December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Chongolo ateta na bodaboda, bajaji

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo

Spread the love

 

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewaahidi vijana 26 wa shina la namba tano la kata Kilimani mkoani Dodoma kwamba atazungumza na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan ili awapatie bodaboda zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi. Anaripoti Dnason Kaijage, Dodoma … (endelea).

Chongolo ametoa kauli hiyo leo tarehe 23 Aprili, 2022 wakati akizindua na kushiriki kupiga kura katika shina hilo ambalo linaundwa na madereva bodaboda na bajaji.

Aidha, Chongolo amewapongeza vijana hao kwa uamuzi wa kuanzisha tawi hilo huku akiwasisitiza kuwa litumike kwa kazi kusudiwa si vinginevyo.

“Lengo letu muwe na makazi bora nyinyi na familia zetu hivyo, nawaahidi nitamuomba Rais Samia awachangie bodaboda hesabu ya jioni itakayopatikana ni yenu mtagawana,” alisema.

Chongolo ameagiza baadhi ya viongozi wa mkoa wa Dodoma kwenda kuangalia kama vijana hao wanakopesheka ili wawaingize kwenye mikopo ya halmashauri.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ametoa rai kwa madereva hao ambao ni vijana kutumia shina hilo vizuri.

Kuhusu mikopo kwa vijana hao, Shekimweri amewataka kuunda kikundi na kukisajili kitakachowawezesha kupata mikopo na kuahidi kuwapa kipaumbele pindi watakapokamilisha shatri hilo.

Hata hivyo, katika uchaguzi huo wa shina namba tano lililopo Kata ya Kilimani, Juma Saigwa aliibuka kidedea katika nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 45 sawa na asilimia 90 ya kura zilizopigwa.

Nafasi ya Katibu ilichukuliwa na Maxmillian Mtabekwa huku wajumbe watatu waliopatikana katika uchaguzi huo ni Liana Danford, Regina Kalindo na John Msalika.

error: Content is protected !!