January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Nchemba: Tanzania haitoacha kukopa

Mwigulu Nchemba

Spread the love

 

WAZIRI wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba  amesema serikali haiwezi kukwepa kukopa fedha kutoka nje ya nchi kwa kuwa bado inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea)

Pia amesema Tanzania imepiga hatua mbalimbali za kimaendeleo licha ya kupitia changamoto mbalimbali za kuyumba kwa uchumi tangu Tanganyika (Tanzania bara) ipate Uhuru mwaka 1961

Dk. Nchemba ametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Novemba, 2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni utaratibu wa kila wizara kuwasilisha taarifa yake kwa waandishi wa habari na kueleza mafanikio na changamoto toka kipindi cha miaka 60 ya Uhuru. 

Amesema tangu uhuru, uchumi wa Tanzania umepitia katika nyakati mbalimbali za mafanikio ya kiuchumi pamoja na changamoto kadhaa zikiwemo ukame katika miaka ya mwanzoni mwa 1970 na 2012.

Amesema changamoto nyingine ni mdororo wa uchumi wa mwaka 2008, vita vya Kagera mwaka 1978 pamoja na ugonjwa wa UVIKO mwaka 2020.

“Hata hivyo, Serikali kupitia mikakati mbalimbali iliweza kujikwamua kutokana na magumu hayo iliyopitia na hii iliwezesha katika historia ya Tanzania kutokuwa na ukuaji hasi wa uchumi  tangu uhuru.

“Takwimu zinaonesha kuwa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru ulikuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali lakini haujawahi kufikia ukuaji hasi.

“Wastani wa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha Serikali ya awamu ya kwanza (1967 – 1985) iliyoongozwa na mwasisi na Baba wa Taifa hili Hayati Mwalim Juluis Kambarage Nyerere ulikuwa asilimia 3.1, Serikali ya awamu ya pili (1986 – 1995) asilimia 3.0, Serikali ya awamu ya tatu (1996 – 2005) asilimia 5.7, Serikali ya awamu ya nne (2006 – 2015) asilimia 6.3, na Serikali ya awamu ya tano (2016 – 2020) asilimia 6.5.”ameeleza Mwigulu.

Akizungumzia mwaka 2020, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019.

Amesema sababu kuu ya kupungua kwa kasi ya ukuaji ni athari za hatua zilizochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani ambao ni washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania katika kukabiliana na janga la UVIKO-19.

Amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na mataifa hayo ni pamoja na kufunga mipaka, kusitisha safari za ndege za kimataifa na kusitisha baadhi ya shughuli za kiuchumi zinazohusisha mikusanyiko.

Amesema hatua hizo zilisababisha uchumi wa dunia kuporomoka mwaka 2020 ambapo nchi nyingi zilikuwa na ukuaji hasi na kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni nchi 11 tu zilikuwa na ukuaji chanya kati ya nchi 45.

Akizungumzia athari za janga la UVIKO-19 zilijitokeza zaidi katika shughuli za kiuchumi za malazi na huduma ya chakula pamoja na sanaa na burudani ambazo zilikuwa na ukuaji hasi mwaka 2020.

“Serikali ya awamu ya sita imeingia madarakani katika kipindi ambacho dunia bado inapambana na athari za kiuchumi na kijamii za janga la UVIKO-19.

“Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021, (Januari – Juni) uchumi umekua kwa asilimia 4.7 ikilinganishwa na asilimia 5.0 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

“Kupungua kwa kasi ya ukuaji katika kipindi hicho kumetokana na athari za UVIKO-19 katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Shughuli nyingi za kiuchumi zimeendelea kuwa na viwango chanya vya ukuaji katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021 ingawa kasi yake ilipungua ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2020” Ameeleza Mwigulu.

error: Content is protected !!