March 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bwawa la maji kujengwa Morogoro kupunguza uhaba

Spread the love

SERIKALI imekiri kuwa mji wa Manispaa ya Morogoro unakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa maji ya uhakika na kusababisha wananchi kukumbwa na hadha ya ukosefu wa maji. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Kauli hiyo ilitolewa leo bungeni na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso alipokuwa ajibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum Devotha Minja (Chadema).

Mbunge huyo katika swali la nyongeza alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuwapatia maji ya uhakika wananchi wa Manispaa ya Morogoro kutokana na bwawa la Mindu kukauka na kuwafanya wananchi hao kukosa maji.

“Upatikanaji wa maji katika manispaa Morogoro ni kizungu mkuti na hili linatokana na bwawa la Mindu kukauka na kusababisha maji kutojitoshelea je serikali ina mkakati gani wa kuchimba bwawa lingine kwa ajili ya kuwapatia maji ya kutosha wananchi wa Manispaa ya Morogoro,” amehoji Minja.

Awali katika Swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum, Silafu Maufi (CCM) alitaka kujua ni kwanini serikali haioni umuhimu wa kuanzisha mradi wa maji kutoka kwenye vyanzo vya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa ili kusambaza maji kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa na Katavi.

“ Kumekuwa na changamoto katika kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma pamoja na kuwa na Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa yako mikoa hiyo.

 “Je, serikali haioni umuhimu wa kuanzisha mradi wa maji kutoka kwenye vyanzo vya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa ili kusambaza maji kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa na Katavi,” amehoji mbunge huyo.

Akijibu maswali hayo, Aweso amesema kuwa ni kweli katika Halmashauri ya Morogoro kuna tatizo kubwa la maji lakini serikali inaangalia uwezekano wa kujenga bwawa lingine kwa lengo la kutatua changamoto hiyo ili wananchi wa Halmashauri ya Morogoro waweze kupata maji ya kutosha.

Kwa upande wa jibu la swali la msingi, Aweso amesema  kwa lengo la kuboresha huduma  ya maji kwa wananchi, serikali inameanza kutekeleza miradi ya kutoa maji katika maziwa makuu nchini kupeleka kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

Amesema katika mkoa wa Kigoma, serikali inatekeleza mradi unaogharimu kiasi cha Sh. 42 bilioni kutoka ziwa Tanganyika kwenda katika manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika  Julai mwaka huu.

error: Content is protected !!