November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF wajitafakari kushiriki Uchaguzi Serikali za Mitaa

Prof. Ibrahim Lipumba

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kitafanya kikao, kwa ajili ya kujadili ushiriki wake katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajia kufanyika tarehe 24 Novemba 2019. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Hayo amesema Jafary Mneke, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi CUF, leo tarehe 9 Novemba 2019 wakati akizungumza na MwanaHALISI Online,  kwa njia ya simu.

Mneke amesema vikao vya chama hicho, ndiyo vitaamua kama CUF kitashiriki uchaguzi huo, au hakitashiriki.

“Msimamo wetu bado hatujautoa, vikao vya chama ndio vinatoa msimamo. Vitakaa mapema wiki ijayo, Jumanne ya tarehe 12 Novemba 2019,  jijini Dar es Salaam,” amesema Mneke.

Aidha, Mneke amesema hadi sasa wagombea wake walioenguliwa katika mchakato wa uteuzi wa kugombea uchaguzi huo, hawajarudishwa.

Mneke amesema, CUF kupitia Naftah Nachuma, Makamu Mwenyekiti wa CUF-Bara, na Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu CUF-Bara, walizungumza na Selemani Jafo, Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kwa ajili ya utatuzi wa changamoto hiyo, lakini haijafanyiwa kazi.

“Mawasiliano na Jafo yalifanyika tangu mwanzo, ya maandishi na hata viongozi wetu kuzungumza nae uso kwa uso, majibu aliyatoa, lakini hakutekeleza alichoahidi, ni muendelezo wa hujuma,” ameeleza Mneke.

Hadi sasa, vyama vitatu vya upinzani vimetangaza kususia uchaguzi huo, kwa maelezo kwamba wagombea wake walifanyiwa hujuma kwa kuenguliwa bila sababu za msingi.

Vyama hivyo ni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA).

Hata hivyo, vyama 11 visivyokuwa na uwakilishi bungeni, ikiwemo chama cha TLP, Sauti ya Umma (SAU), NRA, ADC, UDP, UMD na Demokrasia Makini, vimetangaza kushiriki uchaguzi huo.

error: Content is protected !!