December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CHAUMMA nao wajiondoa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Hashim Rungwe, Mwenyekiti wa Chaumma

Spread the love

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), kimetangaza kutoshiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea). 

Uamuzi huo umetangazwa leo tarehe 9 Novemba 2019 na Hashim Rungwe, Mwenyekiti wa CHAUMMA Taifa, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam. 

Rungwe ameeleza kuwa, wamejitoa katika uchaguzi huo kwa kuwa mchakato wake ulikuwa na hila, kwa wagombea wa vyama vya upinzani.

“Tunashindwa, tunaona kwamba huu uchaguzi umetayarishwa kwa hila, kwamba wananchi wasishiriki. Tunaona kwamba uchaguzi huu umefanywa hila. Na sisi pia tunaamua hatutashiriki uchaguzi huu. Tunaomba wagombea wetu popote walipo wasishiriki,” ametangaza Rungwe.

Rungwe amesema wamefikia hatua hiyo, baada ya kuona jitihada zao za kutafuta suluhu kuhusu hujuma hizo, kugonga mwamba.

“Wanachama wote wafahamu huu uchaguzi una hila, tumekata rufaa lakini haijasaidia chochote. Kama wao ndio wanataka hivi, kwamba wale wana nguvu, wana dola, sisi hatuko tayari kupigana,” amesema Rungwe na kuongeza;

“Watanzania hatuko tayari kupigana. Hatuna tabia hiyo. Unatuzuia hatufanyi siasa. Sasa uchaguzi halali umeutangaza tumekuja kuchukua fomu, matatizo tunasumbuliwa, tumezirudisha zimekataliwa, tufanye nini.”

Rungwe amesema wananchi ambao ndio wapiga kura, wataamua la kufanya kuhusu uchaguzi.

Rungwe amesema CHAUMMA kilisimamisha wagombea zaidi ya 250, ambapo jiji la Dar es Salaam kilisimamisha wagombea 5, Morogoro (38), Iringa (30), Njombe (20) Tabora (38), Kigoma (10), Mwanza (25), Mara (40), Mtwara (7), Tanga 10 na Shinyanga (6).

CHAUMMA kinakuwa chama cha tatu kuususia uchaguzi huo, baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT- Wazalendo, kutangaza kujiondoa.

error: Content is protected !!