Monday , 13 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema yalishukia Bunge kuhusu bei ya mafuta
Habari za Siasa

Chadema yalishukia Bunge kuhusu bei ya mafuta

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimehoji kwa nini Bunge limeshindwa kuisimamia Serikali katika kutatua changamoto ya kuadimika kwa Dola ya Marekani na ongezeko la bei ya mafuta ya petrol na dizeli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Swali hilo limeulizwa na Bunge la Wananchi la Chadema, leo Jumatatu, jijini Dar es Salaam likizungumzia changamoto ya kupanda kwa bei za bidhaa muhimu iliyotokana na kupanda kwa bei za mafuta na kuadimika kwa dola.

Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya bunge hilo, Tito Titalika, amesema kama mhimili huo ungetekeleza majukumu yake kwa ufanisi huenda Serikali ingechukua jitihada za haraka kutafuta muarobaini wake.

“Kwa nini Bunge limekuwa na kigugumizi kujadili hasa linapokuja suala la nishati ya mafuta? Limehitimisha shughuli zake wiki moja iliyopita lakini hakuna mjadala kuhusiana na jambo hili, Bunge lingejadili kwa kina pengine mjadala ungepelekea kuwajibika kwa wahusika,” amesema Titalika.

Akitoa mapendekezo juu ya namna ya kutatua changamoto hizo, Titalika ameitaka Serikali kufufua mpango wake wa uwekezaji katika nishati ya gesi asilia, ili ipatikane ya kutosha kwa lengo la kupunguza matumizi ya mafuta yanayoagizwa nje ya nchi kwa kutumia dola.

Titalika ameitaka Serikali itafute namna ya kupunguza uagizaji bidhaa za nje ya nchi, kwa kuwa suala hilo linapelekea kuongezeka kwa matumizi ya dola na kushusha thamani ya fedha ya nchi.

Ameshauri Serikali iweke mipango itakayosaidia uzalishaji wa mbolea nchini, kwa kuwa asilimia 70 ya mbolea inanunuliwa nje ya nchi kwa kutumia dola za Marekani.

Pia, ameishauri Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujikita katika kununua vito vya thamani ili dola itakapoadimika iviuze kwa ajili ya kupata akiba ya kutosha ya fedha hiyo.

Katika hatua nyingine, Titalika ameshauri Serikali ipunguze kasi ya ukuaji deni la taifa kwa kuwa kwa sasa inatumia dola nyingi kulihudumia.

“Zaidi ya asilimia 65 ya deni la taifa tunalipa kwa dola, kiwango hicho ni kikubwa na hii ina maana gani? maana yake unahitaji kulihudumia na kulipa deni kwa kutumia zaidi ya asilimia 20 ya makusanyo kulipa deni kwa dola. Serikali inatakiwa kupunguza kukopa kusiko na msingi,” amesema Titalika

Kwa upande wa changamoto ya kupanda bei ya mafuta, Titalika ameishauri Serikali kuondoa tozo ya Sh. 100 kwa kila lita ya petroli na dizeli, ili kupunguza gharama zake.

Naye Spika wa bunge hilo, Susan Lyimo, ameitaka Serikali kutumia vyema rasilimali za nchi katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Dk. Biteko: Serikali itaendelea kushirikiana na Red Cross

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Dk.Mpango aagiza trafki kuvaa makoti ya kamera kudhibiti rushwa

Spread the loveMakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk....

Habari za SiasaKimataifa

Palestina mwanachama wa 194 wa UN

Spread the loveBaraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa limepitisha kwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Vijana UVCCM Kagera wataka mwenyekiti wao ajiuzulu

Spread the loveVIJANA wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera wamemtaka Mwenyekiti...

error: Content is protected !!