waomba ujenzi wa barabara uanze haraka

Spread the loveJIMBO la Musoma Vijijini, mkoani Mara, limeomba Serikali kuhakikisha ujenzi...

error: Content is protected !!