May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge ambana Majaliwa mpango kuwainua wanaume kiuchumi

Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haijafikiria kuanzisha mifuko ya kuwainua wanaume kiuchumi kwa kuwa wigo wa kupata mikopo upo lakini Serikali itaanzisha kama kutatokea umuhimu mkubwa wa kuanzisha mifuko hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Waziri mkuu ametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Novemba, 2021 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo (CCM).

Tarimo amesema sera ya kuwainua wananchi kiuchumi imekuwa na mafanikio katika mikopo inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu.

“Lakini tatizo hujitokeza kwa vijana wanapopewa mikopo kwani wakifikisha umri wa miaka 35, vijana wa kike wanaenda kwenye kundi la akina mama, vijana wa kiume wanabaki hawana cha kufanya Je, nini mpango wa serikali kuwainua wanaume kiuchumi kwa sababu sera inasema ni wananchi?.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanzisha mifuko kadhaa ambayo inawanufaisha Watanzania kulingana na eneo lile ambalo mfuko umeanzishwa.

“Tunatambua kwamba kundi la vijana limechanganya maeneo yote kwa sababu lengo ni vijana. Lakini iko mifuko ya wananchi wote ambao wananufaika na mifuko hii, pia tumejiunganisha na taasisi za kifedha ambazo yeyote anakuwa na fursa ya kwenda kukopa.

“Tuliposema vijana, wanawake na wenye mahitaji maalumu, Tarimo anafahamu kwamba sera ya nchi yetu tumeelekeza kumwezesha mtoto wa kike na wanawake kwa ujumla ili na wao waweze kuchangia pato la nchi hii kwa kufanya shughuli mbalimbali akipata mkopo anaweza kufanya biashara.

“Ukimwezesha mwanamke unakuwa umeliinua taifa, ukimuelimisha mwanamke unakuwa umelielimisha taifa, kwa hiyo tuwawekee eneo lao wanakuwa na uhuru mkubwa wa kukopa, anaweza kwenda kwenye mfuko wa halmashauri, benki, mifuko ipo mingi,” amesema.

Amesema hadi sasa ipo mifuko 42 ambayo Serika ina mpango wa kuipunguza ibaki michache ifahamike na kila mmoja aweze kwenda kukopa.

“Kwa hiyo bado hatujafikiria kuanzisha mifuko ya wanaume, lakini tayari wigo wa wanaume hao kupata mikopo upo kupitia mifuko hiyo na taasisi za fedha.

“Hapo baadae tukiona kuna umuhimu mkubwa kama kuna udhaifu tunaweza tukaanzisha, kadiri itakavyowezekana na sheria hizi na mifuko hii tunapoianzisha tunaileta kwenye kamati za bunge na kuona umuhimu wa kuanzisha hicho kitu,” amesema Majaliwa.

error: Content is protected !!