Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali yaanika mwelekeo wa bajeti, deni la taifa lazidi kupaa
Habari za SiasaTangulizi

Serikali yaanika mwelekeo wa bajeti, deni la taifa lazidi kupaa

Spread the love

 

WAZIRI wa fedha na mipango wa Tanzania, Dk. Phillip Mpango amesema, serikali imekopa kiasi cha dola za Marekani 463.8 milioni (Sh. 1.1 trilioni), kutoka benki ya kigeni ya Standard Chartered (SCB), ili kugharamia miradi ya maendeleo. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza bungeni mjini Dodoma, jana Alhamisi, tarehe 11 Machi 2021, Dk. Mpango amesema, fedha hizo zimekopwa ili kugharamia ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa – Standard Gauge Railway (SGR).

Aidha, Dk. Mpango amesema, serikali inaendelea na majadiliano ya kupatiwa mkopo mwingine wa taktribani dola za Marekani 200 milioni, kutoka benki ya Credit Suisse AG, kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miundombinu.

Vilevile, Dk. Mpango amesema, majadiliano mengine yanaendelea na mabenki mbalimbali, ili kuwezesha serikali, kukopa kiasi chote kilichopangwa kwenye bajeti ya mwaka 2020/21, kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kauli ya Dk. Mpango, kuwa mradi wa ujenzi wa reli ya kati unahitaji mkopo kutoka mabenki ya biashara, inapingana na ile iliyowahi kutolewa na Rais John Magufuli, kuwa reli hiyo, inajengwa kwa fedha za ndani.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa reli hiyo, tarehe 14 Machi 2018, Rais Magufuli alisema, Tanzania ni nchi ya pekee barani Afrika, inayotekeleza mradi huo mkubwa kwa fedha za walipa kodi wake.

Alisema, “…hivi karibuni tulitembelewa na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na akashuhudia Tanzania tumetayarisha fedha zetu wenyewe, kwa nguvu zetu wenyewe, na walipa kodi ni Watanzania wenyewe, ambazo ni kiasi cha 2.8 trilioni.”

Alisema, “Uturuki itatupa mkopo wa masharti nafuu kwa awamu zingine za ujenzi, alisema Rais na kuongeza, “kwa hiyo Tanzania tunaweza.”

Katika mwaka wa fedha wa 2020 na 2021, serikali ya Rais John Magufuli, ilipanga kukopa kutoka kutoka taasisi mbalimbali za kifedha, mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, Dk. Mpango amesema, baadhi ya mikopo hiyo, imechelewa kupatikana kutokana na majadiliano yake, kuchukua muda mrefu na masharti magumu yanayotolewa na wakopeshaji.

Akizungumzia ustahamilivu wa deni la taifa, Dk. Mpango amesema, pamoja na serikali kuingia kwenye mikopo hiyo, bado deni la taifa, ni stahamilivu.

Amesema, “tathimini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba mwaka jana, yanaonesha kuwa deni la taifa, ni himilivu kwa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.”

Dk. Mpango ameliambia Bunge, kuwa deni hilo, limeongezeka kutoka Sh. 54.8 trilioni hadi kufikia Sh. 59.0 trilioni.

Amesema, hadi kufikia Desemba mwaka jana, deni la serikali lilikuwa Sh. 59.0 trililioni, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.6 ikilinganishwa na Sh. 54.8 trililioni, kipindi Desemba mwaka 2019.

Mkutano wa Bunge la bajeti, umeanza juzi Jumanne, ambapo wabunge watatumia kipindi cha wiki tatu, kuchambua mpango wa serikali, kutembelea baadhi ya miradi na kupitia bajeti za kila wizara na taasisi za serikali, kupitia kamati za kisekta za Bunge.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, kati ya fedha hizo, deni la nje limefikia Sh. 42.8 trililioni, huku deni la ndani, likifikia kiasi cha Sh. 16.2 trilioni.

Amedai ongezeko hilo limetokana na mikopo iliyogharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji.

Akiongea kwa kujiamini, Dk. Mpango amesema, katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, riba za mikopo imepungua kutoka asilimia 16.28 mwaka 2019 hadi ailimia 15.72 mwaka 2020.

Kwa upande wa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani na sarafu nyingine duniani, Dk. Mpango amesema, shilingi ya Tanzania, imeendelea kuwa tulivu.

Amesema, utulivu huo, umetokana na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti pamoja na kupungua kwa nakisi ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nje ya nchi.

Ameongeza, “tathimini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba mwaka jana, yanaonesha kuwa deni la taifa, ni himilivu kwa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.”

Katika mwaka huu wa fedha, Dk. Mpango amesema, serikali imepanga kuwekeza katika miradi ya kufua umeme wa megawati 2,115 kutoka bwawa la Nyerere; kuboresha shirika la ndege la taifa (ATCL) na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge.

Miradi mingine, ni ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Tanga hadi Uganda, makaa ya mawe ya mchuchuma na chuma cha Liganga, ikijumuisha ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga.

Maeneo mengine ambayo serikali imepanga kutekeleza miradi yake, ni uchakataji wa gesi asilia kutoka Lindi hadi Rumakali, uchimbaji wa madini ya Nickel; ujenzi wa madaraja makubwa na barabara za juu za Kigongo – Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam).

Aidha, serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa bandari ya uvuvi Mbegani, wilayani Bagamoyo, ununuzi wa meli za uvuvi; ujenzi wa kiwanda cha sukari mkulazi; utafutaji wa mafuta katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay North; mradi wa magadi soda – Engaruka na kuchochea uchumi shindani na shirikishi.

Hata hivyo, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21, taarifa ya Dk. Mpango inaonyesha kuwa urari wa malipo ya kawaida unaojumuisha biashara ya bidhaa, huduma, mapato ya vitega uchumi na uhamisho mali wa kawaida umeimarika kwa nakisi ya dola za Marekani 331.3 milioni kutoka nakisi ya dola 344.3 milioni katika kipindi kama hicho mwaka 2019/20.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

error: Content is protected !!