Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Haihitajiki ‘damu mpya’ kuijenga Z’bar
Habari za SiasaTangulizi

Haihitajiki ‘damu mpya’ kuijenga Z’bar

Spread the love

WAZANZIBARI wanaoamini katika utawala mwema unaojali haki, ushirikishwaji na utu, wameshiriki kwa mara nyengine tukio la kukumbuka mauaji ya wananchi wenzao yaliyotokea miaka 18 iliyopita, mbele ya macho yao na macho ya ulimwengu. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Ni mauaji katili yasiyosahaulika, ambayo yalifanywa kuanzia kwenye misururu ya wananchi waliokuwa wameshikana na kushikamana wakishiriki maandamano ya amani yaliyolenga kushinikiza watawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kurudisha haki ya umma ya ushindi uliotokana na uchaguzi mkuu uliokuwa umefanyika miezi mitatu nyuma.

Mauaji hayo yaliyopewa jina maarufu la “mauaji ya tarehe 26-27 Januari” yalitekelezwa katika hatua iliyoelezwa kuwa ni ya kudhibiti maandamano haramu ya wananchi yaliyoitishwa na Chama cha Wananchi – The Civic United Front (CUF) – kilichoongoza kampeni ya nchi nzima kwa lengo la kudai haki yao baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 2000, kuvurugwa kwa makusudi kwa nia ya kuinufaisha CCM.

Baada ya mauaji hayo kutokea, serikali iliunda na kutuma tume maalum ya kuyachunguza ikiongozwa na aliyekuwa Brigedia mstaafu nchini Tanzania, Hashim Mbita. Wachunguzi hao walithibitisha kuwa watu wasiopungua 30 walipoteza maisha.

Waliotekeleza mauaji hayo pia walitajwa na Tume ya Brigedia Mbita kuwa ni askari wa serikali kutoka vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama – vikiwemo vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vile vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Inaelezwa zaidi ya watu 100 alijeruhiwa katika namna mbalimbali, mali chungunzima za wananchi ziliporwa na nyengine kuharibiwa; wanawake kadhaa wakiwemo wasichana, wanatajwa kufanyi wa kukatili, baadhi yao wakitendewa udhalilishaji mbele ya waume na au watoto zao.

Watu wengine kadhaa waliikimbia nchi yao na kwenda kutafuta hifadhi maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi, nchini Kenya. Ingawa maandamano yalihamasishwa nchi nzima, yalishamiri zaidi Zanzibar ambako ndiko hasa malalamiko ya uvurugaji wa makusudi wa uchaguzi mkuu yalitolewa; na basi ndiko nguvu kubwa ya serikali iliwekwa ili kuyavunja kwa kuwadhibiti waandamanaji.

Serikali, wakati huo ikiwa ya awamu ya tatu chini ya uongozi wake Rais Benjamin Mkapa, iliyaita “maandamano haramu” na kutangaza mapema kupitia viongozi wake wa kisiasa na Jeshi la Polisi, kuwa wangeyasambaratisha.

Na kweli, askari wengi na vifaa walipelekwa Zanzibar siku chache kabla ya Januari 27, siku ambayo CUF ilitangaza kuwa ndiyo maandamano hayo yatafanyika. Askari wengi walishuhudiwa wakishuka kwenye meli eneo la Forodha mchanga, karibu na Bandari Kuu ya Zanzibar, iliopo Malindi.

Askari wengine wakaonekana kupandishwa meli nyengine siku zilizofuata kukaribia siku ya maandamano, kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kisiwani Pemba ambako taarifa zilikuja kuthibitisha kuwa, muitiko wa wananchi kushiriki maandamano ulikuwa mkubwa na kwa hamasa.

Sehemu ya askari walibaki kisiwani Unguja wakishirikiana na wale waliokuwa kwenye vituo vyao vya kazi siku zote. Mkazo wa serikali katika kutekeleza walichokitaka, ulikuwa ni kwenye mji wa Zanzibar ambako ilitarajiwa ndiko kutakuwa kituo kikuu cha maandalizi na utekelezaji wa maandamano.

Dhamira ilidhihirika mapema kabisa. Idadi ya askari walitawanywa mitaani mjini Zanzibar kukaribia adhuhuri ya Ijumaa, tarehe 26 Januari na siku ya kulalia siku ya maandamano 27 Januari. Ijumaa inakuwa siku ya Waislam kutokeza kwa wingi kwenye misikiti kwa ajili ya sala ya Ijumaa. Basi misikiti ilikuwa na watu wengi.

Msikiti wa Muembetanga, mmoja wa inayotumika kwa sala ya Ijumaa, upo karibu na jengo la Makao Makuu ya CUF. Lakini ni karibu zaidi, kwa hakika ni mita tano tu, na zilipo ofisi kuu za chama hicho kwa Wilaya ya Mjini Unguja.

Mauaji ya kwanza yalitekelezwa hapa. Imam Juma Khamis, kijana mbichi aliyekuwa ndio kwanza amemaliza kuongoza ibada ya sala hiyo, alitwangwa risasi akiwa amesimama mlangoni kuashiria kutaka kutoka ili kwenda nyumbani kwake. Alianguka palepale na haikuchukua muda akawa amekata roho kwa kuwa muuaji wake alimlenga– alimpiga risasi kadhaa kifuani.

Mauaji haya ya Imam Juma yalitoa ishara ya wazi kwamba kesho yake siku ambayo ndiyo ya maandamano ya amani, hapatakuwa na lelemama. Ni wachache waliofikiri labda ilikuwa tishatoto.

Cha kujifunza hapa ni kuwa, mauaji haya yalifanywa bila ya kuwepo maandamano yoyote maana ni punguani tu atakayesema kuwa, baada ya kutoka msikitini Ijumaa Waislam waliandamana. Maandamano yalipangwa kuwa Jumamosi si Ijumaa.

Imam Juma hakuwa peke yake “aliyeanzwa” siku hiyo. Aliuliwa pia mzee Hamad, aliyekuwa anahangaika kukwepa zahma aloikuta eneo la karibu na Mtendeni alikopita kutokea Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui alikokuwa akifanyia kazi. Huyu baba alikuwa ni kada na mtumishi wa CCM.

Si hasha Polisi walitukanwa kwa kumuua yeye bali si Imam Juma ambaye alikutwa kweupeni kwenye mlango mkuu wa msikiti. Yumkini wakuu wa jeshi waliomba radhi kwa kumuua mzee Hamad kwa “bahati mbaya” maana ilikuwa wakati akikaza mwendo kuuvuka uchochoro nyuma ya makao ya CUF Mtendeni ili kuingia mtaa mkuu wa maduka wa Mchangani.

Hakika mauaji mabaya kabisa kutokea katika historia ya Tanzania yalitekelezwa Jumamosi; maandamano yalifanikiwa Unguja na yalikuwa makubwa zaidi kwenye miji ya Pemba – Mkoani, Chake Chake, Wete na Micheweni.

Vyombo vya habari vilithibitisha kupelekwa helikopta Micheweni ambayo ilivuruga wananchi kwa rubani kuizungushazungusha karibu kabisa na vichwa vya waandamanaji.

Wapo wananchi waliouliwa mitaani. Majumbani mwao. Wengine waliuliwa misituni wakati wakikimbia risasi. Askari walionekana wakiingia ndani ya vijiji kusaka wananchi, kiasi kwamba “walimshughulikia” kila waliyemkuta, pasina kujali. Ilikuwa ni kazi ya kutwa nzima hata baada ya serikali kujiridhisha kuwa maandamano yalishasambaratishwa.

Jioni ya Jumamosi operesheni iliendelea. Watu walifuatwa majumbani mwao. Askari walifanya walichokitaka. Usiku ule ulikuwa mwengine mgumu na mchungu kwa watu kulia na kugugumia pale walipotakiwa kuacha kulialia.

Familia nyingi za kisiwani Pemba zilikumbwa na fadhaa kubwa kwani zilipotelewa na wapendwa wao, wengine wakija kujulikana muda mrefu baadaye kuwa walifika Somalia.

Baadhi yetu tulisikizwa simulizi za namna askari walivyoua na kudhalilisha wananchi hata wale waliobaki majumbani mwao wasishiriki maandamano. Askari mmoja aliniambia kwa raha kabisa kuwa anakumbuka aliua watu saba kwa risasi kwenye dhahama hiyo. Hawa akiwakumbuka kwa kila kitu.

Hakujua idadi ya wengine kwengine. Huyu sasa ni marehemu baada ya kupatwa na ajali karibu na nyumbani kwake. Aligongwa na gari akiwa amepanda vespa kukata barabara.

Dhulma hiyo iliyohusisha umwagaji mkubwa wa damu haiwezi kusahaulika. Eti isemwe kuwa hakuna sababu tena ya wananchi kukusanyika inapofika Januari 27, ili kukumbuka wahanga.

Si utu huo. Wale binaadamu hawakuwa na makosa yoyote. Walijua walidhulumiwa. Walijua yeshakuwa mazoea. Bali walijua haki ni lazima idaiwe au ipiganiwe. Walishiriki kuipigania haki.

Sasa wenzao wawasahau vipi? Wanasahauje ukatili ule? Kuwakumbuka kwa dua ni muhimu kwa sababu walionewa. Lakini dhulma na maonevu ya namna ile hayajasimama. Na hayajasimama hata baada ya pale.

Mpaka leo Wazanzibari wanadai haki ya ushindi wa Oktoba 2015. Wanasema walidhulumiwa. Kupitia njia ileile ya kuuhujumu uchaguzi ili kujibakisha mamlakani. Wanasahauje kukumbuka umwagikaji damu ule wa wenzao?

Kwa yote hayo yaliyotokea, historia inabaki hivyo. Ni juu ya watawala hawa – CCM – kutambua kuwa dhulma ikiendelea, madai ya haki hayatopoa, yatashamiri tu.

Basi ni muhimu na kwa kweli walipopata panatosha, warudishe ubinaadamu wao kwa sababu kuijenga upya Zanzibar hakuhitaji damu nyengine kumwagwa. Iliyomwagwa inatosha na isirudiwe.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!