KESI iliyofunguliwa na kampuni inayoandaa mapambano ya ngumi za kulipwa, Hall of Fame Boxing and Promotion, kuidai fidia ya zaidi ya Sh. 2 bilioni Kampuni ya Azam Media, imeahirishwa hadi tarehe 24 Oktoba 2023, kutokana na taratibu za kimahakama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 18 Septemba 2023 na Wakili wa waleta maombi, Winnie Kawandakamu, baada ya kesi ya madai Na. 100/2023, iliyopangwa kuanza kusikilizwa leo tarehe 18 Septemba 2023, katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Mussa Pomo, kuahirishwa.
“Kesi hii imetoka kwenye usuluhishi na usuluhishi umeshindikana hivyo tumekuja kuendelea mahakamani na kwa sababu za kimahakama na utaratibu wa kesi, kesi hii imeahirishwa hadi tarehe 24 Oktoba mwaka huu,” amesema Wakili Kawandakamu.
Kampuni ya Hall of Fame Boxing and Promotion, inadai Azam Media ilikiuka makubaliano ya kimkataba kwa kurusha maudhui kwenye kipindi, yaliyohusu mapambano mawili.
Mapambano hayo ni kati ya bondia Hassan Mwakinyo na rais wa Ufilipino, Arnel Tinampay na la Twaha Kiduku dhidi ya Dulla Mbabe, ambapo Azam Media inadaiwa kuyarusha bila ya kuwa na haki miliki ya maudhui hayo.
Inadaiwa kuwa makubaliano ya kimkataba yaliyokuwepo baina ya wadai hao na Azam Media ni kurusha mapambano hayo mubashara (live) tu, lakini iliendelea kurusha marudio mapambano hayo kwa nyakati tofauti, kinyume na makubaliano.
Kampuni hiyo inadai kurudiwa kwa maudhui hayo kuliendelea kuinufaisha Azam Media jambo ambalo linawasukuma kudai fidia hiyo. Pia, inadai Azam Media imerusha mapambano hayo bila kuweka nembo “logo” yake.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo ya ndondi, imefikia uamuzi wa kufungua kesi baada ya jitihada za kutafuta suluhu katika mamlaka mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA), kutozaa matunda.
Leave a comment