May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mpango ‘asaka’ dawa uvivu wa kulipa kodi

Spread the love

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango amesema, serikali iko mbioni kukamilisha utafiti kuhusu mwitikio mdogo wa walipakodi, kusajili biashara na uwazi katika utoaji wa taarifa za biashara. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Dk. Mpango ametoa kauli hiyo tarehe 11 Machi 2021, katika ukumbi wa Msekwa, jijini Dodoma wakati akieleza mikakati ya serikali katika kuimarisha ukusanyaji mapato.

Akiwasilisha mapendekezo ya serikali ya mpango, kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka wa 2021/2022, Dk. Mpango amesema, utafiti huo umewalenga zaidi wafanyabiashara wadogo.

“Serikali inakamilisha utafiti kuhusu visababishi muhimu vya kiwango cha chini cha uhiari wa walipa kodi kusajili biashara zao, ulipaji wa kodi kwa wakati na uwazi katika utoaji wa taarifa sahihi kuhusu biashara wanazofanya hususan kwa wafanyabiashara wadogo.

“Utafiti huu unahusisha kuchunguza changamoto  za kitaasisi, tabia sababishi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa,” amesema Dk. Mpango.

Pia amesema, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inatekeleza mradi wa kurejesha usimamizi wa mashine za ukusanyaji mapato za kielektroni (EFD), kutoka kwa mawakala.

“ Aidha, Mamlaka ya  Mapato Tanzania inatekeleza mradi wa kurejeshea kutoka kwa mawakala jukumu la  kusimamia EFD, ili kuongeza ufanisi katika usambazaji wa mashine hizo pamoja na utoaji wa huduma za kiufundi pindi mashine hizo zinapopata hitilafu,” amesema Dk. Mpango.

Sambamba na hilo, amesema serikali inapitia upya mfumo wa mapato na matumizi ili kuwezesha upatikanaji wa mapato yatakayokidhi ugharamiaji wa mahitaji ya serikali.

“Vile vile, serikali  inafanya mapitio ya mfumo wa mapato na matumizi kwa lengo la kuwezesha upatikanaji  wa mapato yatakayokidhi ugharamiaji wa mahitaji ya Serikali na hivyo kuwa na bajeti  endelevu,” amesema Dk. Mpango.

Akielezea hali ya ukusanyaji mapato kwa mwaka 2020/2021, Dk. Mpango amesema, katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021, serikali ilikusanya Sh. 17.1 trilioni kutoka katika vyanzo vyote vya mapato (ndani na nje).

Na kwamba, ni sawa na asilimia 87.7 ya makadirio ya ukusanyaji wa Sh. 19.5 trilioni.

“Mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia Sh. 12.0 trilion sawa na asilimia  87.9 ya lengo la kukusanya Sh.  13.7 trilioni. Kati ya mapato hayo,  mapato  yaliyokusanywa na TRA yalikuwa Sh.  10.4 tril.,  sawa na asilimia 88.3 ya lengo la kukusanya Sh.  11.7 trilioni,” amesema Dk. Mpango na kuongeza;

“Mapato yasiyo ya kodi  kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali yalikuwa Sh.  1.2 trilioni, sawa na asilimia 83.2 ya lengo la kukusanya Sh.  1.5 trilioni, na mapato ya  Mamlaka ya Serikali za Mitaa yalifikia Sh.  462.5 bilioni, ikiwa ni asilimia 93.1 ya  lengo la kukusanya Sh.  496.7 bilioni,” amesema.

error: Content is protected !!