June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo

Kilimo cha mpunga cha umwagiliaji

Spread the love

IMEELEZWA asilimia 80 ya watanzania nchini wanategemea kilimo kutokana na watu wengi kuendesha maisha yao ya kila siku na wengine kujipatia kipato kupitia kilimo hicho na kuongeza pato la taifa, anaandika Moses Mseti.

Kauli hiyo imetolewa leo na John Mongella, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, wakati wa makabidhiano ya jengo litakalotumika kwa ajili ya shughuli za kibenki kwa wakulima wa kanda ya ziwa na Francis Assenga, Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya kilimo na Maendeleo nchini.

Amesema kuwa sekta hiyo ya kilimo ambayo hubeba zaidi ya asilimia 80 ya Wananchi nchini sasa imepatiwa mkombozi na kuwaondolea changamoto mbalimbali ikiwemo za huduma za kibenki zilizokuwa zikiwakabili hapo awali.

“Kama mnavyo fahamu, sekta hii ina mnyororo mrefu, wapo wanaolima, wanaochakata mazao  na wapo pia wanao safirisha mazao kwenda nje ya nchi na wengine wanao leta mzao ndani ya nchi na wote hao wanategemea kilimo, ” amesema Mongella.

Hata hivyo, Mongella ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kutaka kuona watu wote wananufaika na kilimo ili kila mmoja aweze kuendesha maisha yake na kukuza uchumi wa taifa kupitia kilimo hicho ambacho alidai ni muhimu endapo kitasimamiwa vizuri.

Francis Assenga, Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Kilimo nchini, amesema shabaha yakufunguliwa kwa benki hiyo nikutaka kumkomboa mkulima kutoka katika kilimo cha kujikimu na kuingia kwenye kilimo cha kibiashara.

“Kutokana na hilo tukasema tuangalie sehemu ambayo ina matokeo ya haraka lakini eneo ambalo linachangia kwa kiwango kikubwa katika pato la taifa, tukaona Mwanza ni mahali sahihi kwa sasa kufunguliwa kwa tawi la Benki ya kilimo,” amesema Assenga.

Assenga amesema kilichowasukuma zaidi kuanza na kanda ya ziwa ni kanda hiyo kuwa na miradi mingi ya kilimo hasa wingi wa viwanda ambavyo vitatumika katika kusindika , kuchakata na kufanya kilimo cha biashara na kuwakomboa wakulima walio wengi.

Kwa upande wake, Meneja wa Majengo mkoa wa Mwanza, Mhandisi Yohana Mashausi, amesema wao wapo tayari kwaajili kuikabidhi benki ya wakulima jengo ambalo lilikuwa likitumiwa na Mamlaka ya mapato (TRA) hapo awali ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa wazi.

error: Content is protected !!