Saturday , 13 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CUF Maalim: Tunahofia Jaji ametishwa
Habari za SiasaTangulizi

CUF Maalim: Tunahofia Jaji ametishwa

Mahakama Kuu ya Tanzania
Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF), kinachoongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad, umedai kuwa kuna mkakati unaopangwa na baadhi ya maofisa wandamizi wa serikali, kumshinikiza Jaji Dk. Benhajj Masoud, kutoa maamuzi yatakayombeba Prof. Ibrahim Lipumba. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Taarifa ya chama hicho iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jioni hii, inaeleza kuwa sababu zilizotolewa leo mahakani kuhalalisha kusogeza mbele usomaji wa hukumu wa kesi iliyofunguliwa na baraza la wadhamini, hazikidhi mahitaji ya umma na hazijitoshelezi kisheria.

Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Mbarala Maharagande inasema, “…kutokuwapo kwa Jaji, hakuna uhusiano wowote na usomaji wa hukumu ambayo tumeambiwa kuwa tayari ilishaandaliwa.”

Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, leo tarehe 22 Februari, ilipanga kusoma hukumu katika shauri lili lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho kupinga Prof. Lipumba, kuwa mwenyekiti wake.

Hata hivyo, Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Sharmillah Sarwatt, aliwaambia viongozi, wafuasi na wanachama wa chama hicho, waliofurika kwenye ukumbi wa wazi Na. 1 (Open Court Room One), kuwa hukumu hiyo sasa itasomwa tarehe 17 Machi 2019.

Alisema, sababu za kusogezwa mbele kwa uamuzi huo, unatokana na Jaji Dk. Benhajj kupangiwa majukumu mengine nje ya ofisi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kalenda ya mwaka 2019, tarehe 17 Machi, inaangukia siku ya Jumapili; kwa mujibu wa sheria za Tanzania, siku ya Jumapili huwa ni mapumziko.

Kesi ya kuhoji uhalali wa uenyekiti wa Lipumba, ilifunguliwa na Bodi ya wadhamini ya chama hicho. Ilisainiwa na katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Washitakiwa wakuu katika shauri hilo, ni Prof. Lipumba na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.

Bodi halali ya CUF ilifungua shauri hilo, baada ya Prof. Lipumba, akisaidiwa na serikali, kutaka kurejea kwa nguvu kwenye uongozi wa chama hicho.

Prof. Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF kwa hiari, tarehe 6 Agosti 2015, kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa maelezo kuwa amekosa ushirikiano na viongozi wenzake.

Alisema, kwa namna chama kinavyokwenda, nafsi yake inamsuta kuendelea kuwa kiongozi. Akatangaza kung’atuka na kudai kuwa atabakia kuwa mwanachama muaminifu na iwapo chama kitaridhia anaweza kuwa mshauri wake.

Prof. Lipumba alishikilia uamuzi wake wa kujiuzulu licha ya kuombwa kutofanya hivyo na viongozi wenzake wa juu akiwemo Maalim Seif.

Maharagande anasema, “shauri hili lilikuwa limepangwa kutolewa hukumu tarehe 30 Oktoba 2018, lakini tukaelezwa kuwa hukumu bado haijakamilika. Ikapangwa 15 Januari 2019, serikali kupitia Mwanasheria Mkuu (AG), ikaomba ipewe muda ili iweze kujibu hoja nje ya muda

“Kwamba, leo tarehe 17 Machi, Naibu Msajili anaeleza kuwa Jaji amepangiwa majukumu mengine. Sisi katika CUF, tumeipokea taarifa hiyo kwa ukakasi mkubwa na kwa kweli, tumesikitishwa sana.”

Maharagande anasema, Naibu Msajili aliyekuja kuahirisha shauri na kulipanga Jumapili, ndiye huyo huyo ambaye wiki kadhaa zilizopita, alituhumiwa kukataa kupokea nyaraka za kesi iliyofunguliwa na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe na wenzake watano, dhdi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Katika shauri hilo, Zitto na wenzake walitaka Mahakama kutoa zuio la muda ili Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), asihojiwe na Kamati ya Kudumu ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

“Ni katika shauri hili, umma ulishuhudia mabishano makali kati ya Rais wa Jumuiya ya Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume na mhimili wa Mahakama. Tulimshuhdia Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, akitetea kitendo hicho cha Msajili,” ameeleza.

Aidha, CUF inasema, “ni Naibu Msajili huyu huyu (Sarwatt) ambaye taarifa za kuaminika zinaeleza tarehe 15 Februari 2019, alitoa kinyume cha utaratibu nakala ya hukumu kwa Lipumba kumwezesha kuchota takriban Sh. 1 bilioni za ruzuku ya CUF kutoka Benki ya NMB, tawi la Temeke, ambazo zilikuwa zimezuiliwa kwa amri ya Mahakama tangu mwezi Mei, 2018.”

Kufuatia utata ukakasi huo, taarifa ya chama hicho inahoji maswali kadhaa:

Inasema: “hapa tunaweza kusema ilikuwa bahati mbaya kwa Naibu Msajili Sarwatt kuwezesha utakatishaji huo wa fedha za umma ambazo zinatokana na kodi za Watanzania au kulikuwa na msukumo makhsusi wa nia ovu?

“Ni kweli kuwa Jaji ndiye aliyepanga/aliyetoa tarehe hii ya siku ya Jumapili au kuna namna ya wale ‘watu wasiojulikana’ wameingilia kati baada ya kutopendezwa na maamuzi yake ya  HAKI aliyoyatoa Jumatatu iliyopita ya tarehe 18 Februari 2019 ya kuifuta Bodi feki ya baraza la wadhamini ya Lipumba?

“Kama ni hivyo, iweje upande wa Lipumba wawe na taarifa siku moja kabla – 21 Februari 2019 – ya kutokuwepo maamuzi leo, kiasi cha kusambaza ujumbe na viongozi wao wote kutohudhuria mahakamani?

“Ni nani aliwapa taarifa hizo? Walikaa wapi kuratibu na kutekeleza hiki kilichotokea leo? Kwa jinsi Jaji Dk. Benhajj alivyokuwa na kasi ya kusikiliza na kutaka kumaliza kesi zote za CUF zilizokuwa mbele yake kwa wakati muafaka; kiasi cha kuamua kuzisikiliza mfululizo (session hearing), ni nani anayetaka KUMFUNGA SPEED GOVERNER kiasi cha kuhairisha hukumu mara tatu katika kipindi cha miezi 4 tangu kumalizika kusikilizwa?

“Ni kweli ilikuwa bahati mbaya Naibu Msajili kupanga kutolewa hukumu siku ya Jumapili ya Tarehe 17 Machi, 2019 au alikuwa na lengo la kuendeleza hairisha hairisha isiyokuwa na mwisho? Au muda huu kuna lipi linalopangwa kutekelezwa? Yamezingatiwa maelezo ya Lipumba aliyoyatoa jana 21 Februari 2019 alipozungumza na waandishi wa habari?

“Iweje kesi yenye maslahi mapana, yenye ufuatiliwaji mkubwa (Public Interest) na wananchi, viongozi wa CUF, wabunge, madiwani, na wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji nchi nzima inaendelea kuzungurushwa tangu mwaka 2016 mpaka sasa huku Lipumba akiendeleza uharibifu wa rasilimali za Chama?

“Si hivyo tu, anaendelea na wizi wa fedha za ruzuku, kuwavua uongozi na uanachama wabunge na Madiwani; na kusababisha vurugu na kushambulia Viongozi kila wanapohudhuria Mahakamani na wengine kufuatwa majumbani.

“Je, Mahakama haioni umuhimu wa kuyapa kipaumbele mashauri haya ili yaamuliwe mapema na mwenye HAKI apewe HAKI yake?”

Chama hicho kinamaliza taarifa yake kwa kuziomba mamlaka za Mahakama Kuu kuyapa uzito unaostahiki mashauri yote yanayokihusu chama hicho ili kuwezesha haki kutendeka kwa haraka.

Tazama video kamili hapo chini

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Nchimbi aanika ugonjwa wa CCM

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emanuel Nchimbi,...

Habari za Siasa

Chadema yapuliza kipyenga uchaguzi viongozi kanda

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza maandalizi ya uchaguzi...

Habari za Siasa

CCM :Hatutaki ushindi wa makandokando uchaguzi Serikali za mitaa

Spread the loveCHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakihitaji ushindi wa makandokando katika...

Habari za Siasa

Makala: Puuzeni wanasiasa wanaojigamba wanaweza kubadili maamuzi ya mahakama

Spread the loveKATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),...

error: Content is protected !!