December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli anadanganywa na wasaidizi wake – Silinde

Rais John Magufuli

Spread the love

DAVID Silinde, mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Momba, mkoani Songwe amesema, Rais John Magufuli, amezunguukwa na watu waongo. Kila tunavyozidi kuelekea uchaguzi mkuu, ndivyo wanavyozidi kumuongopea. Anaripoti Mwanadishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Anasema, “Rais haambiwi ukweli. Anadanganywa. Jambo hili likiachwa kama liendelee kama lilivyo sasa, rais atashindwa kufanya majukumu yake na taifa litaweza kuangamia.”

Aidha, mbunge huyo anasema, “katika ofisi ya Hazina ya taifa, katibu mkuu wizara hiyo, anagawa fedha za umma kinyume na maelekezo ya Bunge.”

Silinde alitoa kauli hiyo bungeni, Jumamosi iliyopita – tarehe 2 Februri, wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti. Taarifa ya kamati ya Bajeti, iliyowasilishwa na George Simbachawene, mwenyekiti wa kamati hiyo. Simbachawene, ni mbunge wa Kibakwe (CCM).

Akizungumza kwa kujiamini Silinde alitoa mfano wa mkanganyiko uliyopo kwenye taarifa za serikali zinazohusu kukuwa kwa uchumi. Anasema, taarifa hizo nyingi hazina ukweli.

Alisema, “takwimu za serikali kuhusu ukuaji wa uchumi siyo za kweli. Ndio maana ukisoma taarifa za serikali zinazopelekwa kwa rais, zinatofautiana kwa kiwango kikubwa na zile zilizoko BoT (Benki Kuu ya taifa).

“Taarifa ya serikali inaonyesha uchumi wetu umekuwa kwa asilimia moja. Lakini BoT wanaeleza tofauti. Na hawa BoT ndio tunaopaswa kuwaamini kwa kuwa ripoti zao, zinasomwa na IMF (Shirika la fedha la kimataifa) na Word Bank (Benki ya Dunia).”

Hata hivyo, taarifa ya kamati ya Bajeti inasema, katika kipindi hiki cha miaka mitatu (2015-2018), uchumi wa taifa umekuwa kwa asilimia 7.0 ukilinganisha na asilimia 6.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2017.

Lakini papo hapo, Simbachawene anasema, “…utoaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo hauridhishi. Kati ya mafungu 92 ya serikali, ni mafungu 14 pekee yaliyopata fedha za maendeleo kwa zaidi ya asilimia 50.”

Anawataja wanaongoza kupata fedha nyingi, ni wizara ya mambo ya ndani. Anasema, wizara hiyo mpaka Desemba mwaka huu, ilikuwa imeshapokea asilimia 228 ya fedha zake za bajeti.

Lakini Silinde ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti anasisitiza, “uchumi wa taifa hauwezi kukuwa wakati soko la hisa linaporomoka na kupoteza mitaji.” Anasema, yanayoelezwa na serikali yote yanalenga kutaka kumfurahisha rais na kuhadaa wananchi.”

Kwa mujibu wa Silinde, hadi kufikia Novemba mwaka jana, soko hilo la hisa lilikuwa tayari limeshapoteza mtaji wa takribani Sh. 4 trilioni.

Anasema, ripoti ya Kamati ya Bajeti imeeleza kuwa serikali iliahidi kutoa Sh. 251 bilioni ili kukamilisha majengo ya shule za msingi na sekondari (maboma), yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.

Mpaka  sasa, serikali haijapeleka fedha hizo zinazokaribia Sh. 29.7 bilioni.

Anasema, “…haya hawayasemi. Hawaelezi kwa mfano, katika mwaka uliyopita – 2018/2109 – mapato ya serikali yalitarajiwa kupanda kwa asilimia 18, lakini yamepanda kwa asilimia mbili (2).”

Anahoji, “katika mazingira haya, uchumi hauwezi kukuwa.” Hakuna uchumi unaoweza kukuwa kwenye udanganyifu na kwenye takwimu zinazojikanganya. Uchumi utakuwa pale serikali inapolinda wawekezaji na kupeleka fedha za maendeleo kwa wakati.”

Anaongeza, “uchumi hauwezi kukuwa kwa sababu, wasaidizi wa rais wanamueleza kitu tofauti na kile wanachokieleza kwenye kamati za Bunge. Kinachoelezwa kwenye kamati na kwa rekodi hizo hizo za serikali, hakiendani na ukweli halisi.”

Anasema, “haya hawayasemi na hawamwambii hata rais. Wanaishia kuudanganya umma na kumdanganya rais.”

Anasema, “fedha zilizotumika bila idhini ya Bunge, ni nyingi sana. Ni mabilioni kwa mabilioni ya shilingi. Hii siyo sahihi. Ni kosa kubwa sana. Ni jinai kabisa; mtu wa kwanza atakayepelekwa gerezani baada ya Rais Magufuli kuondoka madarakani, atakuwa katibu mkuu Hazina.”

Aidha, Silinde amesema, serikali imeeleza kwenye kamati hiyo kuwa nchi wahisani, waliahidi kutoa kiasi cha Sh. 284 bilioni,lakini wametoa kiasi cha Sh. 4 bilioni tu.

Upungufu huo wa fedha, Silinde anasema, umesababisha serikali kushindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi. Alitoa mfano wa kutokamilika kwa majengo ya shule za Msingi na Sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya Bajeti iliyowasilishwa bungeni, serikali imepeleka sehemu ndogo sana ya fedha za maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge.

“…mwenendo wa utolewaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo, siyo wa kuridhisha. Mathalani, kati ya mafungu 92 ya serikali, ni mafungu 14 tu yaliyopokea fedha hizo zaidi ya asilimia 50,” inaeleza taarifa ya Kamati ya Bajeti.

 Wizara iliyoongoza kwa kupewa fedha nyingi za maendeleo, ni wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Imepelekewa asilimia 228. Wizara ya Mambo ya Ndani siyo wizara ya uzalishaji ama inayotoa huduma moja kwa moja kwa wananchi.

Sekta zinazotoa huduma kwa wananchi, kama vile wizara ya maji, afya, kilimo, elimu na mifugo zimepokea chini ya asilimia 50.

Kw amfano, wizara ya maji imepokea asilimia 11, wizara ya afya imepokea asilimia 14, kilimo imepokea asilimia 41, elimu imepokea asilimia 37 na mifugo imepokea asilimia 39.

“Kwa mwenendo huu, ukilinganisha na kasi ya ongezeko la watu, ni wazi kwamba kuna haja ya serikali kuzipa kipaumbele sekta hizi,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kitabu cha Kamati ya Bajeti kimepewa kichwa cha maneno kisemacho, “Taarifa ya mwaka kuhusu utekelezaji wa majukumu katika kipindi cha Januari 2018 hadi Januari 2019, pamoja na tathimini ya utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha nusu mwaka.”

Kamati imeagiza serikali kutekeleza mapendekezo kumi na tatu, ikiwamo la suala la kupeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo, pamoja na kuimarisha mahusiano na nchi wahisani.

error: Content is protected !!