December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba, Maalim Seif nani kununa leo?

Spread the love

UAMUZI utakaofikiwa leo tarehe 18 Februari 2019 na Jaji Benhajj Masoud wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuhusu wajumbe halali wa Bodi ya Udhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), utapeleka kicheko ama kilio katika kambi mbili ndani ya chama hicho. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Kambi hizo ni ya Prof. Ibrahim Lipumba, mwenyekti wa chama hicho Taifa anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayolalamikiwa kuunda bodi ‘feki’ na Kambi ya Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa chama hicho.

Katika kesi hiyo namba 13 ilifunguliwa mwaka 2017 na Ally Saleh, Mbunge wa Malindi na mfuasi wa Kambi ya Maalim Seif, amepinga bodi mpya iliyoundwa na Prof. Lipumba kwamba imekiuka katiba ya chama hicho.

Ally anaiomba mahakama itamke kuwa, ni ipi bodi iliyoundwa kihalali kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba ya CUF 1992 toleo la mwaka 2014.

Ally kwenye kesi hiyo anawakilishwa na Fatuma Karume, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) akisaidiana na Wakili Mpale Mpoki dhidi ya Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) kwa kukubali uundwaji wa bodi mpya ya CUF. Kambi ya Prof. Lipumba inaongozwa na Wakili Majura Magafu.

Baada ya safari ndefu ya kusikiliza pande mbili zinazosigana kuhusu wajumbe halali wa Bodi ya CUF, uamuzi unaotarajiwa kutolewa leo na Jaji Masoud unatarajiwa kupeleka majonzi kwenye moja ya kambi hizo huku nyingine ikifurahia.

Iwapo Jaji Masoud ataona kuwa, bodi inayotajwa kuwa feki na upande wa Maalim Seif uundwaji wake ulifuata Katiba ya chama hicho pasi na shaka yoyote, Kambi ya Maalim Seif itaugulia maumivu huku ya Prof. Lipumba ikiangua kicheko.

Hivyo hivyo, Jaji Masoud kwa kupitia maelezo ya Fatuma Katime na msaidizi wake na pale atapojiridhisha kuwa, Prof. Lipumba hakuwa na uhalali wa kuunda bodi hiyo, basi jaji anaweza kusoma hukumu ambayo itakuwa maumivu kwa Prof. Lipumba huku Maalim Seif akiangua nderemo.

Ally ameeleza kwamba, baadhi ya majina yaliyowasilishwa Rita kusajiliwa kuwa si miongoni mwa majina yaliyopendekezwa kihalala na kwamba, yalipenyezwa kinyume na utaratibu.

Mussa Kombo, Asha Suleima, Hajira Silia, Amina Mshamu, Salha Mohamed, Peter Malebo, Azizi Dangesh na Abdul Magomba ndio wajumbe wanaolalamikiwa kuteuliwaNA Prof. Lipumba kinyume na utaratibu wa katiba ya chama hicho.

Waliopendekezwa na Kambi ya Maalim Seif na kisha kuenguliwa na Rita ni Mohamed Mohamed, Abdallah Khatau, Yohana Mbelwa Alli Suleiman, Juma Muchi na Joram Bashange.

Kwa upande wa Rita tayari wameeleza kuwa, wao hupokea majina ya wajumbe kutoka kwa viongozi wa vyama na kwamba, walipokea barua mbili tofauti kutoka CUF.

Hivyo, ili kuthibitisha uhalali wa barua ipi yenye majina itumike kama wajumbe halali wa CUF, Rita iliwasiliana na Ofisi ya Msajili wa Vyama kwa kuwa ndiye anayetunza kumbukumbu za vyama hivyo, majibu ya msajili yalikuwa barua iliyowasilishwa na Kambi ya Prof. Lipumba ndio halali.

Chama hicho cha upinzani cha tatu kwa ukubwa Tanzania Bara na cha pili kwa Tanzania Visiwani, kilitumbukia kwenye mgogoro mkubwa mwaka juzi.

Ni baada ya Prof. Lipumba kuandika barua ya kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti mwaka 2016 na mwaka juzi kuandika barua ya kutengua barua yake ya kujiuzulu.

Hatua hiyo iliibua mgogoro wa kiuongozi baada ya kuibuka kwa pande mbili, mmoja ikipinga kurejea kwake na nyingine kubarika kurejea kwake.

Kwa sasa Prof. Lipumba anatambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama mwenyekiti wa CUF.

Maalim Seif ni miongoni mwa wasiokubaliana na uamuzi wa Prof. Lipumba kurejea kwa kuwa, aliomba kutojiuzulu lakini alifanya hivyo bila kulazimishwa na yoyote.

Mzozo huo umeongeza changamoto katika kutekeleza majukumu ya shughuli za chama hicho.

error: Content is protected !!